Faraja Masinde -Dar es Salaam
JAJI mstaafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Harold Nsekela amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Jaji Nsekela alifariki jana asubuhi jijini Dodoma baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kufuatia msiba huo mzito, Rais Dk. John Magufuli ametuma salamu za pole kwa familia, watumishi wote wa Sekretarieti ya Maadili na Mahakama.
Rais Magufuli aliandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa kiongozi huyo alikuwa muadilifu na mchapakazi asiyejikweza.
“Jaji mstaafu Nsekela alikuwa mwadilifu, mzalendo, asiyejikweza na mchapa kazi. Mungu amweke mahali pema Amina,” alisema Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Wasifu wa Jaji Nsekela
Jaji mstaafu Nsekela alizaliwa Oktoba 21, mwaka 1944, ambapo mwaka 1968 alitunukiwa Shahada ya Sheriakutoka Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki.
Mwaka 1970 alitunukiwa shahada ya Uzamivu (Master Degree) ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Yale cha nchini Marekani.
Uzoefu kazini
Kunzia mwaka 1968 hadi 1970 alikuwa Mkufunzi Msaidizi wa Mafunzo, Kitivo cha Chuo Kikuu cha Sheria cha Afrika Mashariki.
Kuanzia mwaka 1971 hadi 1974 alikuwa mkufunziwa Sheria katika Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kuanzia mwaka 1975 hadi 1976 alikuwa mkufunzi wa sharia za benki katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam.
Kuanzia mwaka 1976 hadi Mei 1977 alifanya kazi katika nyadhifa mbali mbali katika Shirika la Sheria la Tanzania na baadaye akaliongoza Shirika kama Wakili Mkuu wa Shirika kutoka 1986. Hili lilikuwa Shirika la Umma lililopewa jukumu la kutoa huduma za kisheria kwa Mashirika yote ya Umma nchini Tanzania.
Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania, Februari 2003 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Novemba 2006 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, baadaye Julai 2008, aliteuliwa kuwa Jaji, Idara ya Rufaa na Makamu wa Rais wa EACJ.
Novemba 2008 hadi Juni 25, 2014 aliteuliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Mei 2014 aliteuliwa kuwa Mwanachama Mshirika, Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania kabla ya Desemba, 2016 kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa Kamishna wa Maadilinafasi ambayo amedumu nayo hadi umauti unamkutajana jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, mipango ya mazishi itatolewa taarifa baadaye.