Na MWANDISHI WETU-DODOMA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, amewataka Watanzania waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) huku wakimtanguliza Mungu.
Ametoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na viongozi wa dini mbalimbali walioshiriki maombi maalumu ya kitaifa kwa Mkoa wa Dodoma dhidi ya Covid-19 yaliyofanyika ukumbi wa Chuo cha Veta, Dodoma.
“Hakuna njia nyingine yoyote isipokuwa kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu. Tuendelee kuchukua tahadhari wakati bado tunaendelea kumtumainia Mungu. Ni heri kumwishia Mungu, na Roho Mtakatifu atatupa njia ya kutoka hapa tulipo,” alisema Dk. Mwanjelwa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inaongozwa na Rais Dk. John Magufuli ambaye ana hofu ya Mungu na ndiyo maana aliomba Watanzania kwa imani zao wafanye maombi kwa siku tatu.
Dk. Mwanjelwa alisema Serikali inatambua mchango wa viongozi wa kiroho na akawataka waliombee taifa kwani mwaka huu linajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu.
“Mwaka huu tunatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu, kwa hiyo tunaomba tumtangulize rais wetu, tumwombee sana kwa yale anayoyafanya kwa nchi yetu,” alisema Dk. Mwanjelwa.
Akizungumza wakati wa kufungua maombi hayo, Rais wa Chama cha Maaskofu na Wachungaji (Tanzania Pastors’ Association – TPA), Askofu Samson Mlawi alitoa maombi akimwomba Mungu aifute Covid-19 kwenye mipaka ya Tanzania.
Naye mwakilishi wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Kisusu Mvumbo alisema dunia huwa inaandika historia kila kunapotokea tukio kubwa akitolea mfano wa vita kuu ya dunia.
“Vita ya kwanza ya dunia iliandika historia, ikaja vita ya pili ya dunia nayo ikapita.
“Sasa hivi, tishio juu ya mdudu huyu corona pia inaendelea. Dunia haiendi, imesimama, imekwama kiuchumi sababu ya mdudu corona. Tumsihi Mwenyezi Mungu atuepushe na hili janga,” alisema Sheikh Mvumbo katika maombi yake.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka madhehebu ya Khoja Shia Mkoa wa Dodoma, Ustaadh Haidary Bakari alisema anamwomba Mungu aiponye Tanzania na pia akaombea Uchaguzi Mkuu ujao uwe wa heri na amani.
Akimalizia maombi hayo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Maombezi wa Wanawake Barani Afrika, Profesa Margareth Kilimali alisema anamshukuru Mungu kwa kuwakutanisha viongozi hao wa dini wa Mkoa wa Dodoma bila kujali tofauti zao za dini.
“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa ana uwezo wa kutokomeza janga hili kwa nchi yetu ya Tanzania na bara zima la Afrika. Asante kwa fursa ya Uchaguzi Mkuu kwani umeshapanga ni jinsi gani utaendeshwa kwa amani wakati ukifika,” alisema Profesa Kilimali.
Alisema Tanzania haitaaibika na janga la corona kwa sababu imemtumaini Mungu.
“Tanzania haitaaibika kwa sababu tumekujua wewe ni Mungu na unaweza kutuponya, Afrika haitaaibika kwa sababu nao wamekukimbilia wewe,” alisema Profesa Kilimali.
Wakati huohuo, Mratibu wa TPA, Askofu Gerald Nzwalla alisema neno kuu la maombi hayo ya kitaifa limetoka nyakati wa pili, sura ya saba mstari wa 14 na wa 15 (2Nya.7: 14-15) na waliona ni muhimu maombi hayo yafanyike jijini Dodoma kwa sababu ni makao mkuu ya nchi na ndipo mahali anaishi Rais wa nchi.
Maombi hayo maalumu yaliandaliwa na TPA kwa kushirikiana na Bakwata, Shia, Hamadia, Hindu, Aga Khan, KKKT, EAGT, FPCT, Menonite na Morovian.