LIVERPOOL, ENGLAND
BAADA ya klabu ya Manchester City kuchezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Liverpool, kocha Pep Guardiola, ameweka wazi kuwa wapinzani wake walikuwa katika ubora wa hali ya juu kwenye uwanja wao wa nyumbani Anfield.
Bao pekee ambalo lilipeleka huzuni katika Jiji la Manchester lilifungwa katika dakika ya 8 lililowekwa wavuni na Gini Wijnaldum na kuufanya mchezo huo kuzidi kuwa mgumu hadi dakika 90 zinamalizika.
Mbali na Manchester City kupokea kichapo hicho, Guardiola amedai kuwa mchezo huo wa kufungia mwaka ulikuwa sawa na timu yoyote ambayo ingekuwa ya kwanza kupata bao ingeshinda mchezo huo kama walivyofanya Liverpool.
“Mchezo ulikuwa sawa, tulianza vizuri huku tukiwa na lengo la kutafuta bao, lakini wapinzani wetu pia walikuwa na lengo hilo hilo na ndio maana mchezo ulionekana kuwa mgumu kwa pande zote na kuwa rahisi kwa pande zote.
“Najua historia ya Manchester City kwenye uwanja huu wa Anfield, lakini kwa upande mwingine wapinzani walikuwa katika ubora wao na ndio maana walitengeneza nafasi nyingi japokuwa hawakufanikiwa kuzitumia zote.
“Kipindi cha pili walikuja kwa kasi zaidi yetu, lakini baada ya dakika 10 tuliweza kubadilisha mchezo kidogo kwa kutengeneza baadhi ya nafasi lakini hatukuweza kufanya lolote, Liverpool ni miongoni mwa klabu bora nchini England, tulikuwa tunalijua hilo na ndio maana sijashtushwa na matokeo hayo,” alisema Guardiola.
Michezo mingine ambayo ilipigwa juzi ni pamoja na Swansea City ambao walikuwa nyumbani na kuchezea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Bournemouth, Southamton ikipigwa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya West Brom, huku Man United ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Middlesbrough, wakati huo Leicester City ikishinda bao 1-0 dhidi ya West Ham.
Vinara wa ligi hiyo, Chelsea, walifanikiwa kushinda mabao 4-2 dhidi ya Stoke City, huku Burnley ikishinda mabao 4-1 dhidi ya Sunderland.
Kwa upande wa kocha wa Chelsea, Antonio Conte, amewasisitiza wachezaji wake kuendelea kupambana hadi hatua ya mwisho ili waweze kutwaa ubingwa huo msimu huu. Hadi sasa klabu hiyo imeshinda jumla ya michezo 13, huku mara ya mwisho kupoteza mchezo wa Ligi Kuu ilikuwa Septemba 24, mwaka jana baada ya kuchezea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Arsenal.