30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yatakiwa kuendelea kuwa na imani na mashirika, Asasi za kiraia

Na Hughes Dugilo, Dodoma

Jamii imetakiwa kuendelea kuwa na imani na Mashirika ya Asasi za Kiraia nchini zinazofanyakazi kubwa ya kuchagiza maendeleo yao katika kuhakikisha wanapata huduma bora za kijamii na kukua kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Oktoba 25, jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Francis Kiwanga alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mkutano maalumu uliokuwa ukizungumzia mchango wa Asasi za Kiraia katika Maendeleo ya nchi uliofanyika kwenye ukumbi wa mlima katika hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF na Mwenyekiti wa TANGO Anna Kulaya (kushoto) akiongoza mada kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 600 jijini Dodoma, (wa pili kushoto) ni Mkurugenzi wa FCS, Francis Kiwanga, (anaefuata) ni Mkurugenzi wa HLRC, Anna Henga, na (wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi wa ANSAF, Audax Lukonge.

Katika Mkutano huo uliokuwa na wazungumzaji watatu akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), Wakili Anna Henga na Mkurugenzi Mtendaji wa ANSAF, Audax Lukonge ulilenga kujadili mchango wa AZAKI katika kuleta maendeleo ya nchi.

Mbali na wazungumzaji hao pia umehudhuriwa na wajumbe zaidi ya 600, na kutoa fursa kwa wajumbe hao kujadili kwa kina namna ya kuboresha na kuendeleza ushirikiano wao katika kuihudumia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo huduma za kijamii, usawa wa kijinsia, haki za Binaadamu na mazingira pamoja na kuihamasisha jamii katika kujiletea maendeleo baina yao na Taifa kwa ujumla.

Akijibu swali lililoulizwa na muongozaji wa mkutano huo Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF na Mwenyekiti wa TANGO, Anna Kulaya kuhusu umuhimu wa AZAKI katika kuchangia na kukuza Maendeleo ya nchi, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga amesema kuwa eneo mojawapo ambalo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kuhakikisha wanajenga imani kwa jamii na serikali kwa kuzitambua kazi mbalimbali wanazozifanya katika kuielimisha jamii na kuihamasisha kuweza kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa ANSAF, Audax Rukonge akichangia mada katika Mkutano huo uliofanyika leo jijini Dodoma.

Amezitaka Asasi za kiraia ziendelee kujenga imani kwa jamii ambayo ndio nguzo yao kubwa nakwamba Asasi hizo ni daraja kati ya wananchi kuweza kupaza sauti zao kwa Serikali ili iweze kutatua changamoto zao mablimbali zinazowakabili.

“Eneo mojawapo ambalo tumefanikiwa zaidi ni hilo la kujenga imani na ndio maana unaona hata mwaka huu Serikali kwa kushirikiana na NaCoNGo wameweza kuendesha kongamano kubwa sana hata kuweza kumwita Mheshimiwa Rais ambae kwa maneno yake mwenyewe aliweza kutambua mchango wetu sisi kama AZAKI na kutupa hamasa zaidi ya nini tunaweza kuchangia zaidi ili kuweza kusongambele,” amesema Kiwanga.

Ameongeza kuwa imani ipo kubwa kwa serikali na kwa wananchi na hivyo kuwakumbusha wadau hao kuwa nguzo yao kubwa ipo kwa wananchi ambao kila siku wanajitahidi kuzipigania haki zao na huduma za kijamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), Anna Henga amesema kuwa Asasi za Kiraia zimesaidia sana kuweza kuisaidia jamii kwenye masuala ya kisheria na kutolea mifano mbalimbali ya namna ambavyo kituo chao kimeweza kuwasaidia wananchi waliopatwa na matatizo ya kisheria iliyowapelekea kukaa na kesi moja kwa miaka mingi bila kujua ni wapi wanaweza kwenda kupata msaada wa kisheria.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), Anna Henga akizungumzia mchango wa Asasi za Kiraia katika kutoa msaada wa Kisheria kwa wananchi.

“Mchango wa AZAKI katika utawala wa sheria ni mkubwa sana katika jamii yetu kwani hakuna mswada wowote unaenda Bungeni kabla ya kuupitia na kutoa mapendekezo yetu kama wadau hivyo tunaishukuru Serikali kwa kuutambua mchango wetu kwenye masula ya Kisheria,” amesema Anna.

Akichangia mada kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa ANSAF, Audax Rukonge amezishauri Asasi za Kiraia kuendesha shughuli zao kwa uwazi na uwajibikaji ili kuendelea kujenga imani yao kwa serikali na wananchi kwa ujumla nakwamba mchango wao ni mkubwa sana katika kuchangia uchumi wanchi.

“Kwa mfano sekta ya kilimo ni muhimu sana katika kuleta maendeleo ya nchi na imekuwa ni muhimili muhimu wa uchumi, sekta hii imekuwa na wazalishaji wengi wadogo ambao hawajiwezi wakiwemo wanawake, hivyo AZAKI imesaidia sana kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi kupitia kilimo hususani pembejeo za kilimo kama mbolea,” amesema Rukonge.

Ameongeza kuwa Asasi za Kiraia zisirudi nyuma katika kusaidia sekta ya kilimo nchini kwani ndio pekee iliyoajiri wananchi wengi ambao maisha yao yametegemea kilimo kuweza kujipatia kipato na kukuza uchumi wao.

Wiki ya AZAKI inaadhimishwa jijini Dodoma ambapo leo ni siku ya tatu tangu kuzinduliwa kwake na inatarajiwa kuhitimishwa Octoba 28 mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles