BEIJING, CHINA
SIKU moja baada ya Marekani kutangaza kuanza uchunguzi juu ya iwapo China ilificha ukweli kuhusu mripuko wa kirusi cha corona, mji ambao kirusi hicho kilianzia nchini China umerekebisha takwimu zake kuhusu idadi ya waliokufa kwa ugonjwa huo kwa takribani asilimia 50.
Mamlaka za mji wa Wuhan zilitangaza jana kwamba kulikuwa na vifo 1,290 vya ziada, kando ya vile 3,869 vilivyokuwa vikifahamika awali.
Mamlaka hizo zinasema kuwa sababu ya vifo hivyo kutokufahamika ni ama kuripotiwa kimakosa au kupotoshwa moja kwa moja.
Kauli hii huenda ikaongeza wasiwasi miongoni mwa mataifa ya magharibi dhidi ya uaminifu wa China kwenye janga hili la kilimwengu, ambalo hadi sasa limeshaangamiza zaidi ya watu 140,000 duniani kote.
Marekani, Uingereza na Ufaransa zina mashaka kwamba chanzo hasa cha kirusi cha corona ni maabara moja mjini Wuhan ambayo ilikuwa ikifanya utafiti kuhusu popo, na kwamba China haikulishughulikia tatizo hili kwa umakini kwenye hatua za awali, wala ilikuwa haisemi ukweli.
ITALIA BADO
Wakati Ujerumani ikitangaza kwamba mripuko wa kirusi cha corona sasa umedhibitiwa na kuamuru kuanza kurejea kwa shughuli za kawaida za maisha kuanzia Mei 4 mwezi ujao, huenda hali nchini Italia ikasalia kama ilivyo kwa kipindi kirefu kijacho.
Waziri wa Elimu wa Italia, Lucia Azzolina, amesema kutokana na hali ilivyo hadi sasa, hakuna uwezekano wa kufunguliwa kwa shughuli zozote mwezi Mei.
Akizungumza na gazeti la Corriere della Sera jana waziri huyo alisema hawawezi kubahatisha kuwatoa wanafunzi milioni nane kuingia mitaani kwa sasa.
Italia ndilo taifa la Ulaya lililoumizwa sana na janga la COVID-19, likiripoti vifo zaidi ya 22,000 na maambukizi yanayokaribia 170,000