27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

FIESTA ILIVYOHITIMISHWA DAR

Na MWANDISHI WETU


TAMASHA la Tigo Fiesta 2017, hatimaye limehitimishwa usiku wa kuamkia jana, ambapo wasanii waliopata nafasi ya kupanda jukwaani kwenye viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, walifanya shoo ya aina yake kufunga msimu wa tukio hilo kubwa la muziki na burudani nchini.

Umati wa wapenda burudani wa Dar es Salaam na vitongoji vyake, walijitokeza kwa wingi mno kupata burudani kutoka kwa vijana wao wa hapa nyumbani.

Hadi inafika saa 12 jioni juzi, viwanja hivyo tayari vilikuwa vimeshapendeza na hadi inafika saa 4:00 usiku, ilitosha kubaini ukubwa na ubora wa tamasha la Tigo Fiesta kwani wengi walijitokeza kupata uhondo kutoka kwa wasanii wao.

Ama kwa hakika Tigo Fiesta ya mwaka huu imethibitisha kuwa tamasha hilo si la kitoto baada ya kuhudhuriwa na watu wengi.

Katika tamasha hilo, wasanii waliopanda jukwaani walifanya kweli kwa kuhakikisha wanakata kiu ya wapenzi wa muziki nchini, lakini pia kuthibitisha ubora wao.

Kati ya matukio ya kukumbukwa katika tamasha la mwaka huu, ni suala zima la ulinzi kuanzia nje hadi ndani ya viwanja hivyo, ukiwamo ule wa njia ya CCTV zilizokuwa zimetegwa kila kona.

Lakini pia, kitendo cha msanii Jux kuwashirikisha wakongwe Q Chila na Kassim Mganga katika sehemu za harakati zake za ‘kurejeana’ na mpenzi wake wa zamani, Vanessa Mdee, kilivuta hisia za wengi na kuupendezesha mno usiku huo.

Mbali ya hilo, Bendi ya Yamoto ilijionyesha machoni kwa mashabiki waliofika Leaders Club baada ya kualikwa jukwaani hapo na aliyekuwa mmoja wa wanachama wake, Aslay, ambapo vijana hao walifanya kweli kwa kukumbushia enzi zao kiasi cha kushangiliwa mno.

Baadhi ya wasanii waliopanda katika jukwaa la Tigo Fiesta juzi ni Roza Ree, Bright, Chege, Mr. Blue, Aslay na Yamoto yake, Ali Kiba, Vanessa Mdee, Maua Sama, Mimi Mars, Rich Mavoko, Weusi, Rostam, Roma, Ben Pol, Barnaba, Darasa, Dogo Janja, Fid-Q, Nandy, Zaiid, Chin Beez, Nyandu Tozi, Ommy Dimpoz na wengineo.

Tamasha hilo limehitimishwa Dar es Salaam baada ya kuzunguka katika miji 16 ambayo ni Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mbeya, Moshi na Mtwara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles