29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Mapinduzi Zanzibar yalikuwa lazima kuleta uwiano wa maendeleo

JUMAMOSI Januari 12, Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea mwaka 1964 yatatimiza miaka 55 tangu kufanyika kwake na kuung’oa utawala wa kisultani na kuleta Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.


Kihistoria Mapinduzi hayo ni tukio muhimu lililong’oa ubaguzi visiwani lakini wapo wanaoyaona Mapinduzi hayo kuwa yalikuwa ni uvamizi dhidi ya serikali halali iliyokuwa madarakani kulikosababisha ukiukwaji wa haki za binadamu.


Kwa wale wanaoyaona Mapinduzi kuwa ni uvamizi dhidi ya serikali ni kutokana na madai ya kuwapo kwa washiriki ambao hawakuwa wenyeji wa Zanzibar, miongoni mwao ni John Okello ambaye kutokana na kuongoza Mapinduzi hayo alipewa cheo cha Field Marshal.


Okello anaelezwa kuwa aliingia Zanzibar mwaka 1963 na kuwasiliana na viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP).
Vijana hao wa ASP inaelezwa kuwa walikuwa wanajipanga kuangalia namna ya kuuondoa utawala wa Waarabu.


Inaelezwa kuwa usiku mmoja kabla ya Mapinduzi hayo, Okello aliwaamuru watu wake kuua vijana wote wa Kiarabu waliokuwa na umri kati ya miaka 18 na 25, lakini wasiwadhuru kinamama wajawazito na wazee na pia wasifanye ubakaji.


Januari 12, 1964 akiwa anaungwa mkono na asilimia kubwa ya watu waliokuwa wanakandamizwa – wengi wao wakiwa Waafrika – Okello na kikosi chake waliweza kuingia katika mji wa Stone Town, Zanzibar, ambalo lilikuwani maskani ya Sultan.


Inaelezwa kuwa takribani watu 10,000 waliuawa, licha ya kwamba kikosi cha Okello kilikuwa na silaha duni. Okello na kikosi chake walilishangaza Jeshi la Polisi Zanzibar na kuchukua ofisi zao.


Hali kadhalika inaelezwa kwenye hotuba yake iliyotangazwa kwa njia ya redio, Okello alitangaza kuwa yeye ni ‘Field Marshal wa Zanzibar na Pemba’ na alimwamuru Sultan aue familia yake na kisha ajiue mwenyewe, la sivyo Okello ataifanya kazi hiyo mwenyewe.


Hata hivyo, Sultani mwenyewe alikuwa tayari ameshajipatia maficho ya usalama nchini Uingereza na waziri mkuu pamoja na mawaziri wengine pia waliwahi kutoroka.


Hata hivyo kutokana na kufanikiwa kwa Mapinduzi hayo, Okello alitangaza Baraza la Mapinduzi na Sheikh Abeid Amani Karume kuwa Rais. Kiongozi wa Chama cha Umma, Abdulrahman Mohamed Babu, akawa Waziri mkuu. Baadaye alikuja kuwa Makamu wa Rais.


Sheikh Karume na Babu hawakuwa wamejulishwa kuhusu mapinduzi hayo ya kijeshi kwani wote walikuwa Tanganyika, lakini walirudi Zanzibar walikokaribishwa na Okello.


Lakini pamoja na shughuli yote aliyoifanya si Karume wala Babu waliomhitaji tena. Okello aliondoka kuelekea Tanganyika na kuanzia wakati huo alizuiwa kurudi Zanzibar na alipigwa marufuku pia asionekane Tanganyika na Kenya.


Baada ya Okello kupigwa marufuku Zanzibar na Tanganyika, aliishi maisha ya kuhamahama kutoka nchi moja hadi nyingine. Aliishi Kenya na baadaye Congo Kinshasa na Uganda. Aliwahi kufungwa mara kadhaa na mara ya mwisho alionekana akiwa na Kiongozi wa Uganda Idd Amin Dada mwaka 1971 na baadaye alipotea.


Katika kitabu cha ‘Revolution on Zanzibar’ kilichoandikwa na Don Petterson inadhaniwa kuwa Idi Amini alimwona Okello kuwa ni tishio kwake na mara nyingine inaelezwa kuwa baada ya Amin kujipandisha cheo na kuwa Filed Marshal, inaelezwa kuwa Okello alisema kwa dhihaka, “Uganda hivi sasa ina Field Marshal wawili.


Hata hivyo inaelezwa kuwa Idd Amini alipanga mipango ya mauaji dhidi ya Okello, lakini pamoja na hali hiyo kifo chake kimebakia kuwa cha utata.
Wapo wanaomuona Okello kuwa ni kama askari wa kukodiwa na ndio maana akatimuliwa. Mara zote askari wa kukodiwa wakimaliza kazi waliyolipwa kufanya huondoshwa haraka.


Yapo mawazo mengine kinzani kuhusu Mapinduzi kwamba hayastahili kufanyika lakini kwa walio wengi wanaona Mapinduzi hayo yalikuwa muhimu katika kuleta uwiano wa maendeleo kwa jamii ya Zanzibar.


Lakini katika mkondo wa historia wanaoyaona Mapinduzi hayo kuwa yalikuwa ni chanya ni kutokana na kutawaliwa kwa karne na kuifanya nchi kugawanyika kwa misingi ya kikabila, kiuchumi na kijamii na kuongozwa na mikwaju ya bakora na taratibu za utawala wa Kiingereza.


Jamii hiyo ilikuwa chini ya himaya ya Waingereza na utawala wa usultani wa Kiarabu kwa karne tatu pia ilipigana kwa uchungu kushinda chaguzi nne zilizokuwa na upendeleo kama ambavyo inaelezwa na Aboud Jumbe kwenye kitabu chake “Partnership: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Miaka 30 ya Dhoruba.”
Mapinduzi Daima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles