Na Dennis Luambano- Dar es Salaam
JUNI, mwaka jana niliandika kupitia safu hii ya kisa mkasa kwamba siasa za Kisiwa cha Zanzibar zina heri na shari yake!
Ndiyo, heri na shari hizo pia zimewahi kuchambuliwa na wabobezi wa sayansi ya siasa katika maandiko ya siku za nyuma.
Kwamba siasa za kisiwa hicho zina msukumo wa kihistoria wa enzi na enzi kwa hiyo kinachotokea sasa hivi si kigeni.
Kwa sababu katika miaka ya utawala wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Salmin Amour, kulikuwa na shari ya siasa za jino kwa jino na miaka 10 ya utawala wa Rais Mstaafu Amani Abeid Karume nako kulikuwa na vuguvugu la siasa za heri na shari.
Vivyo hivyo kwa kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein, kwamba heri ilitawala baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyojumuisha Chama cha Wananchi (CUF).
Pia kulikuwa na sintofahamu kubwa pale matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka juzi yalipofutwa Oktoba 28, mwaka jana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutokana na kasoro kadhaa alizozitaja baada ya aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Seif Sharif Hamad, alipojitangazia ushindi.
Hata baada ya uchaguzi huo kurudiwa Machi 20, mwaka jana hali imekuwa si shwari tena baada ya Seif kuanza kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ya kisiwani humo na kuwatangazia wafuasi wake kuwa Dk. Shein hatamaliza miaka mitano ya utawala wake kwa kuwa ataondolewa.
Akaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa mataifa ya nje yamewapa mbinu za kumwondoa Dk. Shein.
Wakati Seif amefanya ziara hizo, Dk. Shein, naye alipita katika maeneo hayo hayo kuzungumza na wafuasi, wakereketwa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kile kinachoonekana ni kujibu mapigo.
Kwamba alichokifanya Dk. Shein kwa wakati huo ni kufukia mashimo yaliyochimbwa na Seif katika maeneo hayo.
Ndiyo maana alinukuliwa akisema kuwa anayesababisha vurugu za kisiwani humo ni Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF kwa sababu bado anasaka urais kwa kutumia njia zisizokuwa halali.
Dk. Shein alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa nafasi ya urais haipatikani kwa vitisho, vurugu na migogoro bali inapatikana kwa kuchaguliwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia.
Kwa hiyo hakuna wa kumtisha na hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kumwondoa madarakani kwa sababu yupo kwa mujibu wa sheria.
Kwamba si mwanasiasa wala Jumuiya ya Kimataifa yenye uwezo wa kumwondoa madarakani kwa njia ya mkato.
Wakati hali ya mambo ikiwa hivyo, Jumapili wiki iliyopita Seif aliibuka tena na kusema kitendo cha yeye kukaa kimya ina maana kuna kishindo kinakuja Zanzibar.
Pia alikumbushia hoja yake kwamba kamwe hatarudi nyuma, kwa sababu hakushindwa katika uchaguzi huo.
Kauli hiyo aliitoa Unguja katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani wakati akimnadi mgombea wa chama hicho, Abdulrazak Khatib Ramadhan, anayepambana na mgombea wa CCM, Juma Ali Juma.
Naye Dk. Shein alinukuliwa Jumatano wiki hii akisema kuwa mvutano wake na Seif haukuwa mkubwa kiasi cha kuhitaji wapatanishi. Alisema mazungumzo ya mvutano huo yalianza vizuri, lakini yalikuja kukwama kwa hoja moja.
“Mazungumzo yalianza kwa hali nzuri, kuna mambo ambayo tulikubaliana, halafu hili la uchaguzi nikasema tume ikitangaza kuwa turudie mimi na chama changu tutakubali, lakini yeye akakataa,” alisema Dk. Shein.
Kuhusu ziara za Seif nje ya nchi kama zinatia doa Zanzibar na kuwatisha watawala juu ya mustakabali wa visiwa hivyo, alisema jambo hilo si kweli kwa sababu uchaguzi wa marudio ulifanywa kwa mujibu wa sheria na katiba ya visiwa hivyo, hivyo hakuna mahakama yoyote duniani inayoweza kuubatilisha.
Pia alisema mizozo baada ya uchaguzi ndani ya visiwa hivyo ni suala lililodumu kwa muda kabla ya kufanyika kwa mapinduzi na si jambo geni.
Hizo ndizo siasa za Zanzibar na huo ndio mwenendo wa maisha yao ya mara kwa mara, leo ikiwa heri, kesho inakuwa shari au vyote kwa wakati mmoja na kuthibitisha hoja yangu ni kile kinachoendelea sasa hivi kwamba Dk. Shein na Seif wote wamekita miguu chini.
Wanapambana majukwaani, mmoja akipita kushoto na mwingine anapita kulia. Yaani mafahari wawili wanapimana nguvu, mmoja ana dola mwingine hana dola.
Kupimana kwao ubavu kunasababisha huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi kuzorota miaka nenda rudi na kusababisha umasikini wa kutupwa katika kisiwa hicho ambacho ardhi yake haiongezeki licha ya kuhodhiwa na wajanja wachache huku watu wakizidi kuongezeka kila siku.
Ndiyo, utulivu wa kisiasa unapokosekana huku wakubwa wakiparurana ina maana hakuna kitakachoendelea kwa miaka mitano mfululizo na viashiria vyake katika hilo vimeshaanza kujionyesha.
Kwamba kuna taarifa zimeripotiwa hivi karibuni katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zinasema kuwa baadhi ya Wazanzibari wameanza kususana kisa wana itikadi tofauti za vyama vya siasa.
Mathalani kwa kuwa wewe ni mfuasi na mwanachama wa CUF, basi haununui bidhaa zinazouzwa na mwanachama wa CCM, pia hawezi kushiriki shughuli za maziko au harusi ya mtu anayetofautiana naye kiitikadi na kimsimamo.
Si ajabu au sitakuja kushangaa mbele ya safari pindi matukio ya mwaka 2001 ya watu kupigwa au visima vya maji ya kunywa kujazwa vinyesi yatakapojirudia.
Hayo ndiyo maisha wanayoishi sasa hivi! Yaani siasa kwao imekuwa kama dini kwamba atayekiuka au atakayekuwa tofauti na itikadi za vyama vyao ni lazima aadhibiwe kwa kisasi.
Mwendelezo wa hulka na tabia hizo za miaka nenda rudi ndizo zimesababisha maendeleo ya kisiwa hicho kudorora kulinganisha na visiwa vingine kwa sababu kila mmoja anataka kila siku awe mkubwa kwa mwenzake.
Kwa bahati mbaya, Seif ana amini bila yeye hakuna maendeleo katika kisiwa hicho ndiyo maana kwa muda mrefu sasa takribani miaka 20 amekuwa akipambana bila kuchoka kuwa Rais wa Zanzibar. Kwamba Seif amezaliwa kuwa rais wa kisiwa hicho na pengine anaamini umasikini wa kisiwa hicho unaletwa na watu na si mfumo.
Licha ya kuwahi kuwa makamu wa rais kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka juzi.
Kwa hiyo anataka aingie madarakani akiwa na mamlaka kamili ili aigeuze Zanzibar kuwa Dubai ya Afrika!
Ngoja tusubiri tuone na kama nilivyosema mwanzo kwamba wafuasi wa vyama vya CCM na CUF ndiyo wanaoumizana sasa hivi na ndiyo watakaoumizana mbele ya safari kutokana na Seif kujiapiza kwamba ushindi wake ulichakachuliwa huku Dk. Shein naye akizunguka kisiwani humo akisema yeye ndiye rais halali kwa sababu amechaguliwa katika uchaguzi wa kidemokrasia uliofuata misingi ya sheria.