MWANDISHI WETU-DODOMA
KATIBU Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally, ameziagiza kamati za siasa za wilaya, kata na matawi kutowateua wagombea wenye sifa za ovyo ikiwemo kashfa za kuhujumu ushirika, kuuza ardhi za wananchi na wenye mwenendo usioaminika kwenye jamii.
Kauli hiyo imekuja wakati CCM, kikiendelea na michakato ya uchaguzi ndani ya chama kwa ajili ya kupata wagombea wa nafasi za uenyekiti wa Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji kwa ajili ya kupigiwa kura Novemba 24, mwaka huu.
Dk. Bashiru ametoa maelekezo hayo wakati kamati za siasa zikiendelea na vikao katika maeneo yote nchini, kwa ajili ya kuwafanyia tathmini wagombea wote waliojitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho, kuwania nafasi katika Serikali za mitaa, vitongoni na vijiji unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Makao Mkauu wa CCM mjini Dodoma iliyotolewa jana, ilisema Dk. Bashiru alitoa agizo hilo juzi, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa wenyeviti wa mashina, viongozi wa CCM na Serikali ngazi zote za mikoa, wilaya, kata na matawi, akiwa wilayani Liwale mkoani Lindi.
“Tukitaka kuzuia viongozi wababaishaji, Kangomba, Obutura, wadhulumaji wa ardhi, tuwe makini kwenye uchaguzi huu. Kama kuna kiongozi aliwahi kuuza ardhi kwa kuwaibia wananchi, asiteuliwe na vikao vya CCM na kama akihonga akapitishwa, wananchi msimchague mtu huyo na sisi tutashughulika na waliomteua.
“CCM haiingii kwenye uchaguzi ili tu kushinda na kupata viongozi, ila inaingia ili ishinde na ipate viongozi bora watakao wahudumia wananchi, kwa kuwa imeahidi kuwatumikia wananchi kwa haki,” alisema Dk. Bashiru.
Aliwataka wana CCM watakaoshindwa kwa namana yoyote kwenye kura za maoni kutosusa kwa hasira na kwenda vyama vingine kwa kwa sababu awamu hii chama kitaweka nguvu zaidi eneo ambalo mwana CCM amehama na kwenda kugombea upinzani, hivyo CCM itamshinda naye atakufa kisiasa.
Dk. Bashiru pia alielekeza kuwa mwana CCM yeyote atakayeshindwa kwenye kura za maoni kwa hujuma, atulie na kushirikiana na aliyeshinda, baada ya uchaguzi atasikilizwa na waliohusika na hujuma watawajibishwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama.
Alisisitiza na kutolea maelekezo kero mbalimbali za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa, huduma za kijamii na kuagiza viongozi wa Serikali ngazi za wilaya kuzishughulikia kwa kuwa nyingi zilitakiwa kuishia huko.
Alitumia fursa hiyo, kusisitiza viongozi kusikiliza changamoto za watu na kuzitafutia majibu.
Ziara hiyo ya Dk. Bashiru ni sehemu ya muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya kwa viongozi kuendelea kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza na kushughulikia changamoto zao.
Kwa mujibu wa ratiba ya CCM iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, ilieleza kuwa mchakato mzima ndani ya chama hicho ambapo Oktoba 7 – 12 Oktoba, 2019: ilikuwa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kugombea Uenyekiti wa Mitaa, Vijiji na Ujumbe wa Serikali za Vijiji na Mitaa kwa Makatibu wa Matawi ya CCM kote nchini.
Oktiba 13 Oktoba, 2019: Kamati za Siasa za matawi kujadili wagombea na kutoa Mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Kata
Oktoba 14 15 O, 2019: Kamati za Siasa za Kata kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Wilaya
Oktoba 16 – 18, 2019: Kamati za Siasa za wilaya kujadili wagombea na kufanya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni na mkutano wa wanachama wote wa tawi.
Oktoba 19 – 20, 2019: Mikutano ya kura za Maoni ya nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji – Mkutano wa Wanachama wote wa Tawi
BAADA YA KURA ZA MAONI
Oktoba 21, 2019: Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu za Matawi kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu ya Kata
Oktoba 22 – 23, 2019: Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu za Kata kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Wilaya
Oktoba 24 – 26, 2019: Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu za Wilaya kujadili wagombea na kutuma mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya.
Oktoba 27 – 28, 2019: Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya Kufanya Uteuzi wa Mwisho wa Wanachama watakaogombea Uenyekiti wa Mtaa, Ujumbe wa Kamati ya Mtaa, Uenyekiti wa Kijiji na Ujumbe wa Halmashauri ya Kijiji.
RATIBA YA SERIKALI
Oktoba 8 – 14, 2019: Zoezi la uandikishaji wapiga kura siku saba tu kwa Mwananchi mkaazi wa Mtaa/ Kijiji na Kitongoji
Oktoba 29, 2019: Kuanza kuchukua fomu za kugombea
Novemba 4, 2019: Tarehe ya Mwisho ya kurejesha fomu kwa Msimamizi
Novemba 10, 2019: Uwasilishaji wa ratiba za kampeni kwa Msimamizi
Novemba 17 – 23, 2019: Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji
Novemba 24, 2019: Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.