Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kusini kimepinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Reli Manispaa ya Mtwara Mikindani baada ya kubaini zoezi hilo halikuwa huru na haki.
Mara baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa, Katibu wa Kanda ya Kusini ambaye pia alikuwa wakala wa majumuisho, Philbert Ngatunga amesema tangu mwanzo wa maandalizi ya kufungua vituo hadi kubandika matokeo mchakato haukuwa na haki kutokana na kuminywa kwa kanuni na taratibu za uchaguzi ambapo mawakala walinyimwa nakala ya fomu ya malalamiko ambayo inapojazwa wakala anapaswa kuondoka nayo.
“Sisi tunajua kanuni na taratibu za uchaguzi zikoje na zinapaswa kuwaje wakala anapoomba fomu ya malalamiko anapewa fomu mbili ili abaki na moja lakini wa kwetu ameambiwa kuwa haruhusiwi kuhoji kwanini hapewi nakala yake hii inaonyesha wazi kuwa walikuwa na mpango ndio maana walimnyima ile fomu.
“Unajua baada ya uchaguzi kumalizika mawakala wanapaswa kushiriki kuhesabu vibutu vya pembeni ya kitabu cha kupigia kura kabla kura halisi hazijahesabiwa zoezi hilo halikuhusisha mawakala na waliwazuia kwa kuwaambia kuwa hawahusiki,” amesema Ngatunga.
Katika uchaguzi huo, Kata ya Reli CCM ilishinda kwa kura 422, Chadema kura 356, Chama cha Wananchi (CUF) 21, ACT-Wazalendo 27, NCCR-Mageuzi 2 na huku.
Katika hatua nyingine Chama cha ACT-Wazalendo kimekubali matokeo hayo ya uchaguzi katika kata ilizoshiriki na kudai kuwa uchaguzi huu waliutumia kama fursa ya kuzungumza na wananchi.
Kwa mujibu wa kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe katika kata zote 43 nchini zilizogombewa, ACT Wazalendo waliweka wagombea kwenye kata 17 tu na matokeo ya kata zote na hakuna kata waliyoshinda.
“Wapiga kura wameamua na sisi tumekubali. Tunafanya tathmini ya matokeo nchi nzima na tutazungumza na wananchi. Tunawashukuru sana kwa kura tulizopata. Tutazienzi kwani ndiyo haki yetu. Tunajiandaa na chaguzi ndogo zinazokuja ikiwamo za ubunge kwenye majimbo yaliyo wazi.
“Tutatumia mafunzo tuliyoyapata kwenye chaguzi ndogo hizi kujipanga na chaguzi zinazokuja. Kwetu sisi uchaguzi ulikuwa fursa ya kuzungumza na wananchi na kufikisha ujumbe wetu kwani kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kunatunyima fursa hiyo. Hatutachoka kuendelea kusambaza sera zetu kwani tunaamini ni bora zaidi na zinazoweza kuleta unafuu kwa wananchi wetu,” amesema Zitto.