29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Biashara Soko la Kariakoo saa 24

*Taa, kamera za CCTV zaanza kufungwa mitaani
*Lengo ni kulifanya kama masoko makubwa duniani

BIASHARA katika Soko la Kariakoo, hasa kwa maduka yanayozunguka eneo hilo, sasa zitafanyika kwa saa 24 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali.


Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Februari 28, mwaka huu alipokutana na wafanyabiashara wa Kariakoo.


Majaliwa alisema kuwa Serikali imepanga mpango wa kubadilisha utaratibu wa kufanya biashara katika eneo la Kariakoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24 kama yalivyo masoko makubwa duniani.


Alisema lengo la mabadiliko hayo ni kukuza uchumi wa taifa na wa wafanyabiashara kwa ujumla.
“Nchi yetu ina usalama na ulinzi wa kutosha, hivyo hatuwezi kushindwa kufanya biashara wakati wote,” alisema Majaliwa.
Kutokana na agizo hilo, MTANZANIA ilitembelea eneo hilo na kuzungumza na uongozi wa soko ili kujua utekelezaji wake umefikia hatua gani.


Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo jana, Kaimu Meneja Mkuu wa soko hilo, Donald Sokoni, alisema kuwa katika kutekeleza agizo hilo la Serikali kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya kufunga taa zaidi ya 70 katika soko hilo ambazo zitasaidia kuongeza mwanga, hasa nyakati za usiku.


Alisema mbali na taa hizo, pia wameweza kufanya ukarabati wa vyoo na bafu katika soko dogo ili kutoa fursa ya wafanyabiashara kupata huduma za kuoga na nyinginezo.


“Tumeanza ukarabati kama ambavyo Serikali imeagiza na tuna imani ndani ya wiki hii ukifika hapa Kariakoo utakuta mabadiliko makubwa. Kwa kuwa tumejipanga kuimarisha utendaji na ulinzi pia ili agizo hili liwe endelevu,” alisema Sokoni.


Alisema kwakuwa soko hilo limeanza kufanya kazi tangu mwaka 1975, miundombinu yake imechoka, hivyo inahitajika maboresho makubwa.
“Uwezo wetu wa kifedha ni mdogo kwakuwa soko hili ni kwa ajili ya kutoa huduma tu, hatuna uwezo mkubwa wa kulifanya liwe la kisasa zaidi, hivyo tunaomba Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iweze kutusaidia fedha za kupaka rangi jengo hili na tuweze kutoa huduma kwa saa 24,” alisema Sokoni.


Alisema wana jumla ya wafanyabiashara 1,673 ambao wanafanya biashara mbalimbali katika soko hilo.
Sokoni alisema wanakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti walionao ambayo haitoshelezi kufanya maboresho ndani ya soko hilo ambalo lina idadi kubwa ya wafanyabiashara na wateja wanaoingia na kutoka.

UFUNGAJI KAMERA ZA ULINZI
Mei 17, mwaka huu, Mtendaji wa Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Manyala A. M, aliandika barua akiwataka wamiliki wa nyumba zote kuhakikisha wanapaka rangi majengo yao na kuweka taa kubwa mbele pamoja na kufunga kamera za CCTV.


“Kutokana na agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ili kuwezesha eneo la Kariakoo kufanya kazi kwa saa 24, wamiliki wote wa majumba mnaagizwa kupaka rangi majengo, kuweka taa kubwa mbele ya jengo na kuweka CCTV kamera. Hatua kali za kisheria utachukuliwa mmiliki atayeshindwa kuwasilisha agizo hili,” ilieleza barua hiyo ambayo ilinakilishwa kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariakoo Magharibi.

HISTORIA SOKO LA KARIAKOO
Soko la Kariakoo ni soko kuu jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla ambalo hufanyika biashara za aina zote za mahitaji muhimu ya kila siku kwa Watanzania na raia kutoka nje ya nchi.


Wafanyabiashara kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, Zambia, Malawi na Visiwa vya Comoro hufika Kariakoo kununua bidhaa mbalimbali ikiwamo nguo na kupeleka katika nchi zao.


Biashara zinafanyika kwa jumla na rejareja. Soko hili linajumuisha majengo mawili makuu (soko kubwa na soko dogo) pamoja na maeneo yanayozunguka majengo hayo.


Soko la Kariakoo lipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na ndiyo chanzo cha eneo zima la Kariakoo kujulikana kwa jina hilo.
Jengo la Soko Kuu la Kariakoo lipo katika kiwanja namba 32, na limezungukwa na mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.
Historia ya jina la Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.


Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la Kariakoo ulifanywa na Serikali mwaka 1970 baada ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuagizwa kujenga soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani.
Matarajio ya Serikali ya kujenga soko hilo yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa jiji soko kubwa la chakula ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa muda wa miaka 50 hadi 70. Mipango ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi Machi 1971.


Ramani ya jengo la soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo, Mtanzania Beda Amuli na wajenzi wakawa Kampuni ya MECCO wakisaidiana na makandarasi wengine.

Ujenzi uligharimu Sh milioni 22.
Shughuli zote za ujenzi zilikamilika Novemba 1975, na soko lilifunguliwa rasmi kwa matumizi ya wananchi Desemba 8, mwaka 1975 na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

TRA NA MKOA WA KODI KARIAKOO
Septemba 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia kwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, alitangaza kulifanya eneo hilo kuwa mkoa maalumu wa kodi.


Kayombo alisema eneo la Kariakoo ni kitovu cha biashara hapa nchini na kwamba litasaidia kwa kila mfanyabiashara kuwa na mashine ya kielektroniki ya kodi (EFDs) na kuitumia ipasavyo.


Alisema kuwa hiyo ni moja ya mkakati wa harakati za kuhakikisha kuwa mapato yote stahiki yanakusanywa ipasavyo na kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles