29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

KIGWANGALLA AWASILISHA BAJETI YA SH BILIONI 115

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameliomba Bunge limuidhinishie bajeti ya Sh bilioni 115.794, kwa mwaka wa fedha 2018/9, huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, ikitaka Serikali isitishe uwekaji wa vigingi vya mipaka katika maeneo ya hifadhi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nape Nnauye, akiwasilisha maoni ya kamati hiyo  baada ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18 kusomwa, alisema kumekuwa na migogoro mingi ya mipaka baina ya wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi.

“Kamati imetoa ushauri jinsi ya kumaliza migogoro hiyo lakini bado ipo na inazidi kuongezeka.

“Hivi sasa, Serikali inaendesha zoezi la kuweka vigingi katika mipaka ya hifadhi, jambo ambalo limepingwa na wananchi na kusababisha Serikali kutumia nguvu kubwa kutekeleza zoezi hilo.

“Kamati inaona moja ya changamoto kubwa inayosababisha migogoro ni Serikali kuweka mipaka bila kuwashirikisha wananchi kwani vigingi vingine vimewekwa katika maeneo ya shule na vingine ndani ya nyumba za watu.

“Kwa hiyo, Serikali isitishe mara moja zoezi la kuweka vigingi katika mipaka ya hifadhi, Serikali ifanye tathmini mpya ya maeneo yote yaliyohifadhiwa na wananchi washirikishwe katika zoezi hilo.

“Pia, Serikali ibainishe maeneo yote ambayo bado yana sifa ya kuendelea kuhifadhiwa na ambayo hayana mgogoro ili mipaka yake ibainishwe kwa kuwashirikisha wananchi na yale ambayo yamepoteza sifa ya kuwa hifadhi yapangiwe matumizi mengine.

“Mwisho, Serikali ijipe muda wa kumaliza migogoro hiyo vinginevyo itaendelea kuunda tume na kamati mbalimbali kumaliza tatizo,” alisema Nape.

Akizungumzia ongezeko la watalii nchini, Nape alisema kamati yake hairidhishwi na jinsi Serikali inavyotoa takwimu za utalii.

“Kwa mfano, takwimu zinaonyesha idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,284,279, mwaka 2016 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017.

“Lakini, takwimu hizo hazichanganui ni watalii wangapi walikuja nchini kwa ajili ya mapumziko katika hifadhi zetu, jambo ambalo halitoi picha halisi ya mwenendo wa ukuaji wa sekta hii.

“Pamoja na hayo, Machi 17, mwaka 2016, Serikali ilisitisha biashara ya wanyamapori hai nje ya nchi na kusababisha hali ya taharuki kwa wafanyabiashara hao.

“Chama cha Wasafirishaji Wanyama Hai Nje ya Nchi (TWEA), kilitoa malalamiko yake kwamba wakati Serikali ikisitisha biashara hiyo, wafanyabiashara hao walikuwa wamechukua mikopo benki, walikuwa wamelipia leseni na tozo mbalimbali za Serikali na walikuwa wakiwatunza wanyamapori waliokuwa wamewakamata kwa gharama kubwa wakisubiri kuwasafirisha nje.

“Serikali imechukua hatua mbalimbali kushughurikia malalamiko hayo ikiwa ni pamoja na kuahidi kuwalipa fidia ya gharama walizotumia kulipia leseni na tozo mbalimbali.

“Pamoja na ahadi hiyo, fidia hiyo bado haijalipwa na jambo hili limechukua muda mrefu na limesababisha mateso makubwa kwa wafanyabiashara.

“Kwa hiyo, kamati inaishauri Serikali iharakishe kuwalipa fidia zao ili waweze kujikimu kimaisha,” alisema Nape.

WAZIRI WA MALIASILI

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Kigwangalla alisema katika usimamizi wa sekta ya wanyamapori, Serikali imekubali kuwarudishia wafanyabiashara walioathirika kutokana na usitishwaji huo wa kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi.

Dk. Kigwangalla alisema Serikali imetenga Sh milioni 173.3 zitakazotumika kuwalipa wafanyabiashara hao.

“Pamoja na uamuzi huo, hatua inayofuata baada ya uhakiki kukamilika ni kufanya utafiti utakaoonyesha hali halisi ya wanyamapori na kushauri kuhusu biashara ya wanyapori hai.

“Kuhusu kupambana na kuzuia ujangili, wizara inaendelea kusimamia na kuratibu operesheni za kuzuia na kupambana na ujangili kupitia kikosi kazi kwa kushirikiana na Tanapa, NCAA, Tawa na TFC,” alisema Dk. Kigwangalla.

Kuhusu kutangaza utalii, alisema pamoja na mipango mingi iliyopo, wizara yake inashirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzisha chaneli maalumu katika Televisheni ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii.

“Aidha, wizara inaendelea na maandalizi ya kuanzisha studio ya utalii kwa njia ya teknolojia ya habari na mawasiliano,” alisema.

Kuhusu uwindaji wa kitalii, alisema vitalu vya uwindaji vipo 159 ambavyo kati yake vitalu 78 vimekodishwa kwa kampuni za kitalii na vitalu 81 vipo wazi.

Pamoja na hayo, Waziri Dk. Kigwangalla aliliomba Bunge liidhinishe Sh bilioni 115.794 kwa ajili ya shughuli za kawaida na shughuli za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/19.

MCHUNGAJI MSIGWA

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alimtaka waziri huyo awe makini katika utendaji kazi wake ili asije kuharibikiwa kama ilivyotokea kwa mmoja wa watangulizi wake, Khamis Kagasheki.

Kwa mujibu wa Mchungaji Msigwa, Kagasheki aliondoka madarakani baada ya kushindwa kudhibiti Operesheni Tokomeza iliyofanyika miaka kadhaa iliyopita kwa ajili ya kupambana na majangili na wavamizi wa hifadhi za wanyampori.

“Kwa bahati nzuri, nimefanya kazi na mawaziri waliowahi kuongoza wizara hii kama Ezekiel Maige, Khamis Kagasheki na sasa wewe mwenyewe Kigwangalla.

“Kagasheki aliondoka madarakani kwa sababu ya Operesheni Tokomeza na naamini baada ya kupewa nafasi ya kuongoza wizara hii, umejifunza kupitia yaliyompata Kagasheki.

“Kwa hiyo, nakuomba waziri utulie, hebu fanya kazi vizuri kwa sababu siku hizi nakuona umetuliatulia kidogo hauko kama zamani,” alisema Mchungaji Msigwa.

Katika hatua nyingine, Mchungaji Msigwa aliitaka Serikali irudishe fukwe za bahari katika Wizara ya Maliasili na Utalii badala ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilikohamishiwa.

Mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles