Na Asifiwe George, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni linawashikilia vijana 10 waliojifanya wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuandamana katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa kile walichodai kwamba ni kupinga hatua ya Dk. Slaa kustaafu siasa kutokana na Edward Lowassa kujiunga na chama hicho.
Vijana hao waliokuwa wamevaa sare za Chadema walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti huku wakiimba wimbo wa‘hatumtaki Lowassa’… ‘hatumtaki Lowassa’.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema, wanaendelea kuwahoji vijana hao kujua sababu ya maandamano hayo.
Alisema kutokana na watu hao kukamatwa maeneo mbalimbali ikiwamo makao makuu ya Chadema watahojiwa kwa wiki moja.
Wambura alisema polisi hawakuwa na taarifa ya kufanyika maandamano hayo na hawakutoa kibali chochote kwa vijana hao kuandamana.
Chanzo cha habari kilichokuwa eneo la Morocco wilayani Kinondoni kilisema baada ya hapo yalifika magari matatu (Defender) yakiwa na polisi ambao walipiga mabomu ya machozi kuutawanya umati huo.
Mabomu hayo yalisababisha watu hao kukimbia huku na kule kujinusuru lakini wengine walikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Osterbay kilichopo wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Awali taarifa zilizosambaa katika mitandao ya jamii zilisema vijana hao ni mkakati uliokuwa umeandaliwa na CCM kuwavalisha nguo za Chadema ionekana Lowassa anapingwa ndani ya chama hicho.
Taarifa hiyo ilisema katika mkakati huo unaotajwa kuratibiwa na vigogo kadhaa wa CCM akiwamo mmoja wa wagombea ubunge jijini humo (jina tunalo).
Taarifa hiyo ilisema, “vijana wa CCM watavalishwa nguo za Chadema, wataandamana wakimuunga mkono Dk. Slaa na kumpinga Lowassa”.
Ilidaiwa kuwa maandamano hayo yalitakiwa kuishia Ikulu kwa mapokezi ya makubwa.
Chanzo hicho kilisema mgombea huyo alisuka mkakati huo akidai ni maagizo kutoka uongozi wa juu wa chama na serikali.
Diwani wa ubungo kwa tiketi ya Chadema, Boniface Yakobo, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa
tangu jana usiku chama hicho kilipata taarifa ya kikao kilichofanyika Kariakoo, kingine Ubungo na kiliratibiwa na Didas Masaburi(aliyekuwa Meya wa Dar es Salaam na hivi sasa ni mgombea ubunge wa CCM Ubungo) ambaye alinunua fulana za Chadema.
Alisema walizitilia shaka kwa sababu tangu Chadema ianze haijawahi kutokea kununuliwa tisheti nyingi kiasi hicho.
Kijana huyo alipofuatiliwa ilionekana amekabidhi fulana hizo kwa Didas Masaburi na (jana) juzi saa 12:00 jioni alionekana akiwa na vijana zaidi ya 100 akifanya nao mkutano, alisema.
Alieleza kuwa baada ya tukio hilo vijana hao walitakiwa kufika Ikulu kushikana mkono na Rais wakielezwa kuwa kibali kilikuwa kimetolewa na Jeshi la Polisi.
Alisema vijana hao walikuwa wamejipanga katika makundi mawili na saa 5:00 asubuhi kundi la kwanza lilikuwa likitokea Mwenge jingine Ubungo na kundi la kwanza lilipofika Mkwajuni lilisimama.
“Sisi Chadema tulikuwa tumejipanga na tulikuwa tumewazunguka lakini kabla ya kuwakamata polisi waliwakamata vijana hao kabla sisi Chadema hatijawakamata,” alisema na kuongeza:
“Baadhi ya vijana walikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi lakini baada ya kufika kituoni hapo baadhi yao waliachiwa na kujichanganya na wananchi wa kawaida.
“Wenyewe wamesema hatua hiyo iliratibiwa na ofisi ya CCM Ilala na Kinondoni na Didas Masaburi.
“Sisi tunawaambia siasa hizi CCM hazina tija, kwa tukio la jana na muendelezo wa leo inaonekana kuna kitu wanakijua na walikuwa wanataka ionekane ni Chadema.
“Tunashukuru umma umetusaidia watu wote waliokimbizwa wamekamatwa na wananchi na raia… tunamshukuru mtendaji kata kuwahifadhi hao watu ili wasiuawe katika maeneo yale”.