25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dereva teksi kortini akidaiwa kumteka Mo

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

SERIKALI imemfikisha mahakamani dereva teksi Mousa Twaleb (46) kwa mashtaka matatu ya kujihusisha na genge la uhalifu, kumteka mfanyabiashara Mohammed Dewji – maarufu Mo na kutakatisha fedha, Sh milioni nane.

Twaleb alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, akisaidia na Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, walimsomea mshtakiwa mashtaka matatu yanayomkabili.

Kadushi alisema shtaka la kwanza, mshtakiwa anatuhumiwa kujihusisha na genge la uhalifu, akidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei Mosi mwaka 2018 na Oktoba mwaka huo maeneo mbalimbali ya Tanzania na Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa kuteka nyara, kwamba Oktoba 11 mwaka 2018 katika Hoteli ya Colosseum wilayani Kinondoni, akiwa na wenzake ambao hawapo mahakamani, walimteka mfanyabiashara Mohammed Dewji kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri kinyume cha sheria.

Wakili Wankyo alidai shtaka la tatu, mshtakiwa anadaiwa kutakatisha fedha Sh milioni nane. Anadaiwa kuwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, alijipatia kiasi hicho cha fedha huku akijua fedha hizo ni mazalia ya genge la uhalifu.

Hakimu Shaidi alisema hawezi kumruhusu mshtakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Akielezea hatua ya kesi hiyo ilipofikia, Wakili Kadushi alidai sehemu kubwa ya upelelezi imekamilika, wanakamilisha taratibu za kisheria ili shauri lianze kusikilizwa.

Hakimu Shaidi alimuuliza mshtakiwa kama ana kitu cha kusema, naye alijibu kama ifuatavyo:
Mshtakiwa: Naweza kusema sio kweli.
Hakimu: Huruhusiwi kujibu lolote.
Mshtakiwa: Naweza kuomba dhamana maana nilikuwa nje kwa dhamana.
Hakimu: Mashtaka yanayokukabili hayana dhamana.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11 kwa ajili ya kutajwa.

JPM ASHANGAA POLISI

Machi 4, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli aliibua maswali matano kutokana na tukio la kutekwa kwa Mo, huku akionesha kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na polisi

Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na Mo alivyofika Gymkhana na watekaji kuacha silaha zao, muda mfupi baadaye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuonekana akinywa chai na mtekwaji, huku aliyedaiwa kuhifadhi wahalifu hao akiwa hajafikishwa mahakamani.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri na makamishna wapya wa Polisi, Rais Magufuli alisema anashangazwa kuona hadi wakati huo ambao ilikuwa imepita takribani miezi minne hakukuwa na hatua zozote zilizochukuliwa.

 “Watanzania si wajinga, wanafahamu na wanajua ‘ku-analyze’ mambo, alipotekwa Mohammed tulipata ‘story’ nyingi, lakini lilipokuja kumalizika lile suala limeacha maswali mengi zaidi.

“Aliyetekwa alikutwa Gymkhana, alikwendaje pale, lakini bunduki ziliachwa pale, wakajaribu kuchoma gari, lakini baadaye tunamuona aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa, maelezo hayapo.

“Lakini baada ya siku chache tunaelezwa nyumba alikokuwa ametekwa na aliyebeba watekaji huyu hapa, lakini baadaye kimya mpaka leo na miezi imepita.

“Tukio hili limeacha maswali mengi bila majibu, nikajiuliza labda ndiyo mambo ya kisasa kama lilivyo jina la Kamanda Mambosasa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Watanzania wanataka kuona hatua zinachukuliwa, lakini dosari ndogondogo zinalichafua Jeshi la Polisi.

“Watanzania wanataka kuona angalau huyo mmiliki wa nyumba akajibu, haya hata kama Watanzania wakinyamaza, lakini mioyo yao haitakaa kimya.

“Walitegemea huyo aliyeonyesha nyumba alimokuwa akiishi anapelekwa mahakamani kesho, lakini hakuna, mkilianzisha suala lazima limalizike,” alisema.

MO ALIVYOTEKWA

Mo alitekwa alfajiri ya Oktoba 11, mwaka jana alipokuwa akielekea katika Gym ya Hoteli ya Colosseum iliyoko Oysterbay, Dar es Salaam na aliachiwa usiku wa manane wa Oktoba 20, mwaka huo.

Kulingana na taarifa za awali zilizotolewa na polisi, watekaji hawakuwa Watanzania. Wawili kati yao walikuwa wanaongea Kingereza chenye lafudhi sawia na za nchi za kusini mwa Afrika na mmoja alikuwa akiongea Kiswahili kibovu.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Naibu wake, Hamad Masauni, kwa nyakati tofauti walikaririwa wakisema vyombo vya ndani vya ulinzi vina uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Jumla ya watu 26 walikamatwa kutokana na tukio hilo na baadaye 19 waliachiwa kwa dhamana.

Baada ya kukaa kimya kwa siku nne tangu kutekwa, familia ya Mo ilijitokeza na kutangaza kuwa watatoa zawadi ya Sh bilioni moja kwa yeyote atakayewapatia taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwake.

Kwa mujibu wa jarida la masuala ya fedha la Forbes, Mo anakisiwa kuwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni 1.5 na kumfanya kuwa tajiri namba moja Afrika Mashariki na bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles