25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

CHANETA MPYA TUNAHITAJI VITENDO

Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

LICHA ya kupigwa kalenda mara kadhaa kwa uchaguzi mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), lakini mwishoni mwa wiki hii mjini Dodoma  chama hicho kinatarajia kupata viongozi wake wapya.

Chaneta inafanya uchaguzi huo utakaotoa nafasi kwa watu wengine kuvaa viatu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwa ni baada ya kumalizika muda wa waliokuwa madarakani wakiongozwa na mchezaji wa zamani wa mchezo huo, Anna Kibira.

Katika uchaguzi huo nafasi zinazogombewa ni pamoja na mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu na msaidizi wake pamoja na wajumbe sita wanaoingia katika Kamati ya Utendaji ya Chaneta.

Kitendo cha kutajwa tu tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo pamoja na zoezi zima la uchukuaji fomu na ureshaji, limeonekana kutoa tumaini jipya kwa wadau wa mchezo huo  na hii inatokana na hivi sasa netiboli kuonekana ni  sawa na ‘Mfu aliyehai’.

Hili linatokana na ukweli kuwa, kwa sasa Tanzania mchezo wa netiboli bado unaonekana kutokuwa na mwelekeo hasa baada ya baadhi ya wale waliopewa dhamana ya kuiongoza Chaneta kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Wapo wadau wanaodai kuwa netiboli haipewa kipaumbele kama ilivyo kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini, ambapo vyama vya mchezo huo vimekuwa vikipewa motisha kubwa na ndiyo sababu ya kufanya vyema, lakini jambo la kujiuliza je, waliopewa dhamana ya kuongoza mchezo huo nchini wanayatendea haki majukumu yao ipasavyo?

Tanzania ina uwezo wa kufika mbali katika mchezo huo kama nchi nyingine, lakini kwa kuwa viongozi wake wana maendeleo mengi kuliko vitendo, kila siku timu ya Taifa inaishia kuwa wasindikizaji katika mashindano ya kimataifa, huku viongozi wakijisifu kwa kuandaa mashindano ya Taifa wakati hayana faida pale Taifa Queens inapokwenda kucheza nje.

Ni wakati sasa wa kuona Tanzania mpya katika mchezo wa netiboli na hili linapaswa kufanyika mara tu baada ya wapiga kura katika uchaguzi wa Chaneta kutumia haki zao za msingi.

Natarajia kuona mabadiliko makubwa katika netiboli yatakayofanywa na viongozi wapya waliochaguliwa, hasa baada ya kuzisikia sera zao bila shaka mabadiliko ya kweli yataonekana.

Ni wakati wa wagombea katika uchaguzi huo kutambua wadau wa netiboli wanataka nini kutoka kwao, pia kuhakikisha wanajiandaa kikamilifu kutumia nafasi zao wakisaidiana na wizara husika ili kubadilisha taswira ya mchezo huo nchini.

Viongozi watakaochaguliwa wanapaswa kutambua wana jukumu zito la kuhakikisha wanarudisha hadhi ya mchezo huo, kwa kutekeleza vyema ahadi wanazozitoa kwenye kampeni zao, ikiwa ni pamoja na kuibua vipaji kuanzia shule za msingi, kutafuta wafadhirli wa uhakika, kuandaa mashindano mengi ya nje na yale ya kimataifa kwa timu ya taifa.

Siku zote inafahamika misingi mizuri ya mchezo wowote huanzia katika ngazi za chini, hivyo viongozi wanaokuja  wanapaswa kuangalia zaidi vipaji katika shule za msingi na sekondari ili kuweza kuunda kikosi imara kitakachoweza kurudisha heshima ya mchezo wa netiboli na kuweza kufanikiwa kufanya vyema zaidi.

Tanzania ina vipaji vingi vya michezo huu, lakini vimejificha na mara nyingi viongozi wamekuwa na utaratibu wa kuhangaikia wachezaji maeneo ya mjini au wenye majina.

Mbali na hilo, ni wakati wa kuondoa makundi tuliyoyashuhudia yakileta mpasuko mkubwa ndani Chaneta na sasa kuanza mikakati mipya kwa ajili ya maendeleo ya michezo nchini.

Huu ni wakati wa kufanya yale ambayo wadau wa netiboli wanatamani kupata kutoka kwa viongozi, lakini pia  ni muda wa kuinua mchezo huu ili uweze kuitangaza vyema Tanzania katika medali ya michezo kitaifa na hata kimataifa, kwa sasa wadau wanahitaji vitendo zaidi na si porojo za mdomoni.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles