24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

UTATA ‘FIRST LADY’ WA LIBERIA


Na MARKUS MPANGALA 

GEORGE Opong Weah ameandika ukurasa mpya katika historia yake kwa kuwa Rais wa Liberia kupitia Muungano wa upinzani wa CDC, baada ya kuapishwa Januari 22, mwaka huu na kuanza rasmi majukumu mapya ya kiutawala nchini humo. Weah amerithi madaraka hayo kutoka kwa Rais Ellen-Sirleaf Johnson, aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 12.

Liberia ilipata kutumbukia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha maelfu ya watu kukosa makazi na wengine 250,000 kufariki dunia. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa Jumuiya ya Kiuchumi na Maendeleo ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas).

Kihistoria, Weah alianza maisha yake kama mwanasoka, ambapo alizichezea klabu za Monaco, Paris Saint German, AC Milan, Chelsea na Manchester City. Baada ya kustaafu soka, mwaka 2003 aliingia moja kwa moja kwenye masuala ya siasa.

Licha ya kejeli kutoka kwa wanasiasa wenzake, lakini alianza kwa kushinda nafasi ya Bunge la Seneti, kisha akaanza harakati za kupata elimu. Ndani ya miaka 12, Weah alifanikiwa kupata elimu ya sekondari, shahada ya kwanza na uzamili, kisha akarejea kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Kabla na baada ya kuapishwa, gumzo kubwa lilikuwa juu ya ‘mke wa rais’ au maarufu kama ‘First Lady’. Licha ya majina kadhaa kutajwa, lakini jina la Clar Weah lilikuwa nambari moja. Clar amezaa watoto watatu na kiongozi huyo mpya wa Liberia.

Majina mengine yaliyokuwa yakitajwa iwe rasmi au minong’ono ni pamoja na Miapeh Gono, raia wa Liberia, ambaye anatajwa kuzaa mtoto mmoja na Rais Weah na wamewahi kuishi pamoja huko Florida, nchini Marekani, mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Inadaiwa kuwa, Miapeh Gono aliwahi kumfungulia mashtaka Weah, kutokana na kushindwa kutoa huduma za malezi kwa mtoto wao.

Weah alikanusha taarifa hizo za kuzaa na Miapeh Gono, hata hivyo, mahakama ilimuunga mkono mwanamke huyo na kutaka vipimo vya vinasaba vifanyike ambapo vilithibitisha kuwa ndiye baba halisi.

Mwanamke mwingine anayehusishwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Weah ni Macdella Cooper, raia wa Liberia. Macdella pia alikuwa miongoni mwa wagombea urais wa Liberia, alithibitisha kuwa na mahusiano na mwanasoka huyo wa zamani.

Hata hivyo, haikuwa rasmi au kutambulika kisheria kama wanawake wawili hawa, Macdella na Miapeh Gono, walifunga ndoa ya kiserikali, kidini au kimila. Hakuna rekodi hizo popote.

Taarifa za mtandao maarufu barani Afrika wa The Punch wa Nigeria zimebainisha kuwa, George Weah na Clar Duncan-Weah walifunga ndoa takribani miaka 20 iliyopita na kubarikiwa kupata watoto watatu; Timoth, George Weah Jr na Tita Weah.

Mjadala mkubwa kuhusu nani atakuwa ‘First Lady’ umezidi kupamba moto kila kona ya Liberia. Licha ya Clar kutambulika kuwa mke halali wa ndoa, hata hivyo, inaelezwa kuwa, si raia wa Liberia.

Clar ni mzaliwa wa Jamaica mwenye uraia wa Marekani. Inadaiwa kuwa, Clar bado ana uraia wa Jamaica. Mtandao wa gazeti la Jamaica Observer umeandika kuwa, Clar Duncan-Weah ni raia wa Jamaica ambaye atakuwa ‘First Lady’ katika nchi ya kigeni.

Pamoja na mjadala huo, inaelezwa kuwa, kama Clar Duncan-Weah atakuwa ‘First Lady’, inatafsiriwa kwamba kitendo hicho kitajenga uhusiano thabiti baina ya mataifa hayo mawili; Jamaica na Liberia.

Hata hivyo, katika mjadala huo kuna makundi kadhaa yamejigawa. Lipo kundi la wapenda utamaduni wanasema kuwa itakuwa mara ya kwanza kwa Taifa la Liberia kuwa na ‘First Lady’ ambaye hajui hata lugha moja ya asili ya nchi hiyo.

Kundi hili linaamini kuwa, ili mwanamke kuwa ‘Lirst Lady’, ni lazima awe na ujuzi wa kuzungumza lugha za nchi hiyo angalau moja tu. Hivyo basi, linaona kuwa kitendo cha mwanamke wa kigeni si halali, pia lawama zinaelekezwa kwa wanaume wote wa Liberia wanaooa wanawake kutoka nje ya Taifa hilo.

Uzalendo wa kundi hili umeegemea katika kuenzi utamaduni na kuwathamini wanawake wa Liberia. Wao wanambagua Clar kwasababu si mzungumzaji wa lugha za Liberia, na zaidi haujui utamaduni wa nchi hiyo.

Kundi la pili ni la wazalendo, ambalo linaona kitendo cha rais wao kuoa mwanamke wa Jamaica na ambaye hana uraia wa nchi yao si haki. Kundi hili linalalamika kuwa Clar hajawahi kuishi Liberia angalau miaka miwili au mmoja. Maisha yake yote yamekuwa nchini Marekani kama ilivyokuwa kwa Weah mwenyewe.

Kundi hilo linatoa hoja kwamba; Clar haipendi Liberia na anaiona ni nchi ambayo haikuweza kumtosheleza kwa lolote, hivyo si mzalendo wa kweli, licha ya Uafrika wake. Hata hivyo, kundi hilo linakosa sababu nyingi za msingi za kumbagua mwanamama huyo ambaye huko Fort Lauderdale, Jimbo la Florida nchini Marekani anafanya biashara zake za kuendesha mgahawa wa vyakula vyenye asili ya Caribbean.

Kundi la tatu linaegemea kwenye masilahi ya Taifa. Linasema kuwa, Serikali ya Liberia italazimika kutumia rasilimali zake kumhudumia ‘First Lady’ ambaye haonekani kuipenda nchi yenyewe.

Kwamba huduma hizo zilitakiwa kutolewa kwa mwanamke mwenye asili ya Liberia kuliko Clar. Wafuasi wa kundi hili wanaamini kuwa, mali za Liberia zitafujwa kwa kumhudumia ‘First Lady’ wao kwakuwa ni ‘mgeni’.

Kundi la tatu ni lile la wakosoaji, ambao walianza muda mrefu kumpinga Clar. Wao wanaegemea zaidi kwenye uzawa wa Liberia. Hawampendi moja kwa moja, si kwa ubinadamu wake wa kuwa Clar, bali si raia mwenzao.

Wao wanaamini Ikulu safari hii imeingiliwa na mtu wa kigeni kabisa ambaye hana uhusiano wowote na Liberia, nje ya mapenzi yake kwa mshindi wa kiti cha urais, Weah.

Hawa wanashambulia kweli kweli na wanatumia nguvu kubwa. Wanatoa mifano kuwa, kilichomnyima urais mgombea wa chama cha ANC, Alexander Cummings, ni hicho cha kuwa na mke asiye Mliberia.

Mke wa Cummings, Teresa Cummings, naye anaishi Florida, nchini Marekani, akiwa na watoto wao, huku mumewe anaishi Liberia. Hii nayo ni sababu iliyowaudhi baadhi ya wapigakura wanawake na hata wanaume, wakiwa na imani kuwa, huyo si mwenzao.

Katika kipindi cha ndoa yao iliyodumu miaka 20, Clar Duncan-Weah hajawahi kuishi wala kuchukua uraia wa Liberia. Katiba ya Liberia inasema kuwa, Mwafrika (mtu mweusi) yeyote anaweza kuwa raia wa nchi hiyo kwakuwa ni Mwafrika.

Clar anayo sifa ya Uafrika kutoka Jamaica, ambaye anaweza kuwa raia wa Liberia iwapo atapenda, lakini anatakiwa kuishi nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano. Clar hajaishi Liberia kwa kipindi hicho.

Kundi hili linatafsiri kuwa kitendo cha Clar kupuuza kuchukua uraia wa Liberia kinapaswa kuchukuliwa kama kigezo cha kumnyima iwapo ataomba sasa baada ya mumewe kushinda urais.

“Mwanamke ambaye hataki kuishi hapa, wanajihisi kwamba Liberia haiwezi kuwatosheleza. Wanakuja hapa kuwafuata waume zao pekee kuchukua fedha zetu na kupeleka kwao,” alikaririwa na The Punch, Angel Morlee, mwananchi wa Liberia.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kitendo cha Clar kukosa sifa ya kuishi nchini Liberia kwa miaka mitano ili aweze kuwa raia wa nchi hiyo kinaweza kuingiza dosari katika uhusiano wao, kwasababu Weah amekuwa akihusishwa na wanawake wengine ambao wanaweza kutumika kisiasa ili kulinda cheo chake.

Pamoja na mjadala wote uliokuwa ukifanyika na minong’ono ya kila namna, Rais George Weah alilazimika kuzungumzia suala hilo ili kuweka wazi msimamo wake mbele ya Waliberia wenzake katika programu ya kutoa shukrani ndani ya Ukumbi wa Jiji wa Monrovia, kabla ya kula kiapo katika Uwanja wa Antoinette Tubman, nchini humo.

Weah amewaomba wananchi waache kumbagua mkewe, Clar Duncan-Weah, ikiwa ni njia ya kuzima mjadala juu ya uraia wa mwanamke huyo, kwakuwa ni Mwafrika mzaliwa wa Jamaica.

“Niliona maneno mengi kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi yenu mnasema kwanini ‘First Lady’ wetu awe raia wa Jamaica? Kama hiyo ndiyo sababu ya kutotaka George Weah awe rais, basi mnakosea sana. Katika kipindi cha shida alichokuwapo George Weah, naye Clar Weah alikuwapo.

“Ibara ya 27(B) ya Katiba ya Liberia inaeleza kuwa mtu ambaye ni Mwafrika au mwenye familia yenye asili ya mtu mweusi anakuwa na vigezo vya kuwa Mliberia kwa kuzaliwa au kuomba kuwa raia wa Liberia.

“Ni namna gani mtu anaweza kuwa raia wa Jamaica halafu asiwe Mwafrika? Waliberia, huu ni wakati wa Liberia mpya ambayo haitambagua mtu yeyote,” anasema Rais Weah.

Kwa upande wake mke wa Rais  Weah, Clar, amewashukuru wale wote waliomuunga mkono mume wake tangu mwanzo hadi kushinda nafasi hiyo.

“Napenda kuwahakikishia kuwa George atafanya kila analoweza kuitumikia Liberia, atatanguliza mbele masilahi ya Liberia. Na akiwa na mimi kwa upande wangu, ninathibitisha kuwa atafanikiwa yote,” amesema Clar.

George Weah na Clar Duncan-Weah walikutana kwa mara ya kwanza katika tawi la benki ya Chase.

George Rawlon Manneh Oppong Ousman Weah alizaliwa Oktoba 1,1966 jijini Monrovia nchini Liberia. Alilelewa na bibi yake katika kitongoji cha Wet Point jijini humo. Alisoma Shule ya Msingi Muslim Congress, baadaye alisoma Wells Hairston High School, hakumaliza elimu yake baada ya kuacha shule mwaka wa mwisho na kujikita kwenye soka akiwa na miaka umri wa miaka 15.

Aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Mawasiliano la Liberia. Baba yake ni William T. Weah Sr alikuwa makenika, mama yake Anna Quayeweah alikuwa mchuuzi. Kaka zake ni William, Moses na Wolo. George ni miongoni mwa watoto 13 waliolelewa na bibi yao Emma Khonjlaleh Brown baada ya wazazi wake kutengana.

Mwaka 2006 alianza harakati za kusaka urais, hata hivyo alibwagwa kwa kishindo na Rais aliyemaliza muda wake, Ellen Sirleaf Johnson. Mwaka 2011 alirudi kwenye kinyang’anyiro akiwa mgombea mwenza wa chama chake cha CDC, lakini hakufanikiwa.

Hata hivyo alikumbana na kadhia ya kuhojiwa uwezo wake kielimu hali ambayo ilimlazimu kuanza safari ya masomo. Taarifa zinasema George Weah ametumia miaka 12 kusaka elimu ya sekondari na chuo kikuu.

Kampeni za elimu ndogo dhidi yake zilimfanya aseme kuwa yeye alisoma katika Chuo Kikuu cha Parkwood cha London katika shahada ya Sanaa katika uongozi wa michezo. Hata hivyo chuo hicho hakikutambulika, elimu hiyo ilitajwa kuwa sawa na diploma. Baadaye Weah alisoma katika Chuo Kikuu cha Devry mjini Miami nchini Marekani katika shahada ya  usimamizi wa biashara.

Oktoba mwaka 2017 alikwenda kufanyiwa maombi kwa mchungaji wa Nigeria, T.B Joshua akiwa na seneta mwenzake Prince Tormie Johnson.

Aidha, inaelezwa ni T.B Joshua ndiye kiini cha Rais mstaafu Ellen Sirleaf Johnson kuamua kumuunga mkono Weah kwenye kinyang’anyiro cha urais cha mwaka 2017.

Hata hivyo chama tawala cha nchi hiyo Unity Party kimeshamfukuza uanachama Rais Ellen Sirleaf Johnson kwa makosa  hayo ya kumuunga mkono Weah badala ya Joseph Bokai wa chama chake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles