29.5 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Siri yafichuka mkutano wa Dk. Slaa

??????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kutangaza kuachana na siasa na kushusha tuhuma kwa chama chake, maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), imebainika kuwa kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari alikutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Dk. Harison Mwakyembe.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Slaa ambaye alimshambulia mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, alikiri kukutana kwa takribani saa mbili na Dk. Mwakyembe akisema lengo lilikuwa ni kujikumbusha taarifa ya Richmond na ndipo alipopata ujasiri wa kutamka aliyoyasema.

“Hivi kukaa kwangu na Mwakyembe kuna kosa gani? Je, ni dhambi? Watanzania sijui kwanini huwa hawataki kuelewa mambo, mimi nilionana na Mwakyembe kabla ya kuanza mkutano wangu na waandishi wa habari, na tulikaa kuanzia saa nne asubuhi hadi sita mchana.

“Katika suala la Richmond hakuna ‘source ya information’ (chanzo cha habari) zaidi ya Mwakyembe na ndiyo maana nilikaa naye…nilirudia kufanya utafiti.

“Sasa anayeshangaa Dk. Slaa kuongea na Mwakyembe nadhani kwa bahati mbaya akili yake haina upeo wa kutosha, kwa sababu unapofanya ‘research’ (utafiti) lazima urudi kwenye ‘source’ (chanzo) ya hilo jambo na ndiyo maana nilikuwa na jeuri ya kuzungumza kwa kujiamini,” alisema Dk. Slaa.

USALAMA WA TAIFA

 Dk. Slaa pia alikiri kusindikizwa na usalama wa taifa akisema alifanya hivyo kwa sababu tangu amejiuzulu ukatibu mkuu wa Chadema, amekuwa akitishwa hivyo alitoa taarifa polisi kwa ajili ya kulindwa.

“Nikiwa pale mkutanoni nilihoji kama polisi wapo ili tu watu wajue kuwa pale kuna usalama, nilisema kabisa kwamba hakuna kipindi nilichopata vitisho kama hiki, kuliko hata wakati nilipotangaza ‘list of shame’ pale Mwembeyanga, hivyo nilitoa taarifa polisi ili nilindwe.

“Tangu nimejiuzulu ukatibu mkuu, nyumba yangu imekuwa ikilindwa na polisi. Polisi ni maadui zetu, lakini kuna wengine ni wazuri kwa ajili ya usalama,” alisema Dk. Slaa.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, baadhi ya taarifa zilizokuwa zikizagaa zilidai kuwa umeandaliwa na watu wa CCM na Serikali.

MTANZANIA ilipomuuliza Dk. Slaa kuhusu suala hilo, hakuwa na jibu la moja kwa moja.

 

 GHARAMA ZA MKUTANO

 Alipoulizwa juu ya gharama alizotumia kufanya mkutano wake kwenye Hoteli ya Serena na kuurusha moja kwa moja kwenye vituo takribani vitano vya televisheni, wakati akisema yeye ni masikini, Dk. Slaa alihoji: “Hivi kwa uzito wa hotuba ile ulidhani ningefanyia Manzese?”

Gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye baadhi ya televisheni nchini, zinaanzia Sh milioni 6 kwa saa na mkutano wa Dk. Slaa ulirushwa kwa takribani saa moja na nusu.

Hivyo gharama za kurusha matangazo hayo kupitia televisheni hizo achilia mbali ukumbi, redio zilizorusha moja kwa moja, luninga mbili zilizorudia matangazo hayo juzi usiku na kampuni iliyoandaa mkutano huo ni takribani Sh milioni 45.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Dk. Slaa alisema yeye si mtu mwenye uwezo na hata fedha zake huwa zinatumiwa na mke wake kukijenga chama, hivyo yeye na familia yake huishi kwa kula mihogo.

Jana MTANZANIA ilipomtaka Dk. Slaa ataje gharama ya mkutano huo na nani amegharamia, alisema: “Bado nasubiri gharama za mkutano wangu na kampuni inayofanya kazi hiyo wakiniletea nitakwambia.

“Niliamua kufanya mkutano ule kwa kuwa Taifa limegawanyika katika sehemu mbili, wengine ni wale wanaounga mkono ufisadi ambapo ndiyo wanatumia fedha kufanya jambo lolote, kundi jingine ni lile ambalo linapinga, na ndiyo maana nikawatahadharisha Watanzania wawe makini na mafisadi,” alisema Dk. Slaa.

PICHA NA LIPUMBA, MWIGULU

Akizungumzia kuhusu picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, alisema picha hiyo ni ya tangu rais huyo alipokuja nchini.

“(Anacheka) Yaani ninawashangaa sana Watanzania…hivi watu tukimbiane? Lakini bahati mbaya picha hiyo ni ya siku nyingi, tangu rais wa Ujerumani alipokuja nchini, na siku ile Mwigulu alikuja kuiwakilisha Serikali, mimi niliwakilisha chama changu na Lipumba aliwakilisha CUF,” alisema Dk. Slaa.

 

 AMJIBU LISSU

 Pamoja na mambo mengine, alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu afanye utafiti kabla ya kuzungumza chochote na vyombo vya habari.

“Lissu amekuwa mtu wa kukurupuka…hivi alijua mimi niko wapi, kwa anachofanya anapoteza ‘credibility’ yake, na mtu makini anafanya tafiti kabla ya kutoa ‘press’. Sasa aende kwenye kumbukumbu ya chama na atoe vocha yoyote iliyosainiwa halafu aniambie kuwa nilichukua mshahara wa chama,” alisema.

Akizungumzia kuhusu nyumba anayoishi, Dk. Slaa alisema alichangiwa na rafiki yake ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hivyo alimtaka Lissu aweke hadharani uthibitisho wowote kama nyumba hiyo ni ya chama.

“Hivi mtu ukichangiwa nyumba ndiyo umelipiwa na chama? Nyumba yangu nilichangiwa na rafiki yangu Mbowe, sasa Lissu aweke hadharani kama nyumba ni ya chama,” alisema.

 

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles