MONGELLA ATOA SIKU 10 KWA MWEKEZAJI KUFANYA USAFI

1
515

 

Na FREDRICK KATULANDA


MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella  amempa siku 10  mwekezaji  aliyebinafisishwa Kiwanda cha Ngozi cha Mwanza Tanneries Ltd,  kufanya usafi na  kuanza mpango wa kufufua kiwanda hicho ndani ya  miezi sita ijayo.

Mongella alifika kiwandani hapo akitokea kukagua ujenzi wa barabara ya Uwanja wa Ndege ambayo inapanuliwa kuwa njia mbili.

Kiwanda hicho   kilibinafisishwa kwa mwekezaji African Tanneries Ltd.

Aliagiza vifaa mbalimbali vilivyohifadhiwa ndani ya kiwanda hicho kuondolewa katika   siku 10.

Alisema kiwanda hicho ni moja ya raslimali zilizoachwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu  Nyerere.

Rc alisema viwanda hivyo vilikuwa vikichangia kukua kwa uchumi wa Mwanza na Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuchakata ngozi za wafugaji lakini kimekuwa hakitumiki kwa muda sasa na   kimegeuzwa kuwa ghala.

“Nimeamua kupita hapa kwa kuwa rais amekuwa akikitaka kiwanda hiki kifanye kazi.

“Kwa wale ambao walibinafsishwa viwanda kama hivi na wakashindwa kuviendesha viwanda hivi tutaona namna ya kuchukua hatua.

“Sasa ninaagiza kiwanda hiki kisafishwe mpaka kufikia Julai 20  mwaka huu kiwe safi na mwekezaji aje na mpango kazi wake wa kuanza uzalishaji katika kipindi cha miezi sita,” alisema.

Mongella alisema ikifika Julai 20  mwaka huu atarudi katika kiwanda hicho na kumuomba msimamizi wake kuwaarifu wakubwa wake wawepo.

Alisema wamiliki hao  wafike wakiwa na mpango kazi ambao utaonyesha namna ambavyo wataanza kufufua kiwandi hicho katika   miezi sita.

“Nimeagiza hapa kufanyiwe usafi, ikifika tarehe 20 nitarudi kuja kuangalia utekelezaji wa maagizo yangu.

“Ikiwa nitakuta hakujafanyika lolote mimi na timu yangu ya mkoa tutapanga cha kufanya, shida yetu tunataka kuona kiwanda hiki kinaanza kazi,” alisema.

Msimamizi wa Kampuni ya African Tanneries Ltd, Mathew Chacha alisema ameyapokea maelekezo hayo na kuhaidi kuwa atayafikisha kwa uongozi wake kwa ajili ya utekelezaji.

Mongella pia alitembelea Kiwanda  cha Nguo cha Mwanza, Mwatex (2001) Ltd ambako alijonea uzalishaji wa khanga na vitengo.

1 COMMENT

  1. Alichofanya Mhe Mongella ni sawa kabisa. Ni kitendo ambacho kingepaswa kufanywa na kila mkuu wa mkoa/wilaya ambaye kwenye eneo lake kuna kiwanda ambacho kimebinafsishwa lakini waliopewa kiwanda hicho wakakiacha kiharibike au kukigeuza stoo.

    Kwa vile Tanzania tuko kwenye mkakakti wa kujigeuza kuwa nchi ya viwanda, tunatakiwa kufufua viwanda VYOTE ambavyo vilikufa. Wapewe wazawa na waekezaji wa nje ambao wana uwezo wa kuvifufua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here