23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RAFU ZA UCHAGUZI ZAANZA KINONDONI

Na ELIZEBETH HOMBO-DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya vyama viwili vyenye ushindani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuzindua kampeni za uchaguzi wa marudio ya Jimbo la Kinondoni, CCM imeituhumu Chadema kuanza mbinu chafu za kukihujumu.

Chama hicho tawala Wilaya ya Kinondoni, kimedai kukamata gari linalotumiwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (Chadema), likiwa na vijana wawili ambao walitaka kufanya fujo katika ofisi hizo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Kinondoni, Lilian Rwebangira, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba, Chadema imeshajiona itashindwa hivyo imeamua kutumia mbinu mbadala kuhujumu wananchi ili wasiende kupiga kura siku ya uchaguzi kwa kuhofia vurugu.

“Jana (juzi) saa 2:30 usiku, gari la Meya wa Jiji la Dar es Salaam likiwa na vijana wawili waliokuwa  wamevaa kofia za CCM, waliingia ndani ya ofisi zetu na tukawabaini kuwa wametokea Wilaya ya Kigamboni.

“Baada ya tukio lile, tulimbana dereva na tukalipeleka tukio lile polisi, mpaka sasa bado gari hilo liko Kituo cha Polisi Magomeni na dereva pia ameshikiliwa.

“Pia tulikamata simu ya dereva na tukaona alikuwa anachati na Meya Mwita, huku meya akimuuliza tukio linaendeleaje na dereva akamjibu kuwa bado kuna ‘movement’ hapa CCM.

“Awali dereva huyo alisema kuwa amekuja kupaki gari lakini tulipombana, alisema amekuja na meya lakini yeye ameshuka. Pia katika uchunguzi wetu tumewabaini wale vijana wawili waliokuwa kwenye gari, historia yao inaonyesha huwa wanafanya vurugu kwenye matukio mbalimbali,” alisema.

Kutokana na hilo, Rwebangira alivitaka vyombo vya dola kulipa suala hilo uzito unaostahili kwa sababu wameshapata taarifa nyingi za vijana wa Chadema kutaka kufanya fujo.

“Vyombo vya dola hili jambo wasilichukulie kimasihara ni nyeti na tumeshapata taarifa nyingi za Chadema kwamba, wanajipanga kufanya fujo na kutishia wananchi wasiende kupiga kura.

“Sisi vijana wa CCM Kinondoni, tunatoa angalizo kwa vijana wa Chadema wanaojipanga kufanya vurugu kuwa kamwe hatutavumilia vitendo hivi,” alisema mwenyekiti huyo.

Aidha, Rwebangira aliilaani Ofisi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kwa gari lake kutumika kwenye matukio mabaya wakati huu wa kampeni.

“Hii inaonyesha ni namna gani Chadema wanavyotumia mali za umma vibaya katika matukio haya kwa kutumia gari la meya wa jiji.

“Mbali na hilo, juzi tulimkamata mwanamke mmoja akijifanya ni mwendawazimu, aliingia katika ofisi zetu na baada ya kumbana sana akataja jina lake na kumtambua kuwa ni mwana Chadema,” alisema Rwebangira.

MTANZANIA lilipomtafuta Meya Mwita kupitia simu yake ya kiganjani, iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno haukujibiwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi, akizungumzia tukio hilo, alisema juzi usiku walikuwa na kikao cha tathmini na baada ya kikao hicho, Mwita alilalamika kwamba dereva wake haonekani.

Alisema dereva huyo wa meya alitekwa na watu wa CCM kuanzia saa tisa alasiri jana (juzi) na kuachiwa saa 11 alfajiri baada ya kumtesa.

Mwenyekiti huyo wa Bavicha aliliambia MTANZANIA kwamba, kilichofanyika si njama za Chadema bali ni za CCM kwa kutaka kutengeneza mazingira ya kuvuruga uchaguzi huo kwa kisingizio kuwa Chadema ndiyo wameanzisha.

“Hivi inawezekanaje dereva wa Chadema akaenda CCM akafanye nini? Wanachofanya wanatengeneza mazingira ili zikitokea vurugu waseme ni Chadema. Jambo hili halikubaliki, naomba polisi wachukue hatua juu ya hili,” alisema Ole Sosopi.

Alieleza kwamba, kwa sasa dereva huyo wa meya yuko nyumbani lakini hapatikani hewani kwa sababu simu yake ilichukuliwa na vijana wa CCM.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani ambaye ndiye anayeongoza kampeni za uchaguzi katika Jimbo hilo la Kinondoni, Frederick Sumaye, alisema tuhuma zilizotolewa na CCM ni jambo lisiloingia akilini.

Sumaye ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, alikiri kupata taarifa za kuteswa kwa dereva huyo wa meya, lakini bado hajapata taarifa za kina kuhusiana na tukio hilo.

“Haya mambo hayawezekani, hivi kweli gari la mtu yeyote ukilikuta kwenye eneo lako unalikamata? Lakini ni bora umtafute meya mwenyewe ili akupe taarifa kamili,” alisema Sumaye.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Mulilo, alikiri kulishikilia gari la meya huyo wa Jiji la Dar es Salaam kwa uchunguzi.

Uchaguzi wa Kinondoni unafanyika kutokana na aliyekuwa mbunge wake, Maulid Mtulia, kujivua uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na kujiunga na CCM.

Uchaguzi huo wa marudio unatarajiwa kufanyika Februari 17, mwaka huu sambamba na Jimbo la Siha ambako mbunge wake naye, Dk. Godwin Molel, kajivua uanachama wa Chadema na kujiunga na chama hicho tawala ambacho kimempa ridhaa ya kupeperusha bendera yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles