TEHRAN, IRAN
MAOFISA waandamizi wa Iran wamelikataa wazo la Rais wa Marekani, Donald Trump la mazungumzo na viongozi wa nchi hii pasipo masharti yoyote, wakisema halina msingi wowote na ni udhalilishaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, ameonya hatua hiyo ya Trump wanayoitafsiri kama ni njia ya kujitengenezea umaarufu haitafanikiwa.
Kwa upande mwingine, Rais wa Iran, Hassan Rouhani, alisema uamuzi wa Trump kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia, ulikuwa kinyume cha sheria na kuwa hawako tayari kukubali kirahisi kuruhusu juhudi za Marekani za kutaka kuvuruga uchumi wao unaotokana na mafuta.
Hayo yanajiri huku Trump akisisitiza kuwa mazungumzo kati yake na viongozi wa Iran lazima yafanyike, huku akiongeza kuwa ana hisia Iran itakuwa na mazungumzo na Marekani hivi karibuni.
Trump amerudia kauli yake kuwa makubaliano ya nyukilia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu aliyojitoa Mei mwaka huu yaliinufaisha zaidi nchi hiyo.
Alidai kuwa kwa sasa Iran iko katika wakati mgumu wakati Marekani ikitarajia kuiwekea vikwazo zaidi Iran kuanzia Agosti 6.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa waziri wake, Mike Pompeo naye anaunga mkono hoja ya Trump ya kutaka kuwa na mazungumzo na maofisa wa Iran.
Hata hivyo, viongozi wa Iran yakiwamo makundi ya wenye msimamo mkali, ambayo yalipinga vikali makubaliano hayo ya nyuklia, yameungana na Serikali kupinga mpango wa sasa wa Trump wa kukutana kwa mazungumzo.