29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU AONYA WATUMISHI WA MAHAKAMA

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


WANANCHI wametakiwa kuchukua hatua kwa kuwaripoti katika vyombo vya usalama, watumishi wa mahakama wasiokuwa waadilifu ikiwamo kuomba na kupokea rushwa ili wachukuliwe hatua badala ya kulalamika.

Hayo yalisemwa jana na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, alipokuwa akifungua wiki ya kutoa huduma za kisheria iliyoanza jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Nguvu na umuhimu wa mahakama ni imani kwa wananchi na imani kwa wananchi itaongezeka kama watapewa haki kwa kufuata maadili ya kazi.

“Mwananchi huna haja ya kulalamika, chukua hatua, nenda kwenye vyombo vya usalama, nenda kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili ukamtaje mtumishi asiye na maadili ili tuachane naye na ukiendelea kulalamika, unapoteza muda.

“Katika mahakama zote, kuna mabango yenye namba za simu zinazoweza kutumiwa na wananchi kutoa taarifa pale wanapokuwa na malalamiko badala ya kutumia njia ya kuandika barua,” alisema Jaji Profesa Juma.

Pamoja na hayo, Jaji Mkuu alisema kwamba, katika wiki ya sheria wananchi watajifunza na kuona nguvu ya sheria na inavyofanya kazi.

“Si lazima unapofikisha shauri lako mahakamani kutafuta haki, ushinde na wengi huwa wanadhani hivyo.

“Suala la kupata haki ni mtiririko mzima wa kulifikisha shauri lako mahakamani kwa maana ya kulisikiliza na kufikia uamuzi.

“Misingi ya haki ni wewe na jirani yako na vilevile kutafuta suluhu nje ya mahakama, kwani mahakama sasa imeanzisha utaratibu wa mahakama inayotembea ambayo itakuwa inawafuata wananchi walipo kwa gari na mashauri yatasikilizwa kwa mfumo wa Tehama,” alisema.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, aliwasisitizia wananchi kujenga utaratibu wa kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika ili hatua zichukuliwe kwa wanaokiuka maadili ya kazi zao badala ya kulalamika.

“Suluhisho la malalamiko ni kuyasema na hatua zichukuliwe. Tatizo kubwa la Watanzania ni kulalamika, toeni taarifa hatua zichukuliwe, acheni kulalamika,” alisema Profesa Kabudi.

Utoaji wa elimu ya sheria na msaada wa kisheria ulianza jana katika Viwanja vya Mnazimmoja na utafikia mwisho Februari mosi.

Maonyesho hayo ya wiki ya sheria, yalitanguliwa na matembezi maalumu ya kuadhimisha wiki hiyo yaliyofanyika kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kuongozwa na Jaji Profesa Juma ambaye alikuwa mgeni rasmi badala ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kama ilivyotangazwa awali.

Wakati wa maadhimisho ya wiki hiyo, majengo mbalimbali ya mahakama yakiwamo Mahakama ya Mwanzo Kawe, Kituo cha Kisasa cha Mafunzo Kisutu, Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mahakama ya Wilaya Mkuranga na Mahakama ya Wilaya Kigamboni yatazinduliwa.

Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Februari mosi mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Rais Dk. John Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles