24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

DMDP kumaliza kero ya miundombinu Segerea

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wananchi wa Jimbo la Segerea wataondokana na kero ya miundombinu ya barabara baada ya kutekelezwa kwa awamu ya pili ya Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Hatua hiyo inatokana na barabara kadhaa za jimbo hilo kuingizwa katika mradi huo ikiwemo ya Mwananchi – Savana iliyopo Mtaa wa Kisiwani Kata ya Tabata ambayo imekuwa kero hasa nyakati za mvua.

Akizungumza Desemba 5,2023 baada ya kufanya ziara kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa utekelezaji wa mradi huo.

“Barabara za Jimbo la Segerea ni miongoni mwa barabara zilizopewa kipaumbele kwenye mradi wa DMDP awamu ya pili, barabara hii (Mwananchi – Savana) itajengwa kwa kiwango cha lami na kuondoa kero ya usafiri kutokana na kukatika mawasiliano hasa wakati wa mvua.

“Kwahiyo nawaomba wananchi kuweni wavumilivu, Serikali inatambua kero ya barabara hii na nyingine zilizoko katika jimbo letu,” amesema Bonnah.

Amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha barabara nyingi kuharibika na kwamba zile zilizopata athari wakandarasi watazirekebisha ili zipitike ikiwemo barabara ya Mwananchi – Savana.

Aidha katika Barabara ya Bonyokwa – Segerea, Bonnah amesema inajengwa kwa kiwango cha lami kupitia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura).

Amesema tayari mkandarasi yuko katika eneo la mradi na kwamba ujenzi wa barabara hiyo ulitarajiwa kukamilila Desemba mwaka huu.

Mbunge huyo ameiomba Tarura kuiingiza barabara ya zahanati iliyopo Kata ya Bonyokwa katika mfuko wa dharula ili ipitike wakati utaratibu wa kujengwa kwa kiwango cha zege ukiendelea.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amempongeza mbunge huyo kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kuwataka wananchi kuiamini serikali yao.

“Mbunge anafanya kazi kubwa kuhakikisha miundombinu inajengwa na kukamilika, ujenzi wa barabara utachochea maendeleo hivyo, tuiamini serikali yetu,” amesema Sidde.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Ilala, Mhandisi Sylivester Chinengwa, amesema barabara nyingi za jimbo hilo zitajengwa na kwa sasa kinachofanyika ni kurekebisha changamoto ya kukatika mawasiliano kwa kuweka mawe katika maeneo korofi hasa katika Barabara ya Mwananchi – Savana ili iendelee kupitika.

Kwa mujibu wa meneja huyo, Sh bilioni 5.5 zimetengwa na Tarura kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara wilayani humo kwa lami, changarawe na zege.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles