24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

OLE SOSOPI: NINA NDOTO YA KUWA MWENYEKITI CHADEMA


Na EVANS MAGEGE

WIKI iliyopita gazeti hili lilichapa sehemu ya kwanza ya mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Patrick Ole Sosopi.

Endelea sehemu hii ya mwisho…

MTANZANIA Jumapili: Hivi karibuni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, alifanya mazungumzo na Rais John Magufuli, baada ya hapo aliibuka na kumpongeza Rais kwa utendaji kazi wake, kwa mtazamo huo, hudhani kuwa wanachama wenzenu wanaweza kutumia mwanya huo kuendelea kukihama chama?

Ole Sosopi: Watu walianza kuondoka kabla Lowassa hajakutana na Rais, sidhani kama yeye anaweza kuwa moja ya hamasa ya kuwafanya watu waendelee kuondoka kwa sababu ya kauli yake.

Siwezi kushawishika kuamini watu wengi zaidi watahama kwenda upande wa pili kwa sababu ya kauli hiyo ya Lowassa.

Kama kumbukumbu zangu ziko sawa, Rais Magufuli akiwa Singida alipata kueleza  kwamba, itakapofika 2020 vyama vya upinzani vitakuwa vimekufa, kwa maana vitakuwa vimekwisha vyote.

Sasa kama huo ndio mpango wake, binafsi naamini Chadema katika kipindi tunachopitia ni bora kuliko vipindi vyote, kwa sababu tunakwenda kupata wanachama wa kweli, wa uhakika na watu ambao watakuwa tayari kwa mapambano wakati wote, tofauti na hawa wanaorubuniwa  na kuondoka.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini Rais alimwita Lowassa na si Sumaye? Au ni kwasababu Lowassa ndiyo nguzo kuu ya Chadema?

Ole Sosopi: Chadema ni taasisi, hakuna mtu maarufu kuzidi Chadema, watu wote wanapata umaarufu kupitia Chadema.

Leo hii ukitaka kuwa maarufu jiunge na Chadema, ukitaka kuwa na uwezo mkubwa wa ushawishi katika jamii njoo Chadema.

Kwa hiyo, kitendo cha Rais kumwita Lowassa  na si Sumaye si kwamba hatamwita Sumaye, kuwa wa kwanza kuitwa na Rais haina maana kwamba wewe ni bora kuliko wa pili, ila ni maamuzi yake na utashi wake kama Rais ndio ulimtuma aanze na Lowassa.

Ndani ya Chadema kila mtu anaheshimika kwa mchango alionao, nafasi aliyonayo na uwezo wa kiutendaji alionao na si kwamba ni bora kuliko Chadema.

Leo chama hiki kilipofikia hata Mbowe akihama, Chadema hakiwezi kufa, hii ni taasisi.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini upinzani inawawia vigumu kupongeza utendaji kazi wa Rais Magufuli?

Ole Sosopi: Mbona tunapongeza, ingawa si kazi yetu kupongeza. Tukimpongeza Rais Polepole atafanya kazi gani? Sisi tuna jukumu la kukosoa pale tunapoona panafaa kukosolewa.

Mimi binafsi nampongeza Rais kwa kufikisha miaka miwili madarakani, maana kutawala nchi hii kwa miaka miwili si mchezo, sasa kama wewe utasema nimpongeze kwa unayoyataka wewe, yaseme wewe, lakini hayo yatakuwa hayanihusu.

Hata hivyo, CCM kama wanataka pongezi zetu kwa Rais tutawapa tu,  ila kwa sasa bado ni haraka sana, labda hajagusa pale tunapopataka, shughuli nyingine anazozifanya na kuridhisha moyo wake ni kutimiza hitaji la wale waliomfanya yeye kuwa Rais.

MTANZANIA Jumapili: Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James amepata kusema kuwa yuko tayari kushirikiana na mabaraza mengine ya vijana, ikiwamo Bavicha, je, uko tayari kushirikiana naye?

Ole Sosopi: Ninachoamini siku zote UVCCM wanachofanya ni maelekezo ya chama chao, hawana kazi kubwa wala uwezo wa kuikosoa au kuishauri serikali, wakati wote ndimi zao zimekuwa zikitamka kuwa wako tayari kushughulika na mtu atakayemsema Rais vibaya, kwamba wao watamtetea Rais wakati wote.

Suala la yeye kutaka tukutane mimi niko tayari kukutana na kiongozi wa chama chochote cha siasa, kama ni kwa masilahi ya nchi na si vinginevyo.

Lazima tujue dhamira yetu ni nini katika kipindi hiki ambacho sisi tumepata kuaminiwa na vijana wenzetu.

Kheri akipata hiyo fikra ya kukutana na mimi kama mwenyekiti wa Bavicha milango iko wazi.

Ifahamike kuwa, Bavicha tunasimama kama baraza mbadala, inamaanisha tunasimama kama baraza kivuli la vijana hapa Tanzania, kwa sababu nchi yetu haina baraza la vijana ambalo linawaunganisha vijana wote kutoka itikadi tofauti.

Binafsi namtakia kila lenye heri kiongozi mwenzangu kijana, pia namuasa ajue kuwa, hatakuwa mwenyekiti wa kudumu wa UVCCM, hivyo aongoze jumuia hiyo kwa masilahi ya Taifa ili siku nyingine aongoze pengine.

MTANZANIA Jumapili: Aina ya siasa zako za majukwaani zinatafsiriwa kuwa ni za mlengo mkali, unajitathimini vipi kwa aina hiyo ya siasa zako na uchochezi?

Ole Sosopi: Kwanza ufahamu kuwa, nina ndoto ya kuwa mtu fulani ndani ya taifa hili. Ni mapema kusema, lakini kwa bahati mbaya mataifa yetu mengi ya Afrika hayathamini ndoto za vijana.

Kuna sura inayotafsiriwa kwamba ninaposimama na kusema chochote ni uchochezi, pia ujue kuwa, kukamatwa na kutuhumiwa haina maana umekosea.

Nimewahi kukamatwa na nikatuhumiwa, lakini sina hatia, kwa hiyo sauti yangu inaweza kuonekana kwamba ina sura ya uchochezi, ndivyo Mungu alivyoniumba. Sifikiri kama nitabadilika kwa sababu sifikiri kama nina kosa na mara nyingi katika maisha usipende kuiga, ishi kwa asilia uliyonayo.

MTANZANIA Jumapili: Chadema mnaingia katika uchaguzi wa ndani mwaka huu, Mwenyekiti aliyepo madarakani kaongoza chama kwa muda mrefu, wakati huo huo hisia za wengi zinadai kwamba, ndani ya chama hakuna demokrasia, hili unalizungumziaje?

Ole Sosopi: Maandiko yanasema kabla hujaona kibanzi kwenye jicho la mwenzio toa boriti iliyo jichoni mwako.

Hii demokrasia wanayoihubiri wao kwamba Chadema hatuna, ngoja tuweke kumbukumbu sawa, Chadema ndiyo chama kinayaishi maneno yake kwa maana ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo. CCM hawajawahi kubadilisha mwenyekiti.

Chadema tuna historia ya kuwa na wenyeviti wengi. Ngoja nifafanue ni hivi; CCM wakati wote anayepaswa kuwa mwenyekiti ni mwanachama mwenye sifa ya urais tu, kwamba hakuna mwanachama mwingine yeyote mwenye haki ya kuwa mwenyekiti.

Huo muundo wa Katiba yao hauleti maana ya demokrasia na msingi wake ni kwamba kuna watu watakufa bila kuwa na ndoto ya kuwa mwenyekiti wa CCM. Mtu kuwa Rais si jambo dogo, ni mchakato mgumu, kwa hiyo ni watu wachache sana watapata nafasi hiyo ya uenyekiti.

Kwa hiyo CCM haina demokrasia katika nafasi ya kupata mwenyekiti na hawajawahi kuwa na demokrasia hata siku moja kwa nafasi hiyo.

Upande wa Chadema demokrasia ya kuwa mwenyekiti ipo kwa mtu yeyote, binafsi nina ndoto ya kuwa mwenyekiti wa Chadema. Si kwa sababu nitakuwa Rais au ni kwasababu nimekuwa mwenyekiti wa Bavicha.

Uchaguzi uliopita tuliofanya Mlimani City, Mwenyekiti Freeman Mbowe aligombea na mtu ambaye ni mwanachama wa kawaida kabisa na Mbowe alishinda kwa asilimia takribani 94, sasa jifikirie mwenyekiti wao CCM anashinda kwa asilimia 100, ni jambo la aibu.

Hawakuwashindanisha watu, walichokifanya ni kuweka NDIO au HAPANA, hii ina tofauti gani na kuweka picha na kivuli? Yaani upende usipende, binadamu ndiye mwenyekiti, kivuli hakiwezi kuongoza.

Kwa hiyo Chadema tuna demokrasia na kila mmoja ana haki ya kuwa mwenyekiti, demokrasia ndani ya chama chetu haijawahi kuwa dhoofu au kuwa katika mazingira hatarishi, bali imeimarishwa.

Kwa hiyo, Mbowe kuwa mwenyekiti kwa muda mrefu si ajenda inayowazuia CCM kufanya maendeleo ya nchi hii.

Kwanini wawe na hofu kuhusu Mbowe wakati sisi wanachama ndio tunaomkubali.

Mwenyekiti wa sasa ni Mbowe, uchaguzi ukifanyika na wanachama wakichagua awe Mbowe, tutamtetea yeye na Katiba ya Chadema mpaka hapo wakati utakapofika kwamba mwenyekiti mwingine anapaswa kuwapo kuendeleza mapambano.

Kwa hiyo sisi hatubadilishi kama fasheni, madamu ni jambo la kikatiba na hatukiuki sheria za vyama vya siasa nchini.

Sisi hatumchukulii mwenyekiti wetu kama kiongozi tu ndani ya chama, bali ni mtu anayeongoza mapambano ya kutafuta uhuru wa pili wa taifa letu kifikra, kimtazamo na kiuchumi.

Dhamira yetu ni kuwa na mtu anayeongoza mapambano ya kushinda dola, Mbowe anaongoza mapambano na tunahitaji mtu imara wa kufanya hivyo na kila mtu anaufahamu uimara wa Mbowe, ndiyo maana hawamtaki.

Kwa misukosuko anayokumbana nayo Mbowe, ingekuwa mtu mwingine wa kawaida angekuwa ameshakimbia nchi. Siasa ya nchi hii ni ngumu, kuna watu wanafikiri kiwepesi wepesi, lakini mambo magumu sana tunakumbana nayo, kwa hiyo hatuwezi kubadili mtu kirahisi rahisi kwenye mazingira kama haya ambayo demokrasia iko mahututi, imedhoofika na hatujui kama itatoka salama.

MTANZANIA Jumapili: Hudhani kuwa ipo haja sasa ya kuwa na ukomo wa madaraka kwa nafasi za viongozi, hususan ngazi ya mwenyekiti Taifa?

Ole Sosopi: Mbona ukomo upo, binafsi siwezi kuwa mwenyekiti wa Bavicha kama umri wangu ukiwa zaidi ya miaka 35. Kwani huo sio ukomo au mnataka ukomo wa Mbowe peke yake?

Sisi tupo kwenye mapambano, tunafanya siasa na kwa sababu hatufungwi na Katiba yetu au sheria za nchi, tunaendelea kumchagua mtu kwa sababu ya uwezo wake na lengo la kufikisha taasisi yetu pale tunapofikiri.

Ukomo ni jambo la muhimu, lakini si lazima, inatakiwa kuweka desturi katika kuwapata viongozi na kwa muda huu sisi hatuoni suala la ukomo kama ni ajenda kwetu. Ajenda ya muhimu kwa sasa ni sisi kuikomboa nchi hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles