TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
Jamii imeshauriwa kushiriki kikamilifu katika kuwajengea mazingira wezeshi watumishi wa sekta ya afya kutoa huduma bila wao kuambukizwa magonjwa.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya usalama wa wafanyakazi wa sekta ya afya duniani iliyofanyika leo Alhamisi Septemba 17, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya Aga Khani ya jijini Dar es Salaam, Dk. Ahmed Jusabani amesema ni vyema kuongeza ufahamu na ushiriki wa wananchi katika kulinda usalama wa watumishi wa sekta ya afya ili kupunguza madhara kwa mgonjwa na mtoa huduma.
“Tunapoadhimisha siku hii jamii nzima inatakiwa kushiriki katika kuwalinda watoa huduma za afya ili kupunguza madhara kwa wagonjwa na anayemuhudumia,” amesema Dk. Jusabani.
Amesema wao wanaunga mkono mpango wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa utoaji huduma za afya kwa kuweka kipaumbele cha usalama wa wafanyakazi.
Amesema wakati watoa huduma za afya wanatekeleza majukumu yao ni vyema kuhakikishiwa na taasisi zao kuwapo na tahadhari ya kuepuka kupata maambukizi ya magonjwa
“Taasisi zinazoongoza zinatakiwa kutoa kipaumbele na kuchukua hatua za ziada kuwakinga wafanyakazi wake ikiwamo kuweka mpango ya wafanyakazi na kuwawekea bima kwa afya zao.
“Kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi tuliweza kutoa vifaa vya kujinga na ugonjwa wa Covid 19 kwa watumishi wa sekta ya afya katika hospitali za serikali,” amesema Dk. Jusabani.
Naye Mkurugenzi wa Wauguzi wa Hospitali hiyo, Aika Mongi amesema mlipuko wa virusi vya corona ulileta changamoto kubwa kwa watumishi wa sekta ya afya nchini na duniani kote.
“Wafanyakazi wa sekta ya afya walikabiliwa na hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo kutokana na kuuguza wagonjwa, kufanyiwa ukatili, ajali, unyanyapaa na hata wengine kupoteza maisha,” amesema Aika.