29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

NI UKWELI AU HOFU YA KUDONDOSHA TONGE?

mtz10-23-3

Na EVANS MAGEGE,

MAZINGIRA yanaonyesha wazi kwamba mwenendo wa hofu umewasababisha hata wale wasema ukweli kushindwa kuusimamia ukweli wanaouamini mbele ya mtawala, iwe mchana, usiku, asubuhi na hata jioni.

Inawezekana hofu yao ya kulinda walichokitia kibindoni katika kumtaarifu mtawala ndiyo imesababisha washindwe kujenga hoja za kumfikirisha na kumpa picha halisi juu ya wimbi nyemelezi la baa la njaa ambalo linatishia maisha ya wananchi kwa sasa.

Wakuu wa mikoa na wilaya ni sehemu ya mhimili mkuu wa kumpatia taarifa mtawala juu ya uhalisia wa maisha ya kila siku ya wananchi. Sina uhakika kama wanafikisha taarifa za kina juu ya mwenendo wa hali ya njaa inayowakabili wananchi kwenye baadhi ya maeneo.

 

Kama wanafikisha taarifa za kina basi tukubali mtawala anajua kiwango au mwenendo wa njaa nchini, anayo ratiba ya nini atafanya na wakati gani atawasaidia wananchi wake.

Kwa mantiki hiyo tumaini pekee ambalo tunabaki nalo wananchi ni kwamba, kauli juu ya njaa alizozitoa Kagera na Simiyu ni majibu ya kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani na wafanyabiashara, lakini si kwa waathirika wa njaa kama wengi wetu tunavyofikiria kwa sasa.

Hakuna anayebisha kwamba mtawala ndiye tajiri wa taarifa kuliko mtu yeyote hapa nchini na inawezekana kiashirio cha kuja baa la njaa kakifahamu mapema kuliko sote, lakini swali la kujiuliza taarifa anazopata kwa sasa juu ya mwenendo wa njaa zina ukweli au ‘ukweli mchungu’ ambao unamchochea afanye uamuzi wa kufungua misaada kwa wananchi?

Inawezekana anapewa taarifa za kweli lakini zile za ukweli mchungu zinafifishwa ili yasije kuwakuta watoa taarifa kwa sababu dhana ya utumbuaji haina siku wala saa, haina anayejiamini wala asiyejiamini.

Wahenga wanasema kunguru mwoga hukimbiza bawa lake, kauli hii ninaweza kuinasibisha kwa yale ninayoyaona kwa watendaji wengi wa mtawala wa sasa kwamba wengi hawana ujasiri mkubwa wa kuusemea ukweli mchungu machoni mwake kwa manufaa ya jamii.

Tukirudi katika gurudumu la siasa ambazo wengi wanazihitaji na kupenda kuziona na kuzisikia hasa patapohitajika misaada ya kibinadamu (humanitarian aid) ni kuonyesha nia na si kupambana na nia.

Tafsiri ya ‘njaa’ ni hali ambayo mtu kwa kipindi fulani, hushindwa kula chakula cha kutosha kinachokidhi mahitaji yake ya mwili, hapo ndipo huinua macho juu na kumwangalia aliye juu yake kwa maana ya mtawala kwamba ana kipi cha msaada wa kunusuru maisha yake ili aione kesho na kesho izae siku nyingine kwa ujenzi wa Taifa?

Kihistoria inaonyesha baadhi ya watu duniani wamekuwa wakikabiliwa na vipindi virefu vya njaa na mara nyingi hali hii imekuwa inatokana na kuathiriwa kwa upatikanaji wa chakula kutokana na kuwapo kwa vita, magonjwa ambukizi na ukame.

Katika miongo kadha baada ya Vita Kuu ya Pili, maendeleo ya kiteknolojia na kuongezeka kwa maafikiano ya kisiasa baina ya mataifa, kulikuwapo matarajio ya kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na majanga ya njaa duniani.

Lakini wakati maendeleo ya kufikia matarajio haya yalikuwa yakisuasua ilipofika mwaka 2000 tishio kubwa la njaa lilipungua katika maeneo mengi duniani.

Takwimu za Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), zinasema takribani watu milioni 795 duniani hawana chakula cha kutosheleza kuishi maisha ya afya inayotakiwa, hiyo ni kama mtu mmoja katika kila watu tisa.

Na idadi kubwa inayofikia takribani asilimia 12.9 ya watu wote duniani, wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Kuna sababu nyingine kubwa kwanini hali hii hujitokeza katika nchi mbalimbali kama ilivyo Tanzania.

Charles Darwin, mwanasayansi aliyebobea katika elimu ya viumbe katika Karne ya 19 alitamka: “Iwapo machungu yanayowaandama watu masikini yanatokana na maamuzi ya asasi zetu na viongozi wake na si matakwa ya kiasili (dictates of nature) basi dhambi zetu ziwe kubwa mno.”

Na hili linadhihirika kila kukicha kwamba siku hizi umasikini husababishwa zaidi na maamuzi ya wale waliopo madarakani kuliko mambo mengine.

Mifuko mitupu, wahenga wamenena, haimrudishi mtu nyuma, bali vichwa na mioyo mitupu ndiyo hufanya hivyo.

Umasikini ni somo la ajabu sana na hasa kwa nchi tajiri duniani ambazo hutumia mabilioni ya dola kulisoma na kulielewa.

Na linapokuja suala la uwajibikaji siku hizi watu masikini mara nyingi hawathaminiwi tena.

Tanzania bado ni nchi masikini sana lakini wengi wanasena haikupaswa kuwa katika kiwango hiki cha umasikini zaidi ya nusu karne tangu uhuru.

Tumeshindwa kuzitumia rasilimali zetu madini ya kila aina, maziwa, mito mbuga za wanyama na vinginevyo kuleta angalau ahueni kwa wananchi.

Tumeshindwa kutumia maziwa yetu makuu na mito tuliyonayo katika kilimo cha umwagiliaji kujikinga na athari za ukame. Kwa mfano hakuna sababu ya watu kulia njaa kutokana na ukame uliyoyakumba maeneo mengi ya nchi wakati tunajivunia tumezungukwa na maziwa makuu.

Leo hii kumekuwa na taarifa ya kuwapo kwa nyemeleo la baa la njaa katika maeneo kadhaa nchini kutokana na ukame unaoendelea sehemu hizo wakati Serikali ikibaki na msimamo wa kutotambua hali hiyo.

Wiki iliyopita kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alitoa changamoto kwa Serikali akiitaka itangaze rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria.

Kauli hiyo aliitoa katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Nkome mkoani Geita kupitia chama chake.

Alisema hali ya chakula nchini si nzuri kwani wananchi wanashuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku.

Alitoa mfano wa unga wa sembe ambao bei ya sasa kwa kilo moja imefikia Sh 1,600 pale Morogoro na mchele kilo umefikia Sh 1,500 na kuvifanya vyakula vitokanavyo na mazao hayo mawili muhimu, yaani ugali na wali kuwa bei sawa.

Zitto alieleza kwamba, hali hiyo inatokana na kile alichokiita “uamuzi mbovu wa Serikali kuhusu hifadhi ya chakula.”

Alisema Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa, chakula hicho kiingie sokoni na hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) yana tani 90,000 tu za chakula wakati kwa kipindi kama hiki mwaka juzi lilikuwa na tani 450,000.

Aliongeza chakula kilichopo kwa sasa ndani ya ghala hizo kinatosha kwa wiki moja kwa mujibu wa takwimu katika taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mapitio ya uchumi ya Novemba, mwaka jana.

Wakati Zitto akisema hayo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, anasema Tanzania ina chakula cha kutosha na kwamba hawezi kutaja kiasi kutokana na kile alichokiita sababu za kiusalama.

Swali, kama Serikali ina chakula cha kutosha ni lini itaona umuhimu wa kukitoa kuwasaidia walioishiwa chakula?

Sababu ziko wazi matatizo ya tabia nchi yamesababisha ukosefu wa mvua mwaka huu. Maeneo mengi ni kame na watu walionyesha nia ya kulima lakini mazao yamekauka mashambani.

Inakuwaje mtawala aseme kwamba Tanzania haina njaa na wakati mazao yamekauka mashambani!?

Msaada kwa mwananchi ndani ya nchi yake si jambo la kubezwa kama siasa za majukwaani kwa sababu sehemu ya nguvu yake ndiyo ujenzi wa Taifa na ujenzi wa Taifa ndio maendeleo ya nchi.

Ni sahihi mtawala kusimamia ukweli na hata kuusemea ukweli mchungu, lakini wajibu wake kwa wananchi hauishii hapo tu bali uzito wa nafasi yake na taasisi yake ni mfariji mkuu kwa wananchi wake.

Hata kama anasema ukweli wa kuwafurahisha wote, lakini ana wajibu wa kupima uzito wa ukweli huo kwa saikolojia ya waliopoteza mazao kwa ukame.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu  Lissu, ameonyesha kutoridhishwa na kauli za mtawala kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera pamoja na uwepo wa dalili za ukame ambazo zinazua hofu ya njaa.

“Kwa historia, nchi hii imekumbwa na njaa mwaka 1963 na 1987 na Mwalimu Julius Nyerere hakuona aibu kwenda kuomba chakula Marekani ili watu wasife na njaa,” Lissu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles