29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KISHINDO KINONDONI


AGATHA CHARLES Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

VYAMA viwili vyenye ushindani wa karibu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana vilizindua kampeni za uchaguzi wa marudio kwa vijembe katika Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam.

CCM ambayo ilizindua kampeni zake katika viwanja vya Biafra Kinondoni na Chadema viwanja vya Ali Mapilau, karibu na Hospitali ya Mwananyamala, vimenyoosheana vidole, kila kimoja kikimwambia mwenzake hafai kuongoza jimbo hilo.

Wakati CCM ikidai Chadema imekosa sera kwa sababu imekwishatekeleza karibu kila jambo, chama hicho cha upinzani nacho kimemshutumu mshindani wake huyo kuwa hakijaweza kushughulikia matatizo ya wananchi na badala yake kimesababisha hasara ya kurudia uchaguzi unaotumia fedha ambazo zingetumika kutatua kero nyingi zilizopo kama ajira, huduma za afya nk.

HOJA ZA CCM

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ambaye aliongoza mamia ya wafuasi wa CCM katika uzinduzi wa kampeni hizo, akiwa ameambatana na kada mkongwe, Stephen Wassira na viongozi wengine wa chama hicho, alisema uchaguzi huo umebeba uzito sawa na uchaguzi mkubwa.

Mwigulu ambaye alikuwa akimnadi mgombea ubunge wa chama chake, Maulid Mtulia, alisema akiangalia tathimini ya hali ya kisiasa, sera na ajenda za kitaifa zote zinatekelezwa na Ilani ya CCM.

Kwa muktadha huo, alisema haina haja ya kumpa kura mpinzani kwa sababu wananchi wana mkataba na CCM hadi mwaka 2020.

Alisema kumpa kura mpinzani katika uchaguzi huo mdogo ni sawa na kujicheleweshea maendeleo na kumtaka kila mmoja kuwa meneja wa kampeni ili kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.

“Kama una safari na ukagundua gari ulilopanda ni bovu unashuka na kuhamia gari ambalo ni zima, sasa kule gari lenyewe hata dereva hajulikani, sasa unakaa unasubiri nini, yani hata kupe akushinde akili?

“Sisi wafugaji tunajua ukiwa na ng’ombe ukamchinja, kupe wote wanaondoka haraka katika ile ngozi na kwenda kwenye ng’ombe mzima, wale watakaobaki ndio watakaukia kwenye ngozi hiyo,” alisema Mwigulu.

Aliongeza kwamba anaamini kuwa kama vyama vya upinzani vingekuwa vinatekeleza wajibu wake ipasavyo, watu wasingekuwa wanavihama.

Mwigulu pia alitumia fursa hiyo kutetea kile kinachotajwa kuwa hali ngumu ya kimaisha, akisema kuwa hatua zinazochukuliwa na Rais Dk. John Magufuli ni sahihi kwa sababu msingi wa uchumi siku zote ni kuwekeza fedha ili kupata fedha.

“Hizi lawama za kusema eti kuna mzunguko mdogo wa fedha nchini hazina mashiko kwa sababu huwezi ukajenga reli, ukanunua ndege, kujenga mitambo ya kufua umeme, ukapanua bandari, ukatoa elimu bure halafu fedha ikawa vilevile.

“Ukiishajenga reli, ukapanua bandari na ukanunua ndege sio kwamba kila mwaka utakuwa unafanya hivyo, kwa sababu kama ujenzi ukikamilika na ukianza kuzalisha fedha, unakuwa na wigo mpana wa kupandisha mishahara, unatoa ruzuku kwa wakulima, kwahiyo fedha uliyoiwekeza ukianza kuivuna ndiyo utakuwa unaitumia kwa kujidai,” alisema.

Alisifia miradi inayofanywa na Rais Magufuli akisema itaishi hadi kizazi cha wajukuu zetu na hivyo kushangaa wapinzani wanapowazuia wanachama wao kuipongeza.

Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Wassira, alisema wapinzani wamekuwa hawana sera madhubuti na badala yake wamekuwa wakitumia uongo kujiaminisha kwa wananchi.

“Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 walijitangaza sana mabadiliko, watu walikwenda pale Jangwani kwenye kampeni zao kwa hamasa ya hali ya juu wakisubiri mgombea wao anasema nini, cha ajabu aliposimama aliongea kwa dakika tatu tu na hotuba yake fupi kuliko sala ya ‘Baba yetu uliye mbinguni’.

“Yaani alisimama na kusema elimu, elimu, elimu halafu mengine mkasome kwenye Website, sasa hawa machinga wa Kinondoni ndio wana Website? Huyo ndio alikuwa mgombea wa Chadema, alikuwa hajui ilani yao na hakuwa na cha kusema chochote,” alisema.

Alisema uongo wa mabadiliko uliathiri sana Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe na Mara kwa sababu wananchi walichagua mabadiliko bila kufafanuliwa ni mabadiliko ya aina ipi.

“Tulifanya makosa, katika Mkoa wa Dar es Salaam mkachagua wabunge sita kati ya 10, yaani CCM ikapata wabunge wanne na wao wakapata wabunge sita,” alisema Wassira.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mtulia, kwa mara nyingine tena alisema mgogoro ndani ya CUF ndio uliochangia kuhama.

Alisema kwamba ilimuwia vigumu kuishi ndani ya chama hicho kwa sababu akimsikiliza katibu, mwenyekiti ananuna vivyo hivyo kwa mwenyekiti.

“Nimeona jahazi linaelekea kuzama, mbele nikaona chombo cha CCM nami nimechupa nijiokoe. Jamani si mnakumbuka wenzangu wabunge 10 wa viti maalumu walichofanyiwa, sasa mlisubiri na mimi nifukuzwe?

“Nilichupa kwa kujinusuru, leo nipo salama  nasimama kwenu Kinondoni, naomba tena kugombea ubunge sasa wao wananongwa ya nini, kwani huu ndio usaliti?” alisema.

Aliongeza kwamba amejiunga CCM kwa sababu anampenda sana Rais Dk. John Magufuli na sifa zake zinapendwa na kila Mtanzania.

Alisema amejiunga na CCM ili kuwatumikia vyema wananchi kwa sababu kuwa ndani ya chama hicho ni kujenga daraja la kuwaletea maendeleo wananchi.

“Ndani ya ubunge wangu kwa miaka miwili namba ya rais sikuwanayo, lakini kwa sasa kama mgombea namba ninayo hapa, sasa wana-Kinondoni mnataka nini? Kama mnataka maendeleo sasa nakuja nayo,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudencia Kabaka, alisema anampenda Mtulia kwa kuwa kaonyesha ushupavu kwa dhamira ya kuwatumikia wananchi wa Kinondoni kwa uhakika.

Alisema Mtulia kwa sasa yupo kwenye chombo salama cha kuwaongoza wana-Kinondoni, hivyo ni wajibu wa wananchi kuhakikisha wanampigia kura za kutosha ili aibuke mshindi kwenye uchaguzi huo mdogo.

“Nakumbuka pale Chang’ombe kwenye sherehe ya kupongezwa baada ya kushinda uwenyekiti wa UWT, kijana huyu Mtulia nilitambulishwa kwa mara ya kwanza, nami nilimpenda kwa uthubutu wake, kwa msingi huo sote tuhamasishane kuhakikisha tunampigia kura nyingi ili awe mbunge wetu,” alisema Kabaka.

Naye aliyekuwa mgombea ubunge wa Ilala kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Muslim Hassanali, ambaye kwa sasa amejiunga CCM, alisema chama chake hicho cha zamani hakina sera ya kuwasaidia Watanzania.

Alisema kwa kutambua hilo, aliona umuhimu wa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa sababu anayoyatekeleza ndiyo matakwa yaliyokuwa yanahitajiwa na wananchi kwa muda mrefu.

“Nimekuwa Chadema kwa miaka 15, nakifahamu chama hicho ndani na nje, bila saini ya Katibu Mkuu hupati posho na nimeona mengi mle, kusema ukweli hawana sera yoyote ya kuja kuwasaidia wananchi.” alisema.

Alielezwa kusikitishwa na watu wanaobeza na kuwatukana viongozi, hasa kupitia kwenye mitandao ya kijamii.

Katika hilo, Hassanali alimwomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu, kutumia kikosi cha askari wasio na mipaka (Interpol) kumkamata Mange Kimambi ambaye alidai amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kukashifu viongozi wa nchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema anashukuru Mungu kutokea uchaguzi huo wa marudio ndani ya jimbo hilo, kwa sababu utawasaidia wakazi wa Kinondoni kusahihisha makosa waliyoyafanya katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Awali Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba, alisema chama hicho kitashinda kwa goli la tikitaka huku wakiwa wamevaa msuli.

HOJA ZA CHADEMA

Kwa upande wake, Chadema licha ya uzinduzi wake kupambwa na msafara na umati wa wafuasi wake, pia ulikuwa na viongozi wengi wa kitaifa, wakiwamo wabunge.

Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa, aliyeongoza uzinduzi wa kampeni hizo, aliwaasa wananchi kuhifadhi demokrasia.

Akimnadi mgombea wa Chadema, Salum Mwalimu, aliwataka wananchi wa Kinondoni kushughulika kutafuta kura kwani CCM haitabiriki.

“Msipohifadhi demokrasia mwafa, huyu Mtulia msimsemeseme, wa nini? Shughulikieni kutafuta kura, CCM hawatabiriki,” alisema Lowassa.

Lowassa ambaye aliongoza kwa kushangiliwa katika kampeni hizo, alisema alishiriki katika uchaguzi mdogo wa kata 43 na kushuhudia umati mkubwa uliojitokeza katika kampeni hizo, lakini alishangaa kuambiwa kuwa kura hazikutosha.

“Salum ni kijana safi, ana uwezo wa kufanya kazi. Naomba mlinde kura, wenzetu wanatupatia kwenye kulinda. Heshima ya Chadema ni kubwa, wenzetu iko chini,” alisema Lowassa.

Pamoja na hilo, Lowassa ambaye alianza kwa kuwaongoza vijana kuimba wimbo wa ‘Vijana msilale bado mapambano’, alisema alifurahi kuwaona na kwamba anawakumbuka, hivyo mbali na kura za urais mwaka 2015 kutotosha, bado ana imani iko siku zitapatikana.

Mbali na Lowassa, mwingine aliyepanda jukwaani kumwombea kura Mwalimu, ni Waziri Mkuu mstaafu na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye.

Sumaye ambaye kama ilivyo kwa Lowassa, wote walihama CCM, alisema kazi ya mbunge ni kutetea wananchi na si kumtetea rais.

“Mtulia anasema amependezwa na rais kwa kazi anazozifanya, basi akateuliwe na rais. Wewe kama umehama basi ulikuwa huelewi kazi ya mbunge, diwani, hivyo Mtulia na genge lake waache kutukana Watanzania na kudharau fedha zetu,” alisema Sumaye.

Alisema fedha za kurudia uchaguzi huo zingeweza kwenda kuleta maendeleo katika sekta ya afya na elimu.

Sumaye alisema CCM imewadharau wananchi kwa kumrudisha Mtulia kugombea katika jimbo lile lile alilojiuzulu.

“Demokrasia ya vyama vingi ni wananchi wanapewa dhamana kuchagua na tunapokosa, tunakuwa na mvutano unaoelekeza utawala wa imla. Katiba inaruhusu maoni, lakini leo ukitoa maoni unaambiwa mchochezi,” alisema Sumaye.

Alisema vikao vya Bunge wakati wa utawala wa awamu ya tatu iliyoongozwa na Rais mstaafu  Benjamin Mkapa na ile ya awamu ya nne iliyoongozwa na Jakaya Kikwete vilionekana tofauti na wakati huu.

Sumaye alisema mfumo wa vyama vingi hivi sasa uko zaidi katika maneno kuliko vitendo.

“Tunakuwa na mfumo wa vyama vingi kwa maneno, lakini kwa vitendo hakuna, nchi itazama. Vyama vya upinzani vikifa tutazamisha nchi,” alisema Sumaye.

Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mwalimu, aliposimama kwa takribani dakika tisa, alisema anatafuta kura za utumishi wa Kinondoni kwa miaka mitatu.

Aliwaomba wana CCM na wale wa Chadema kumpigia kura ili akawawakilishe bungeni na kwenda kudai demokrasia, kusimamia haki masilahi na vilio vya wananchi.

Alisema anafahamu changamoto zinazowakabili watu wa Kinondoni ikiwamo ajira, huduma za afya nk.

Mwalimu alitumia nafasi hiyo kulikumbusha Jeshi la Polisi jinsi alivyotumia kalamu yake kama mwanahabari kulitetea na hivyo kuliomba lisimwangushe.

“Nilitumia kalamu yangu kutetea Jeshi la Polisi kwa miaka tisa kupitia kituo cha Televisheni cha Chanel ten, hivyo polisi wa Kinondoni hawatapata shida,” alisema Mwalimu.

Akizungumzia kuhusu soko la Tandale, Mwalimu alisema zilitengwa shilingi milioni 100, lakini mradi huo ulishindwa kukamilika kwani zinatakiwa milioni 54 nyingine hivyo aliomba kura ili akazitafute.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye pia alishangiliwa sana na wananchi wakati akipanda jukwaani, alisema watu wa Dar es Salaam wanaongea zaidi kuliko vitendo.

“Ninaongea haya wakati Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu) akiwa nchini Ubelgiji akiuguza majeraha yake, ninaongea haya wakati Sugu (Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi) akiwa mahabusu, ninaongea wakati robo ya wabunge wetu tuna kesi. Watu wa Dar mnaongea sana kuliko vitendo,” alisema Lema.

Lema alisema moja ya sababu za kutoipigia kura CCM ni wabunge kushindwa kuzungumza pamoja na hali ya maisha.

Alimshangaa Mtulia ambaye alikuwa mbunge na baadaye kujiuzulu kurudi tena kuomba ridhaa ya wananchi kumchagua kwenda kuwa mwakilishi wao katika Bunge lile lile.

“Wanasema ‘tutaiba kura tuna dola’, wala msiogope, tunakokwenda watakuwa walinzi wazuri. Kata 43 waliiba na kupiga watu, safari hii hatukubali kwani kinga ya taifa hili ni upinzani imara,” alisema Lema.

Alisema hadi wamekubali kurejea kwenye uchaguzi huu baada ya kususia uchaguzi mdogo uliopita, ni kwamba wamejipanga na hawakubali kuibiwa majimbo ya Kinondoni na Siha.

Alisema vijana wasiwe waoga kwani ni dhambi kubwa, lakini pia wasifanye fujo bali waweke heshima (ushindi) siku ya uchaguzi.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ambaye pia ni Meneja wa Kampeni wa Mwalimu, alisema ana rekodi ya kumwangusha aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, marehemu Didas Masaburi kwa kura 27,000.

Alisema wakati Mtulia alipochaguliwa jimboni hapo, alikodi pikipiki 300 za makamanda kwa fedha zake ili kukamilisha shughuli yake ya kuelekea kuapishwa.

Kubenea alitumia fursa hiyo kueleza harufu ya ufisadi akisema wakiwa katika majukumu yao katika Halmashauri ya Jiji, walikuta majoho yakifuliwa kwa Sh bilioni 4 na laki nane, hivyo waligoma kuyafua na kuyavaa mwaka mzima.

Alisema pamoja na wote kupatiwa ofisi, lakini Mtulia alipanga katika hoteli moja hapa jijini huku pia akichukua mkopo wa Sh milioni 500 benki, mkopo wa gari na fedha zake bungeni, hivyo wasimchague kumwezesha kupata tena fursa ya kukopa.

Tambwe Hiza, yeye alisema aliwahi kutoroka kwenye kampeni za urais za mwaka 2015 akiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Mbonde ambaye kwa sasa ni marehemu ili kwenda kumnadi Mtulia.

Alisema kutokana na usaliti alioufanya Mtulia, juzi alimshtaki kwa Mbonde.

Tambwe ambaye alipata kuwa mfuasi wa CUF baadae CCM kabla ya kuhamia Chadema mwaka 2015, aliitaja CUF inayoongozwa Profesa Ibrahim Lipumba kama ‘Mungiki’ na kusema hawahangaiki nayo na kwamba ile ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad haijasimamisha mgombea.

“Niliondoka CCM ili nisifie huko maana umri unaenda na dhambi ndio zinazidi. Cuf Mungiki wanatukana mitandaoni, Salum kasoma hapa tangu darasa la kwanza na anaishi hapa. Ni wa hapa, Dk. Mwinyi aliwahi kugombea bara na kisha Zanzibar,” alisema Tambwe.

Akizungumza katika kampeni hizo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, alisema usaliti alioufanya Mtulia utakitafuna kizazi chake chote.

Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje, alihoji mwanamume anahongwaje?

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, ambaye naye anaongoza timu ya kampeni, alisema vijana wamejiandaa kwa gharama yoyote kuwa jimbo hilo halitapotea huku akilinyooshea kidole Jeshi la Polisi.

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, alisema Februari 17 iwe mwanzo na mwisho wa biashara ya kuuza watu na wananchi kuuza utu wao.

Huku akilinyooshea kidole Jeshi la Polisi, alisema Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, akiwa Mkuu wa Polisi Tarime, alishuhudia kuapishwa kwa Matiko, hivyo alisema anatarajia kuona haki pia ikitendeka Kinondoni.

“Polisi waache huu mchezo uwe kati ya CCM na Chadema,” alisema Matiko.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo, alimfananisha Mtulia na bagia kuwa ilikuwa ni bidhaa iliyokuwa sokoni.

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, alisema Kinondoni anayoijua haiwezi kuacha kufanya mabadiliko na kwamba hawawezi kuruhusu kupigwa bao.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Dk. Milton Mahanga, alisema CCM wanamtambua kama jasusi, hivyo wamchague Mwalimu ili kukata hila.

Mbunge wa Mikumi ambaye pia ni mwanamuziki wa Hip Hop Tanzania, Joseph Haule, maarufu Prof Jay, akishangliwa mara kwa mara kutokana na kusherehesha kwa kuimba baadhi ya nyimbo zake, alisema Mtulia akipita Kinondoni demokrasia itakuwa imedhalilishwa.

MAANDAMANO

Ufunguzi wa kampeni hizo ulipambwa na maandamano makubwa yaliyojumuisha pikipiki na magari kutoka Ofisi za Chadema Kanda ya Pwani zilizopo Magomeni hadi uwanjani hapo.

Msafara wa magari hayo ulijumuisha yale ya waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Lowassa na Sumaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles