Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Anamringi Macha amesema ameridhishwa na kazi zilizofanywa katika Jimbo la Segerea na kusifu ushirikishwaji uliopo baina ya mbunge na madiwani.
Amesema mbunge wa jimbo hilo, Bonnah Kamoli, amekuwa daraja zuri la kuunganisha Serikali kuu na jimbo na kuhakikisha juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaeleweka vizuri kwa wananchi.
Macha ameyasema hayo Februari 11,2024 wakati wa mkutano mkuu maalumu wa Jimbo la Segerea ambapo Bonnah aliwasilisha utekelezaji wa Ilani ya CCM na mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia katika jimbo hilo.
Katika mkutano huo Bonnah aliwasilisha ilani kielektroniki kwa utekelezaji ilani ulivyofanyika katika kata zote 13 za jimbo hilo kupitia video.
“Lazima nikiri hii ‘documentary’ imenifupishia kazi, mwenye macho haambiwi tazama, tulizoea taarifa za kusomeana lakini mbunge ametuonyesha taarifa hizo mubashara.
“Kuna ushirikishwaji mkubwa na wa kiwango cha juu kati ya mbunge na madiwani, huu ni mfano wa kuigwa na kama mtu angeniuliza kikosi hiki (mbunge na madiwani) vipi…ningesema kinafaa kwa 2025,” amesema Macha.
Amesema katika baadhi ya maeneo kuna mgawanyiko ambapo baadhi ya madiwani wamekuwa hawashirikiani na wabunge licha ya kwamba wote dhamana zao zinafanana.
“Bonnah angeweza kutumia dakika 40 au zaidi kutoa maelezo badala yake amewaachia wenzake (madiwani) waeleze yaliyotekelezwa kwenye kata zao. Ana uhakika, hana mashaka na watu alionao na haya ndiyo mahusiano tunayotaka ya utendaji kazi.
“Hapa Segerea nasema kweli, sina nia yoyote ya kuwapigia kampeni kabla ya muda lakini kama mtu anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi tusiogope kumsifu na nimemfuatilia kwa muda mrefu,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu huyo pia amewatahadharisha watendaji wa chama na Serikali kuacha kupanga safu za wagombea badala yake wazingatie kanuni na taratibu.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema; “Bonnah ni miongoni mwa wabunge wachache na tunu katika wilaya yetu na heshima kubwa kwa chama.