Na Mwandishi Wetu
Takriban watu 83 wamefariki dunia baada ya feri waliyokuwa wakisafiria kupinduka kwenye mto Tigris karibu na mji wa Mosul nchini Iraq.
Maafisa wa Serikali walisema kuwa zaidi ya watu 180 walikuwa kwenye kivuko hicho wakisherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa Kikurdi.
Inaelezwa kwamba wengi wa waathirika ni wanawake na watoto ambao walionekana kujaribu kuogelea kwenye mto huo ambao maji yake yalikuwa na kasi kubwa.
Viongozi wamesema shughuli za uokoji bado zinaendelea na tayari watu angalau 55, ikiwa ni pamoja na watoto 19, wameokolewa.
Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad umetuma salamu za rambirambi kwa jamaa za wahanga wa ajali hiyo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdul-Mahdi, ameamuru uchunguzi wa tukio zima ufanyike na kusema kuwa wale waliohusika watawajibishwa.