31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango kuongoza mapokezi ya ndege

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango kesho Oktoba 3, anatarajia kuwaongoza Watanzania kupokea ndege mpya aina ya Boeing 737 MAX 9 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) yenye uwezo wa kubeba abiria 181.

Aidha, Dk. Mpango anatarajia kukabidhi ndege mbili za injini moja aina ya Cessna Skyhawk 172 kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), lengo likiwa ni kuendeleza Kituo cha Umahiri katika Uendeshaji wa Usafiri wa Anga na Usafirishaji.

Akizungumza leo Oktoba 2, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuhusu ujio wa ndege hiyo na zile za mafunzo amesema mwaka 2021 Serikali iliiwezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege mbili ndogo za mafunzo ya urubani aina ya Cessna Skyhawk 172 zinazotumia injini moja.

“Zilikuja katika vipande vidogo vidogo zikaunganishwa hapa kisha ndiyo unapata hizi ndege. Kila moja inaweza kubeba watu wanne ikijumlisha rubani zitatumia mfumo wa kisasa ambao unamuwezesha rubani kuratibu taarifa kiurahisi na hivyo kuongeza umakini na usalama wakati wa urushaji wa ndege,” amesema Prof. Mbarawa.

Amesema ndege hizo zilitengenezwa na Kampuni yaTextron Aviation ya Marekani, ziliwasili nchini Januari mwaka huu zikiwa zimevunjwa, kwa sasa zimekamilika kuundwa na zipo tayari kuzinduliwa na tayari kwa kuanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa urubani.

Amesema chuo hicho kitatumia ndege hizo kutoa mafunzo ya urubani kwa daraja la awali ambayo yatachukua miezi sita na ya leseni ya CPL yatachukua miezi 12 kwa gharama ndogo ikilinganishwa na gharama za mafunzo hayo nje ya nchi.

“Kwa wastani kwa mwanafunzi mmoja kwa kozi zote mbili takribani Sh milioni 300 zilikuwa zikitumika, lakini kwa kuja ndege ndogo hizi bei itashuka sana kwa kuwa ndege moja inaweza kufundisha wanafunzi watano, chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 10 kwa wakati mmoja,” amesma.

Aidha, kuhusu ndege mpya ya ATCL amesema itachukua abiria 181, ambapo ndege hiyo ina madaraja mawili, la abiria 165 na daraja la abiria 16, ujio huo wa ndege hiyo ATCL itafikisha ndege 14 mpya.

Amesema ujio huo wa ndege itawezesha vituo vya Pemba, Tanga, Mbeya, Nachingwea na Musoma, ambapo itatengeneza mruko wa ndege saa za usiku, huku leo Oktoba 2, wakitarajia kuanzisha safari za usiku mkoani Dodoma.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi, Biseko Chiganga alisema Serikali imewapa NIT eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kujenga hanger ambayo itatumika kwa masomo ya urubani wakiwemo marubani.

“NIT itajenga shule ya urubani KIA na kwa wakati huo chuo kitakuwa kinatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa mafunzo ya vitendo,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wananchi kujitokeze kuipokea ndege hiyo ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi anayofanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles