Na JANETH MUSHI-ARUSHA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Arusha, imeendelea kuahirisha kesi inayomkabili Mmiliki wa Shule ya Lucky Vincent ya mjini hapa, Innocent Mushi, hadi Julai 5, mwaka huu kutokana na upelelezi kutokukamilika.
Mtuhumiwa huyo pamoja na mwenzake ambaye ni Mwalimu Mkuu Msaidizi, Longino Nkana, wanatuhumiwa kwa makosa ya usalama barabarani ikiwamo kusafirisha watoto bila kuwa na vibali muhimu.
Mushi aliburuzwa kwa mara ya kwanza Mei 12, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambapo anakabiliwa na mashtaka manne ya usalama barabarani.
Mbele ya Hakimu Desderi Kamugisha, Wakili wa Serikali, Alice Mtenga, aliiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyingine kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.
Watuhumiwa hao walikuwa wakitetewa na Wakili Method Kimomogoro ambapo Hakimu Kamugisha alikubaliana na wakili huyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 7, mwaka huu.
Awali wakisomewa mashtaka yao Mei 12, mwaka huu, Wakili wa Serikali, Rose Sule, alidai mtuhumiwa wa kwanza Mushi anakabiliwa na makosa manne wakati Nkana akituhumiwa kwa kosa moja.
Wakili Sule alidai kwamba Mushi akiwa Mkurugenzi wa Shule ya Lucky Vicent anatuhumiwa kuendesha gari la abiria bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji.
Alidai kuwa Mei 6, mwaka huu katika eneo la Kwamrombo wilayani Arusha, mtuhumiwa huyo alifanya shughuli ya usafirishaji wa abiria akiwa anamiliki gari aina ya Mitsubish Rossa T. 871 BYS.
Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa kosa la pili linamkabili mtuhumiwa huyo ni la kuruhusu kuendeshwa kwa gari bila kuwa na bima (Road Licence), ambapo Mei 6, mwaka huu aliruhusu gari hilo kuendeshwa huku akijua halina bima.
"Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiri wake ambapo Mei 6, mwaka huu ukiwa mmiliki wa gari hilo ulishindwa kuingia mkataba wa ajira na dereva wako Dismas Joseph Gasper ambaye kwa sasa ni marehemu,” alidai Wakili Sule alipokuwa akisoma mashtaka na kuongeza:
"Mtuhumiwa unakabiliwa na kosa la nne ambalo ni la kubeba abiria waliozidi zaidi ya 13 ambapo Mei 6, mwaka huu ukiwa Mkurugenzi, Ofisa Usafirishaji na mmiliki wa Lucky Vicent ulibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13, kinyume cha sheria,” alidai.