Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Kesi ya matumizi mabaya ya inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando inatarajia kuanza kusikilizwa mfululizo Aprili 24Â na 25, mwaka huu.
Kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa imehamishiwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo leo Jumatano Machi 28, ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuleta mashahidi.
Hakimu Shaidi amesema mahakama itasikiliza kesi hiyo mfululizo siku mbili kuanzia Aprili 24 na 25 mwaka huu hivyo Jamhuri wanatakiwa kuita mashahidi wa kutosha siku hizo.
Tido anakabiliwa na mashtaka matano yakiwa matumizi mabaya ya madaraka ambapo Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa Mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.