Na MWANDISHI WETU
BENKI ya ABC imeendelea kupanua wingo wake kwa kufungua tawi jipya Tegeta, Dar es Salaam kwa lengo la kuhudumia ongezeko kubwa la wateja katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tawi hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema ni uamuzi mzuri kwa kupeleka huduma za kibenki katika maeneo ya nje ya jiji, kwani huduma nyingi zinapatikana maeneo ya mjini.
“Nachukua fursa hii kuupongeza uongozi wa Benki ya ABC kwa kuja na mbinu ya kufungua tawi lenu Tegeta. Ni vizuri kufahamu maeneo kama haya ndiyo yenye Watanzania wengi ambao wanahitaji huduma za kibenki,” alisema Mpango.
Kuhusu huduma zitolewazo na benki hiyo, Dk. Mpango alionyesha kuridhishwa na taarifa kwamba zaidi ya wafanyakazi 60,000 wa Serikali wananufaika na mikopo na fursa ya kuwekeza.
“Kwa jinsi mnavyohudumia wafanyakazi wa Serikali, fanyeni hivyo hivyo kwa sekta binafsi na watawaamini na kutumia huduma zenu,” alisema.
Alitoa wito kwa Watanzania kujiwekea utaratibu wa kuweka akiba, kwani ndio njia pekee mtu kutimiza malengo yake.
“Kuweka akiba kuna faida nyingi zikiwamo kufikia malengo, inajenga imani kwa benki pale mtu atapohitaji kupata mkopo,” alisema.
Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa benki hiyo na taasisi nyingine za fedha kufikiria namna ya kupunguza riba ya mikopo, kwani Watanzania wengi ambao wamekuwa na nia ya kukopa, wanashindwa kutokana na riba kubwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABC, Dana Botha, alisema ufunguzi wa tawi hilo ni hatua kubwa ya kuleta huduma za kibenki karibu na wananchi.