KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
MCHUNGUZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyika (44), anayeshtakiwa kwa Uhujumu Uchumi ikiwamo kushawishi rushwa ya zaidi ya Sh. Milioni 300, kupokea na kutakatisha Dola za Marekani 20,000 yuko katika mchakato wa kukiri makosa.
Kesi hiyo iliendeshwa kwa njia ya Mahakama Mtandao jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai upelelezi haujakamilika, ndugu wa mshtakiwa wanaendelea kufuatilia mazungumzo na DPP kuhusu mshtakiwa kukiri makosa yake.
Alidai mazungumzo yakikamilika upande wa Mashtaka utaijulisha Mahakama hivyo aliomba kesi iahirishwe. Hakimu Chaugu aliahirisha hadi Aprili 30 mwaka huu kwa kutajwa.
Mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Agosti 9, 2019 akidaiwa katika shtaka la kwanza kwamba, Februari 9, mwaka huo eneo la Upanga, mshtakiwa akiwa mwajiriwa na Takukuru kama Mchunguzi Mkuu, aliomba rushwa ya ShnMilioni 200 kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham kwa lengo la kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi tuhuma zilizokuwa chini ya uchunguzi wa mwajiri wake.
Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Februari 10,mwaka huu Viwanja vya Maonyesho ya Biashara, Sabasaba vilivyopo Temeke Jijini Dar es Salaam, alijipatia Dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Faizal Hasham kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi dhidi ya Hussein Gulamal Hasham zilizokuwa zinafanyiwa uchunguzi na Takukuru.
Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa Februari 13, mwaka huu katika ofisi za Makao Makuu ya Takukuru, mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru, alishawishi rushwa ya Dola za Marekani 50,000 kutoka kwa Thangavelu Nallavan Vall kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma zilizokuwa zinamkabili za kukwepa kodi zilizokuwa zinamkabili.
Katika shtaka la nne, inadaiwa kuwa Februari 14,mwaka huu mtaa wa Haile Selasie karibu na Merry Brown, Wilaya ya Kinondoni alishawishi rushwa ya Dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Nallavan Vall kama kishawishi cha kuharibu ushahidi uliokuwa chini ya uchunguzi wake dhidi ya kukwepa kodi.
Shtaka la tano, Februari 10, mwaka huu eneo la Sabasaba mshtakiwa akiwa mwajiriwa kama Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, anadawa alipokea Dola za Marekani 20,000 wakati akijua ni zao la kutakatisha na zimetokana na rushwa.
Katika shtaka la sita, ilidaiwa kuwa Februari 19,mwaka huu eneo la Village Super Market katika dula la kubadilishia fedha za kigeni la Electron, mshtakiwa alibadilisha sehemu ya Dola za Marekani 7,000 (alipata Sh. Milioni 16.1)kati ya 20,000 huku akijua ni zao la rushwa.
Katika shtaka la saba, ilidaiwa kuwa Februari 19, mwaka huu eneo la Chamazi Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alinunua ardhi eneo ambalo halijapimwa lenye thamani ya Sh. Milioni 15.8 huku akijua fedha hizo ni za kutakatisha na ni zao la rushwa.