NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), amekiri kupokea malalamiko kutoka pande mbili katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake na anayafanyia kazi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
“DPP amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa  washtakiwa na wahanga, anaiomba mahakama imvumilie wakati anafanyia kazi jalada hilo ili uamuzi atakaotoa uwe wa haki
“Jalada bado liko mikononi kwa DPP, nimelifuatilia bado linafanyiwa kazi, lina mambo mengi,” alidai Mwita.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo kwa sababu DPP analifanyia kazi jalada, hivyo apewe muda wa kutosha.
Hakimu Simba alisisitiza upande wa Jamhuri kuendelea kufuatilia jalada hilo na kesi iliahirshwa hadi Agosti 14, mwaka huu kwa kutajwa.
Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Revocatus Muyella.
Kwa pamoja wanadaiwa Mei 25, mwaka 2016 katika eneo la Kibada Kigamboni, Dar es Salaam, walimuua kwa makusudi dada wa bilionea Msuya, Aneth Msuya.