LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu Jakaya Kikwete, ameishauri Serikali na wamiliki wa hospitali kuangalia upya gharama za mazoezi tiba yanayotolewa kwa watoto wenye usonji ili kuwawezesha kupata huduma hiyo.
Kikwete alitoa ushauri huo Dar es Salaam juzi, alipozungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyolenga kuchagisha fedha za kuwasaidia watoto wenye ugonjwa huo unaoathiri mawasiliano na uhusiano na kusababisha changamoto kubwa katika malezi
Hafla hiyo iliandaliwa na taasisi ya Lukiza Autism Foundation.
Kikwete alisema kwa taarifa alizonazo kwa kila zoezi moja ambalo watoto hupashwa kufanyiwa, hugharimu Sh 20,000 kwa muda wa dakika 20 Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Sh 50,000 kwa dakika 45 hospitali binafsi.
Alisema ikiwa mtoto atafanyiwa mazoezi yote sita kila siku, mzazi atalazimika kulipa Sh 300,000 kwa wiki au milioni 1.2 kwa mwezi kwa gharama za Muhimbili.
“Haya mazoezi tiba ndiyo yanayowasaidia kupata nafuu, sasa gharama ni kubwa, ni matajiri pekee watakaomudu, lakini hata kwa familia tajiri labda kwa kina Mo (Mohamed Dewji).
“Tutafute namna ya kuzitazama gharama hizi. Na hili ni suala la kukaa wadau na Wizara ya Afya na hili litazamwe hata watu binafsi. Lakini kwa Muhimbili ambayo ni hospitali ya Serikali, lazima tulitazame hili kwa sababu na kodi zetu zinakwenda kule,” alisema Kikwete.
Pia alishauri wadau mbalimbali kusaidia upatikanaji wa basi maalumu la kuwapeleka shule watoto wenye usonji ili kuwaepusha wazazi wao na adha ya usafiri wanayokumbana nayo kwa kukataliwa kupanda kwenye usafiri wa umma unaobeba waru wengi kutokana na watoto hao kufanya vurugu pale wanapoingia.
Alisisitiza kufanyiwa kazi ushauri uliotolewa na mmoja wa walimu wanaowahudumia watoto wenye usonji wa Shule ya Msimbazi Mseto, aliyeshauri kuanzishwa kwa shule ya bweni ili kutoa nafasi kwa wazazi wao kuweza kufanya kazi za maendeleo kwani kwa sasa wanapowapeleka watoto wao shule hulazimika kusalia shuleni kuwangoja hadi masomo yamalizike.
Alisema pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya nchini kwa sasa ikilinganishwa na huko nyuma, ikiwamo kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba, lakini safari bado ni ndefu, hivyo juhudi zaidi zinahitajika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation, Hilda Lukiza alisema alipata wazo la kuanzisha taasisi hiyo baada ya kurejea nchini miaka mitano iliyopita akiwa na mwanaye aliyemzaa nje ya nchi akiwa na usonji na kukosa mahala pa kumpeleka ili kumwendeleza.
Alisema lengo la kuanzisha taasisi hiyo ni kutoa ushauri kwa watoto na wazazi ambao watoto wao hawana kiwango kikubwa cha ugonjwa huo pamoja na kutoa msaada wa hali na mali.
“Hapa nchini kuna Shule ya Msimbazi Mseto inayowalea watoto hawa, lakini baada ya kumaliza ‘primary’ hakuna pa kuwapeleka. Mwanangu alipaswa kuwa sekondari kwa sababu ana miaka 14, lakini hakuna sehemu ya kumwendeleza,” alisema Hilda.
Daktari bingwa wa watoto wa mfumo wa fahamu na ubongo na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dk. Edward Kija alisema ugonjwa huo huathiri zaidi uwezo wa kufanya mawasiliano kwa kuongea na vitendo, kutengeneza uhusiano na watu wanaomzunguka na kuwa na tabia ya kurudia rudia mambo.
Alisema tangu kugunduliwa kwa ugonjwa huo mwaka 1940, umeendelea kuongezeka kote duniani na kwa nchi ya Marekani katika kila watoto 59 wenye umri chini ya miaka 18 mmoja ana ugonjwa huo, huku utafuti wa kidunia ukionyesha kuwa katika kila watoto 132 wenye umri huo mmoja ana ugonjwa huo.