31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

DK. KIGWANGALA ATOA TISHIO JIPYA ARUSHA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala, amesema wamiliki wa majumba ya kifahari 83 wanaodaiwa kujenga katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA) eneo la Njiro jijini Arusha, wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia.

Akizungumza wakati akikagua eneo hilo jana, Dk. Kigwangala alisema wamiliki wa majengo ni wavamizi kama walivyo wavamizi wengine.

Wakati wa ziara hiyo, Dk. Kigwangala alikuwa ameongozana na Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk. Fredy Manongi na maofisa wengine wa mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa Dk. Kigwangala, eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 40 liliuzwa na Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) mwaka 2006 na NCAA kulinunua kwa gharama ya Sh bilioni 1.8.

“Nimepokea maelezo ya kina kutoka kwa wataalamu wa NCAA, hapa hakuna mgogoro kwa sababu eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 40 ni mali ya NCAA.

“Hao wenye nyumba 83 kwenye eneo la ekari 20 lililovamiwa, wajiandae kisaikolojia kwa sababu ni wavamizi kama wavamizi wengine.

“Tunajua hawana hati ya maeneo yao kwa sababu hati iliyopo ni moja tu na ndiyo iliyotolewa na Kamishna wa Ardhi na kama nao wana hati, basi ni batili.

“Tunawataka wajipange kwani Serikali ya Awamu ya Tano tunafanya kazi ya kuisafisha Serikali pamoja na nchi.

“Sasa basi, wanapaswa wajue tutasafisha na hapa, nawataka wajiandae kisaikolojia, nawaambia eneo hili halina mgogoro wa ardhi.

“Awali, eneo hili lilikuwa likimilikiwa na iliyokuwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTC), kisha likahamia kwa Bodi ya Utalii ya sasa (TTB) ambao ndio bado wana hatimiliki ya eneo hilo.

“Kwa hiyo, nawaagiza TTB waikabidhi hati hiyo kwa NCAA kwani kwa kuwa TTB walikuwa wameanzisha mgogoro na NCAA, nimewaambia waondoe kizuizi hicho ili wawapishe wenye eneo waendeleze eneo lao walilonunua kihalali.

“Mgogoro kati yao umekwisha na mimi ndiye mwenye mamlaka ya kusema hivyo. Huwezi kujenga eneo ambalo uhalali wake una maswali na ukawekeza nyumba ya Sh milioni 500 eneo ambalo huna uhakika nalo.

“Kesho (leo), nazindua rasmi bodi ya wakurungenzi wa NCAA na kazi ya kwanza nitakayowapatia ni kuhakikisha wanaanza na jukumu hili,” alisema Waziri Dk. Kigwangala.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu, Dk. Manongi alisema wanayo michoro waliyokuwa wamepanga kujenga katika eneo hilo jengo kubwa miaka 10 iliyopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles