ANDREW MSECHU na AGATHA CHARLES -DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amesimulia namna polisi wanane walivyoshiriki mchezo mchafu wa kukamata watuhumiwa watatu waliokuwa wanasafirisha kilo 300 za dhahabu.
Dhahabu hiyo yenye thamani ya Sh bilioni 30 ilikamatwa Januari 4, mwaka huu jijini Mwanza ikisafirishwa kwenda wilayani Sengerema, huku watuhumiwa wakiwa na Sh milioni 305 zinazodaiwa kuwa zilikuwa ni kwa ajili ya kuhonga.
Akizungumza wakati wa kuwaapisha mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wa Tume ya Utumishi wa Umma, Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema baada ya kupata taarifa zilizohusisha rushwa katika ukamataji huo, aliamuru askari na watuhumiwa wote wakamatwe.
Rais Magufuli alisema japokuwa hataki kuingilia uchunguzi, anazo taarifa zote kwamba watuhumiwa hao wa usafirishaji dhahabu walikamatwa Januari 4, mwaka huu huko Misungwi na kurudishwa jijini Mwanza chini ya kikosi cha polisi kilichoongozwa na mrakibu msaidizi wa polisi wakiwa wanane na walifikishwa Kituo cha Kati, lakini hawakuwekwa ndani, ila waliishia katika gari.
Alisema ana taarifa kuwa wahalifu hao na polisi waliowakamata walifanya makubaliano, na polisi waliambiwa watapewa Sh bilioni moja, hivyo waliondoka nao kituoni usiku bila kutoa taarifa kwa yeyote, akiwamo RPC (Kamanda wa Polisi), ikidaiwa walipewa fedha za hongo.
“Polisi hao waliongozana na watuhumiwa hadi kwenye kivuko na kutoka Mwanza hadi Kamanga.
“Walitaka kulipwa Sh milioni 300 zilizobaki, walishapewa milioni 700 kwa kuwa walipewa milioni 300, baadaye milioni 400, baadaye walitaka wamaliziwe hizo milioni 300 ambazo waliambiwa watazikuta Sengerema,” alisema.
Alisema askari hao walikuwa wakiwasindikiza kwa kutumia gari ya polisi na mafuta ya Serikali, lakini wakiwa njiani taarifa zilimfikia mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela na yeye aliongea nao na kuwaagiza wawakamate.
“Watuhumiwa walipokamatwa pamoja na yule aliyekuwa akiwapelekea fedha kwenye gari, wale askari polisi waliokuwa wakiwasindikiza walipiga king’ora wakidai walikuwa wakiwafukuzia.
“Wewe uliwashika tangu jana hukupiga hata king’ora, ukakaa nao usiku kucha king’ora hakikulia, ukapanda nao kwenye kivuko ambacho kinajulikana, ukakaa nao kwenye gari na dhahabu zao hukupiga, ulipofika Sengerema umeona polisi wengine wako tayari kuwashika ukasema na sisi tulikuwa tunawafuatilia hawa.
“Ndiyo maana nikatoa maagizo kwa mkuu wa mkoa wanyang’anywe silaha wale askari wote wanane waliokuwa wakifuatilia, wapigwe pingu, warudishwe Mwanza na ndiyo maana wanahojiwa kisha wapelekwe kwenye mahakama za kijeshi, baadaye watapelekwa kwenye mahakama za kiraia,” alisema.
MTANZANIA LILIVYOVICHUA UTATA
Rais Magufuli ametoa kauli hii, ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti hili kuripoti kwa kina taarifa za kushikiliwa kwa askari saba kuhusiana na tukio hilo.
Katika taarifa hiyo iliyochapishwa Januari 8, mwaka huu, MTANZANIA lilieleza namna kulivyokuwa na mazingira ya utata baada ya polisi kuwatia nguvuni watuhumiwa.
Tulieleza kwa kina namna mazingira ya utata yalivyokuwa yamegubika ukamataji huo.
Katika taarifa hiyo MTANZANIA lilieleza kuwa inadaiwa askari baada ya kuwakamata watuhumiwa, walifanya nao majadiliano ya kupewa fedha ili wawaachie wasipelekwe kituoni.
Inadaiwa siku ya tukio, mpango wa mazungumzo na polisi na watuhumiwa hao ulisababisha wachelewe kupelekwa sehemu husika, baada ya mmoja wa watuhumiwa kudaiwa kwenda benki kuchukua fedha ambazo zilionekana kuvuka Sh milioni 50 kitendo ambacho kiliwafanya watumishi wa benki kutoa taarifa kwa uongozi wa mkoa na vyombo vya usalama kwa ufuatiliaji zaidi.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka nyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zilidai kuwa miongoni mwa askari waliowekwa chini ya ulinzi, yumo aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo na askari wengine sita.
KAMANDA SIRRO APONGEZWA
Kutokana na hali hiyo, alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kwa namna alivyoshughulikia suala hilo kwa kuwakamata, kisha kuwaweka ndani askari wote waliohusika.
Rais Magufuli alisema kama IGP Sirro asingechukua hatua hizo haraka angemhusisha na yeye kwenye tukio hilo.
Alisema alisimamia vizuri suala hilo kwa kuwa askari hao ni miongoni mwa askari wake wachache ambao si wema na wana nia ya kulichafua jeshi hilo.
Alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kudhibiti usafirishaji wa dhahabu katika utaratibu usiofaa kama lilivyofanya Mwanza na kuangalia pia usimamizi wa madini mengine yasitoroshwe.
CHANGAMOTO SEKTA YA MADINI
Rais Magufuli alisema sekta ya madini ina changamoto kubwa kwa sababu hata katika ripoti ya nchi za Afrika Mashariki inaonesha nchi inayoongoza kwa kuuza dhahabu siyo Tanzania wakati ndiyo yenye dhahabu nyingi.
Alisema hiyo inaonesha kuna mahali kuna udhaifu na Wizara ya Madini haiwezi kukwepa.
Rais Magufuli alisema kama Bunge limepitisha sheria nzuri na madini yapo, bado wizara haijawahi kuuliza mahali dhahabu inayopatikana nchini inapouzwa.
Alisema kuna maeneo mengi ambayo yametolewa kwa wachimbaji wadogo na wakubwa wa dhahabu, lakini wizara haijui wanapochimba wanauza wapi na kama wanauza haijui Serikali inapata asilimia ngapi kutokana na mauzo hayo.
“Kwa kuwa sheria tayari iko wazi, suala hilo ni la wizara na wala halihitaji Bunge au waziri mkuu kujiuliza kwa sababu wizara ipo na ina wataalamu, makatibu wakuu, makamishna, Tume ya Madini na watendaji wengi ambao wanatakiwa kusimamia majukumu yao kisawasawa,” alisema.
Rais Magufuli alisema inaonekana wizara haijawahi kujiuliza dhahabu inayopatikana inauzwa wapi.
“Ukimwambia mtu alime korosho si lazima ujue na soko lake liko wapi? Ukimwambia mtu alime mahindi pia lazima ujue soko lilipo, sasa hawa tumewaambia walime dhahabu, soko lao tunalijua la hao walimaji liko wapi?
“Kwahiyo unaona hii dhahabu bado haifaidishi kwa kiasi kikubwa nchi yetu, wajiulize ni kwanini?” alihoji.
Alisema sheria ya madini iliweka wazi namna ya kuingia mikataba na wawekezaji wakubwa na nchi nyingine, lakini iliweka pia namna ya kuwashirikisha wachimbaji wadogo katika suala la madini na soko la dhahabu na madini mengine, hivyo bado wizara haijaonesha inashirikije.
Alihoji kuhusu kuanzishwa kwa vituo vya madini kama sheria inavyoelekeza ambavyo hajui vimeanzishwa vingapi na viko wapi, hatua ambayo ingesaidia kufanya ufuatiliaji wa kiasi cha madini kilichozalishwa, kilichopokewa, kilichouzwa na hata kupata taarifa za kila wiki za kiasi cha dhahabu zilizouzwa kwenye vituo hivyo.
“Ni kitu gani kinachotushinda kama wizara, kama sheria ilishapitishwa na Bunge, wizara inayohusika imeshindwa kitu gani katika kuanzisha hizi?
“Nimelazimika kuzungumza haya ili ndugu zangu mjue ‘challenge’ tulizonazo kwa sababu inauma unaposikia kilo zaidi ya 300 zimekamatwa zikisafirishwa isivyo kawaida,” alisema.
Alisema japokuwa si maneno mazuri, inaonekana kuwa Tanzania ni nchi kubwa yenye madini na dhahabu za kutosha, ina watu hawajitambui japo ina wataalamu, majiolojia, wahandisi. Hivyo ataendelea kufanya mabadiliko kila wakati na kila atakayeshindwa kwenda na kasi yake ataondoka.
Rais Magufuli alisema huo ni ukweli ambao hataki kuuficha kwa sababu Serikali inahitaji fedha na rasilimali za Watanzania lazima ziwasaidie masikini katika kupata huduma za afya, elimu na nyingine,
Alimtaka Waziri mpya wa Madini, Dk. Dotto Biteko kuanza na suala la kuanzisha vituo vya madini na ikiwezekana akae na Wizara ya Fedha hasa Gavana wa Benki Kuu na kuanzisha utaratibu wa kununua na kuweka akiba ya dhahabu kwa kutumia fedha ilizonazo na kuweka hazina, ambayo ni hazina inayoweza kuhifadhiwa na kusaidia kwa kuwa dhahabu ni fedha.
Alitaka pia vituo hivyo vya madini vitakavyoanzishwa kusimamia mali ya Watanzania kwa kujua kiasi cha dhahabu kinachozalishwa, kuhifadhiwa na kuuzwa nchini kwa mwaka na kuitaka wizara husika kuamua pia kuhusu uwezekano wa kuchuja na kuzalisha dhahabu nchini, akiitaka kujipanga upya kushughulikia masilahi ya Watanzania.
Alisema ni vyema sana kufanya kitu hata ukikosea kuliko kuogopa kukosea kwa kulinda kazi yako kwa kuwa kwa kufanya hivyo utashindwa kuilinda hiyo kazi.
“Watendaji fanyeni kazi, mbuni kitu chochote ambacho mnafikiri mkikifanya hiki ni kwa masilahi mapana ya nchi. Hilo ndiyo ombi langu. Kwahiyo waziri wa madini, katibu mkuu na tume ya madini mkafanye kazi, siyo kazi yenu kutoa leseni tu,” alisema.
AZUNGUMZIA UTEUZI WA BITEKO
Akizungumzia uteuzi wa Biteko, alisema ulianzia pale Spika Job Ndugai alipomteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini na kuichachafya Serikali kwa namna alivyochangia.
“Alichangia michango yake kwa namna ya kuishauri Serikali, na baadaye lilipokuja suala la madini, ukaunda kamati, inayohusu madini, kuchunguza jinsi madini yetu yanavyoibiwa. Mmoja wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ukamchagua tena Biteko. Nikaanza kujiuliza kama Spika amemchaguachagua huyu, vipi huyu, ngoja na sisi tumwangalie aangalie huku.
“Ndiyo maana kamati ilipomaliza kutoa ripoti tukamchukua serikalini akawa naibu waziri, kafanya kazi, tumemwona anavyozunguka kwenye maeneo, na kwa kutambua Wizara ya Madini bado matatizo yapo, tukaona ngoja tumpe uwaziri kamili.
“Nenda ukafanye kazi ukishindwa nitakutoa, una uwezo ndiyo maana uko hapa, umebaki na naibu waziri mmoja mkachape kazi,” alisema.