31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Apuuzwe

Pg 1 MBOWEPg 4Na Grace Shitundu, Dar es Salaam

MWENYEKITI Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amewataka Watanzania kumpuuza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kwa kauli zake zilizojaa uchochezi na propaganda za siasa.

Pia alionya kauli za ovyo zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba wapinzani wakishinda vyombo vya ulinzi vitachukua nchi.

Alisema jeshi la Tanzania linasimamia misingi yake na kiongozi yeyote atakayeingia madarakani litafanya naye kazi kwa kuwa wote ni Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kufafanua mambo mbalimbali yalitamkwa  na Dk. Slaa juzi, Mbatia alisema  tuhuma alizozitoa kiongozi huyo zinalenga kuleta mpasuko katika taifa na kuvunja amani ya nchi.

Alisema hotuba nzima ya Dk. Slaa ililenga kumshambulia moja kwa moja Mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kwa sababu amekuwa tishio kwake na kwa CCM.

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema mara zote propaganda kama hizo huwa zinafanywa na chama tawala ambacho kimekwisha kuona viashiria vya kuondolewa madarakani kupitia sanduku la kura.

Mbatia alitoa mfano kuwa kitendo cha Dk. Slaa kuwasingizia baadhi ya viongozi wa dini kwamba walihongwa na Lowassa ili wamuunge mkono ni hatua ya kuwataka waumini wasiwaamini viongozi wao jambo ambalo ni hatari kwa amani ya nchi.

“Hoja alizozitoa ni nyepesi ambazo Watanzania wanatakiwa kuzipuuza na wasikubali mpasuko hasa unaoletwa kwa mlengo wa imani ya dini.

“Kuwahusisha viongozi wa dini na tuhuma za uongo ni siasa nyepesi za mtaroni.

“Kusema eti Lowassa anaungwa mkono na Walutheri kwa sababu ni wenzake ni mpasuko mkubwa katika nchi,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa NCCR Mageuzi alisema alisikitishwa na uongo uliosemwa na Dk. Slaa kwamba hakuunga mkono kuingia kwa Lowassa Chadema kwa sababu mwanasiasa huyo alishiriki kwa ukamilifu mchakato mzima wa kumshawishi Lowassa na wenzake kujiunga na Ukawa.

“Nimesikitishwa sana na uongo uliosemwa jana na kaka yangu Dk. Slaa kwa sababu  alishiriki katika kumshawishi Lowassa na wengine kujiunga nasi katika harakati za mabadiliko ya kweli,”alisema Mbatia.

Alisema kusema kwamba Lowassa alitoa ahadi ya kujiunga na Ukawa akiwa na kundi kubwa la wana CCM ni kutunga na hauna mashiko ya katiba na kanuni kwa vile  hakuna katiba yoyote ya chama cha siasa yenye masharti kama hayo.

“Lowasa alipokuja Ukawa hakutoa ahadi ya kuja na viongozi na pia hakuna masharti aliyopewa kwa sababu alifuata taratibu zote za kujiunga Chadema.

“Mbona mwaka 1995 yeye (Dk. Slaa) alipokatwa na CCM na kuhamia upinzani hakupewa masharti wala kubaguliwa?

“Katiba ndiyo inayotoa utaratibu wa mtu kujiunga na chama sasa yeye ni nani mpaka awe juu ya Katiba ya Chadema? Mbona yeye hakubaguliwa na aliendelea kufaidika hadi akagombea urais?” alihoji Mbatia.

Kuhusu kauli kwamba Dk. Slaa alikuwa hajaomba wala kuteuliwa na chama chake kugombea urais, Mbatia alisema kabla ya kuingia   Lowassa Ukawa, tayari Chadema kilikuwa kimekwisha kumteua Dk. Slaa kuwa mgombea ambaye angepambana na wenzake kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR.Mageuzi.

“Si kweli kwamba Dk . Slaa hakuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais, bali chama chake kilikwisha kumteua na yalipojitokeza majina ya Profesa Ibrahim Lipumba na Dk. George Kahangwa, alisema yeye ndiye mwenye vigezo vyote vya kuteuliwa kuwa mgombea wa umoja huu.

“Tulifanya vikao mbalimbali kikiwamo tulichofanya nyumbani kwa Profesa Lipumba lakini hatukufikia muafaka, lakini baada ya Lowassa kujiunga tulimwomba kwa pamoja agombee urais.

“Sababu iliyotufanya tumshawishi Lowassa agombee nafasi hiyo ni nyota yake ya siasa aliyonayo. Je, haya mafuriko tunayoyapata na tuliyopata pale Jangwani tungeyapata?

“Hizo tuhuma za ufisadi wanazozitoa juu ya Lowassa …tukianza kuwataja kwa masakata yaliyotokea katika uongozi wa Rais Kikwete (Jakaya) hakuna hata mtu mmoja atakayebaki.

“Sakata la EPA, BoT (Benki Kuu), Deep green, Richmond, vichwa hewa vya treni… hakuna atakayebaki msafi. Hivyo ufisadi si mtu bali mfumo,” alisema Mbatia.

Alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, anaweza kueleza namna alivyosimamia uuzwaji wa nyumba za serikali.  Je, huo siyo ufisadi?

Mbatia alisema   wale wanaotaka mdahalo na Lowassa si saizi yake bali yeye ndiye anaweza kupambana nao.

Alimtaka Waziri wa Uchukuzi, Samueli Sitta, kuwaeleza Watanzania fedha za serikali alizotumia kujengea nyumba ya Spika kule Ulambo wakati akijua usipika ni kazi ya muda tu.

 

MBOWE AMJIBU DK. SLAA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Chadema siyo mali yake wala mali ya mtu yeyote bali ni mali ya wanachama.

Kutokana na hali hiyo, amesema kama kuna mtu na mkewe wana mawazo tofauti na wenzao ndani ya chama hicho, watu hao wataachwa   chama kiendelee kusonga mbele.

Mbowe alitoa kauli hiyo mjini hapa jana alipohutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, waliohudhuria mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Nduwa.

“Makamanda najua kuna watu wamekuwa wakiniuliza juu ya kauli iliyotolewa jana (juzi) na aliyekuwa Katibu Mkuu wetu, Dk. Wilbrod Slaa.

“Napenda niwaambie kuwa mwaka 1992 tulipoanzisha Chadema, ilikuwa ni kama safari ya treni kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma. Tulipoanza safari hiyo na kufika Pugu, abiria wengine walishuka na wengine wakapanda na tulipofika Morogoro, abiria wengine wakashuka na wengine wakapanda na mwaka huu Oktoba 25 safari yetu itafika Kigoma.

“Chadema siyo mali yangu, wala siyo mali ya mtu yeyote bali ni mali ya wanachama, anayedhani Chadema ni mali yake, ataondoka, chama atakiacha.

“Kamati Kuu, Baraza Kuu na mkutano mkuu wa Chadema viliamua Lowassa ndiye awe mgombea wa urais kupitia Chadema pamoja na Ukawa.

“Sasa, kama kuna mtu na mkewe wana mawazo tofauti na sisi, hatuna muda wa kupoteza, tutawaacha, tutasonga mbele,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Kwa mujibu wa Mbowe, Watanzania wanahitaji mabadiliko na   ili mabadiliko hayo yafikiwe  ni lazima kila mmoja ashiriki kadiri atakavyoweza.

Wakati huo huo, Mbowe alisema kutokana na muda mfupi wa kampeni uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mgombea wao wa urais  na mgombea mwenza wake, Duni Haji, hawataweza kufika majimbo yote nchini.

Kutokana na hali hiyo, alisema wamelazimika kuunda vikosi vinne vya kampeni vitakavyotumia helkopta nne kuzunguka nchi nzima.

“Nchi yetu ina majimbo 215 Tanzania Bara na ina majimbo 50 Zanzibar. Katika hali ya kawaida, mgombea urais na mgombea mwenza wake  hawataweza kuyafikia majimbo yote kabla ya tarehe ya uchaguzi.

“Kwa hiyo tumeunda vikosi vinne vya kampeni vitakavyotumia helkopta nne kuanzia wiki ijayo ili maeneo atakayoshindwa kufika mgombea urais na mgombea mwenza, vikosi hivyo vifike,” alisema Mbowe.

Aliwataja baadhi ya watakaokuwa katika vikosi hivyo kuwa ni  aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje, aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na aliyekuwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na yeye mwenyewe.

LOWASSA AANZA NA HELKOPTA

Wakati huo huo, Lowassa jana alianza kutumia helkopta katika kampeni zake baada ya kufanya hivyo katika majimbo mawili ya Namtumbo na Mbinga Magharibi mkoani Ruvuma.

Pamoja na kufanya kampeni katika majimbo hayo, jana saa 11 jioni, aliwasili mjini Sumbawanga akitumia ndege ya kukodi ya Kampuni ya TANZANAIR iliyokuwa na namba za usajili 5H-DJS.

Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga, Lowassa alilakiwa na maelfu ya wananchi waliokuwa wamejaa uwanjani hapo wakimsubiri.

Baadhi ya wananchi hao walikuwa na mabango mbalimbali yakiwamo yaliyosema, ‘Dk. Slaa tumekusikia ila haturudi Misri, lazima tufike Kaanani’, ‘Chadema bila Slaa inawezekana’ na jingine lilisema ‘Slaa rudisha nyumba na gari la Chadema’.

Lowassa alipowasili uwanjani hapo akiwa na Mbowe, uwanja ulilipuka kwa shangwe na baadaye alikutana na mapokezi makubwa ya wananchi waliokuwa wamejipanga mistari miwili barabarani kuelekea Uwanja wa Shule ya Msingi Nduwa.

Akiwahutubia wananchi hao, Lowassa aliwasisitizia umuhimu wa kumchagua yeye, wabunge na madiwani wa Ukawa kwa kuwa amedhamiria kuwakomboa wananchi walioelemewa na umasikini.

Pia aliwahakikishia wananchi hao kwamba kama watampigia kura nyingi na kufanikiwa kuingia madarakani, hawatajuta kumchagua kwa sababu nchi itapiga hatua katika maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles