Bethsheba Wambura
Wanawake nchini wametakiwa kusherehekeea Siku ya Wanawake Duniani kwa kuzingatia chanzo cha sherehe hizo ambazo lengo lake ni kutetea haki zao za msingi za ambazo walikuwa wakizikosa kama kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa.
Siku ya Wanawake duniani huadhimishwa Machi 8, kila mwaka ambapo wanawake wanatambuliwa kwa mchango wa mafanikio yao bila kujali mipaka ya kitaifa, rangi, lugha, utamaduni, uchumi wala siasa.
Hayo yamesemwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala, Daniel Zenda leo Ijumaa Machi 8, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Aziza Mangosongo, katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kiwilaya yameadhimishwa katika kijiji cha Kitangari na kauli mbiu ya mwaka huu ‘Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu’.
“ Nasisitiza juu ya jamii kubadili fikra hasi juu ya wanawake ambazo zimekuwa ni vyanzo vya kuwanyima wanawake katika maendeleo ya jamii, kila siku ingekuwa siku ya wanawake duniani laiti kama pangekuwa na mtizamo sahihi wa kijamii.
“Tunaposheherekea siku hiii ni muhimu kuwa na maneno hayo hapo juu kichwani mwetu, tuache utamaduni wa kusheherekea kwa vile ni ratiba au kwasababu wengine wanafanya hivyo, tusheherekee tukitafakari chanzo cha sherehe zenyewe cha mapambano haya ambayo lengo lake kubwa ni kutetea haki za wanawake,”amesema.
Aidha Katibu Tawala huyo alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa Newala kutumia fursa za kipindi hiki cha mvua kulima mazao ya chakula ili kuepusha kukumbwa na baa la njaa hususani katika wilaya hiyo.