Na TIMOTHY ITEMBE
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Tarime wameonywa kuacha tabia ya kuwachafua wagombea wenzao katika mitandao ya jamii katika kipindi hiki cha uchaguzi wa ndani wa chama.
Onyo hilo lilitolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mukaruka ambaye alisema watakaobainika kujihusisha na tabia hiyo hatua za nidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
“Chama hakitawavumilia wanachama na wagombea au wanachama wowote ambao wanatumia njia ya kuwachafua wenzao wanaogombea kwenye mitandao ya jamii.
“Niseme kwa sasa tuko makini na watakaobainika watachukuliwa hatua za nidhamu,” alisema.
Aliwataka wanachama waliokisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kutopoteza muda wao kwa kugombea nafasi za uongozi kwa kuwa wataenguliwa.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Tarime, Mathias Lugola aliwasihi wanachama kuendelea kujitokeza kuwania nafasi za uongozi wa jumuiya hiyo.
Nafasi hizo ni mwenyekiti, katibu wa siasa na uenezi, wajumbe wa halmasghauri kuu ya wilaya nafasi 10, wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa nafasi tatu na wajumbe wa mkutano mkuu mkoa nafasi tano.