Na CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM
RAIS Dk.John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya 41 ya Biashara Kimataifa ya Sabasaba ambayo yanatarajiwa kuanza leo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema Rais Magufuli atafungua maonyesho hayo Julai Mosi mwaka huu.
Alisema suala la ulinzi na usalama limeimarishwa katika viwanja hivyo.
“Tumejipanga kuhakikisha maonyesho haya yanakuwa ya aina ambayo kamera zimeongezwa pamoja na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama ambavyo vitaongoza kamera hizo,” alisema Mwijage.
Alisema kaulimbiu ya maonyesho hayo mwaka huu ni ‘ukuzaji biashara kwa maendeleo ya viwanda’.
“Ukiwa na viwanda bidhaa unazozalisha zisiweze kuuzwa biashara itakufa,” alisema Mwijage.
Mbali na hilo Julai 6 mwaka huu itakuwa siku maalumu ya wafanyabiashara wa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema katika maonyesho ya mwaka huu nchi 30 zitashiriki na kutakuwa na mabanda maalumu yatakayoonyesha bidhaa za Afrika na kuwapo mabanda maalum likiwamo la asali na ngozi.
Alizitaja baadhi ya nchi zitakazoshiriki kuwa ni pamoja na Burundi China, DRC, Ujerumani, India, Japan na Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Uturuki, Marekani, Uingereza na Vietnam.
Alisema viingilio vya mwaka huu katika maonyesho hayo ni Sh1,000 kwa watoto na wakubwa ni Sh 3,000 na siku ya kilele Julai 7 kwa wakubwa kiingilio kitakuwa Sh 4,000.
Hata hivyo alisisitiza washiriki wa maonyesho hayo kuhakikisha wanakua na risiti za bidhaa wanazouza.
Aliwasihi wananchi watakaonunua bidhaa katika maonyesho hayo kudai risiti kuondokana.na.usumbufu unaoweza kujitokeza kutoka kwa walinzi na wakaguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), watakaokuwapo milangoni katika viwanja hivyo.