23 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

JAMII INA WAJIBU KUSAIDIA MAPAMBANO YA FISTULA

Na MWANDISHI WETU

FISTULA si neno geni kwa wengi wetu, ingawa inawezekana tusijue maana halisi ya neno hili. Fistula ni tundu linalounganisha njia mbili za mwili zilizo wazi.

Kuna fistula za aina nyingi, lakini inayozungumziwa hapa ni fistula ya uzazi (obstetric fistula), ambayo ni tundu lisilo kawaida ambalo halikutakiwa kuwapo kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke (Vesico-Viginal Fistula – VVF) au kati ya njia ya haja kubwa na uke (Recto-Vaginal Fistula – RVF). Wanawake wengi hupata VVF, wachache RVF na wachache zaidi hupata zote kwa pamoja.

Inaelezwa kuwa, fistula mara nyingi hutokana na uzazi pingamizi (obstructed labour) wa muda mrefu, ambao haukuhudumiwa kwa wakati mwafaka.

Hali hii inapotokea kunakuwa na msuguano kati ya mfupa katika nyonga na kichwa cha mtoto unaopelekea jeraha katika njia ya haja kubwa au ndogo, ambalo baadaye hugeuka kuwa tundu.

Uzazi au uchungu pingamizi ni uzazi usioendelea aidha kwa sababu mtoto ni mkubwa kuliko njia ya uzazi, nyonga za mama kuwa na tatizo(aidha mama hakuwa na ukuaji mzuri kutokana na utapiamlo utotoni au ajali iliyoathiri nyonga) ama ulalo mbaya wa mtoto tumboni.

Upasuaji kwa ajili ya uzazi au matibabu mengine katika viungo vilivyopo maeneo ya nyonga huweza kusababisha fistula. Hii hutokea pale daktari ama kwa bahati mbaya ama uzembe anatoboa kuta za njia ya haja kubwa au ndogo ya mgonjwa na kusababisha fistula.

Benki ya NMB ni sehemu ya wadau muhimu katika mapambano ya ugonjwa wa fistula ambapo hivi karibuni, wafanyakazi wake waliwatembelea wagonjwa wa fistula wanaoendelea kupata matibabu katika Hospitali ya CCBRT, jijini Dar es Salaam.

Ugeni huo kutoka NMB kwa CCBRT, hasa Kitengo cha Fistulam ulikuwa wenye Baraka, kwani NMB ilikabidhi msaada wa Sh milioni 13 ili kusaidia mahitaji mbalimbali yanayotakiwa katika kuuguza kundi hili la akina mama amboa ni wahanga wa fistula.

Hafla hiyo imehudhuriwa na maofisa wa NMB kutoka Morogoro, Bagamoyo, Kibiti na Dar es Salaam.

Hospitali ya CCBRT ina kauli mbiu inayosema “Fistula Inatibika”, hii ni kutokana na ukweli kwamba, jamii imekuwa na mtazamo hasi juu ya mwanafamilia anapokutwa na dalili au kupata tatizo la fistula.

Familia nyingi zimekuwa zikichukulia tatizo hili kama laana au kuhisisha na mambo ya kishirikina na wengine kudhani kwamba ni ugonjwa ambao unasababishwa na mwanamke kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume zaidi ya mmoja.

Wengine wamekwenda mbali zaidi kufikiri kwamba, fistula ni mmoja ya magonjwa hatari ya zinaa na hauna tofauti na HIV.

Akizungumza na ugeni huo, Mkurugenzi Mkuu wa Uendeshaji wa Huduma CCBRT, Brendaali Msangi, anasema Fistula inatibika kwa kipindi kifupi pindi mgonjwa anapopatiwa matibabu stahiki.

“Fistula inatibika, tena kwa muda mfupi sana, inachukua wiki tatu hadi mwezi mmoja kutoka siku ya operesheni kwa mhanga wa fistula kupona na kuendelea na matibabu ili kupona kabisa.

“Tunapokea wagonjwa wengi sana kupitia mabalozi wetu ambao tunao katika jamii. Hii ni kutokana na watu wengi wamekuwa hawajui kama tatizo linatibika au wengine wamekuwa wakiona aibu kujitokeza ili watibiwe.

“Nina furaha kubwa sana leo tumeongeza idadi ya mabalozi wengine ambao ni NMB.  NMB ina matawi zaidi ya 213 nchi nzima, maofisa wa NMB watakuwa mabalozi  wazuri juu ya elimu waliyoipata hapa leo. Naomba nishukuru uongozi wa NMB kwa kuona umuhimu wa kusaidia kundi hili la akina mama, tunashukuru sana msaada huu utasaidia katika kukidhi mahitaji ya wagonjwa wa Fistula hapa CCBRT,” anasema Msangi.

Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki wa NMB, Aikansia Muro, anasema benki yao imejikita zaidi katika kusaidia jamii, hasa katika sekta ya elimu na afya.

“NMB imejikita zaidi katika kusaidia jamii inayoizunguka kwa kutoa msaada kwenye  sekta ya elimu, afya pamoja na majanga mbalimbali. Hivyo leo tumekuja CCBRT kutoa msaada wa shilingi milioni 13 ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kutatua changamoto za afya ambazo zinawakumba kina mama wengi, hasa wakati wa uzazi,” anasema Muro.

Kutokana na hali hiyo, anasema wanawajali wateja wao na wangependa kuona kina mama na watoto wanapata afya nzuri, kwa kuwa wanatambua watoto ndio Taifa la leo na kesho, ila wasipokuwa na usimamizi wa mama mwenye afya bora ni hakika hawatafikia malengo yao.

Kwa hali hii, imefika wakati sasa kwa jamii iondokane na dhana hiyo potofu, lakini pia wanajamii wote tunatakiwa kuwa mabalozi wazuri wa afya ya mama na mtoto kwa kuhakikisha usalama wao wakati wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,250FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles