22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

POLEPOLE AAHIDI EKARI 4000 ZA MASHAMBA SIHA

Na SAFINA SARWATT-SIHA


KATIBU wa Itikadi na Uenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Humphrey Polepole, amesema chama chake kitaielekeza Serikali iwatafutie wananchi wa Kata ya Eldrument, ekari 4000 kwa ajili ya ujenzi wa makazi baada ya CCM kushinda ubunge wa Jimbo la Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.

Polepole aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Matandi, Kata ya Eldrument, alipokuwa akimnadi mgombea Ubunge wa CCM, Dk. Godwin Mollel.

“Kama CCM tutashinda ubunge wa jimbo hili, tutaielekeza Serikali itafute ekari 4000 kwa ajili ya  wananchi wa Kata hii ya Eldrument ili mkajenge makazi yenu ya kudumu.

“Pamoja na hayo, tukishinda mjue tutamalizia ujenzi wa Zahanati ya Sinai iliyoko Kata ya Ormelili kwa sababu CCM ndiyo chama kikubwa kinachoongozwa kwa ilani inayotekelezeka,” alisema Polepole.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge, Dk. Mollel, alisema vyama vya upinzani ni sawa na kikundi cha Saccos na havina uwezo wa kuongoza nchi.

“Namshangaa Mbowe kwa kauli zake, kwamba mimi ni sawa na gunia la misumari na sibebeki. Najua aliyasema hayo kwa sababu anajua mimi siwezi kuingia kwenye vita ya kitoto.

“Kwa hiyo, nawaombeni ndugu zangu, mchague gunia la misumari ili tukajenge nchi. Najua Chadema wamenitukana sana, lakini siogopi matusi kwani kiu yangu kubwa ni maendeleo ya wananchi na si kufungwa mdomo kwa namna yoyote.

“Mkinipa kura, nitashughulika na kero zenu bila kujali chama kwani nipo kwa ajili ya masilahi ya watu wa Siha,” alisema Dk. Mollel.

Wakati huo huo, mgombea ubunge kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Mdoe Azaria, alisema kama atafanikiwa kushinda ubunge wa jimbo hilo, atatoa nusu ya mshahara wake kwenda katika halmashauri ili fedha hizo zitumike kutatua kero za wananchi.

Katika hatua nyingine, Mgombea Ubunge Jimbo la Siha kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Tumsifuel Mwanri, alisema endapo wananchi wa Siha watamchagua, atahakikisha anatatua kero za elimu, maji, afya na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni jana, Masoud Omar ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF Taifa, aliwataka wananchi kuchagua watu wasiofunga plasta ili wakawaletee maendeleo.

Kwa upande wake, Mgombea wa Chadema, Elvis Mosi, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza na kumpigia kura siku ya uchaguzi Februari 17, mwaka huu  na kuachana na maneno yanatolewa na baadhi ya watu kuwa hali ya usalama si shwari jimboni humo.

“Ndugu zangu wana-Siha, suala na ulinzi na usalama naamini limeimarishwa na Jeshi  la Polisi, kila mmoja ahakikishe kuwa anatumia haki  yake  vizuri ya kupiga kura na kumpa kiongozi atakayeweza kuwaletea maendeleo,” alisema Mosi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles