Na Waandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimetumia mbinu za kisayansi na kuhakikisha kimeshinda kata 42 kati ya 43 zilizofanya uchaguzi wa marudio juzi, huku Tume ya Uchaguzi (NEC), ikisema uchaguzi huo umekuwa na mafanikio kwa asilimia 95.
Kauli hizo zimekuja siku moja baada ya uchaguzi huo, ambao Chadema iliambulia kata moja, huku ikisusa kushiriki kwenye hatua za mwisho za upigaji kura katika kata tano za Arumeru Mashariki ikidai chama tawala kimecheza rafu.
CCM na mbinu za kisayansi
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema chama kikuu cha upinzani kiache visingizio kutokana na ushindi wao.
Àlisema mwaka 2015 walikuwa na wanachama milioni 8 nchi nzima na sasa wana wanachama milioni 12 na takribani asilimia 67.67 wamejitokeza kukichagua chama hicho na kupata ushindi wa kishindo.
Aliongeza kuwa ushindi huo ni kutokana na akili na matumizi ya sayansi ya siasa hadi kuhakikisha wanaupata, ikiwa ni pamoja na kujisahihisha makosa waliyokuwa wameyafanya kwa wananchi na katika chaguzi mbalimbali zilizopita.
Alisema ushindi huo pia ni ishara tosha ya kupata ushindi katika uchaguzi wa majimbo ya ubunge, likiwamo la Singida Kaskazini.
“Narudia tena, Singida Kaskazini tutashinda na majimbo mengine tutashinda yanayorudia uchaguzi, kwa kuwa chama makao makuu kimetoa maelekezo ya viongozi wake wa kata, matawi, mashina na ngazi ya taifa kufanya kazi vizuri ili kuijenga CCM mpya tuitakayo,” alisema Polepole.
Akizungumzia kuhusu vurugu zilizotokea na watu kuumia, alisema ziliongozwa na chama kikuu cha upinzani pasipo kutaja jina, na kwamba waliobainika katika vurugu hizo wanapandishwa mahakamani.
Aliongeza kuwa vyama vya upinzani vinapenda kutumia mitandao kulalamika kuhusu kuonewa au kufanyiwa vurugu, huku wao wakitumia Jeshi la Polisi na kufuata sheria zaidi.
Alimtolea mfano mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani bila kumtaja jina, kwamba aliandika katika mtandao wakati watu wakipiga kura, kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani, lakini baada ya muda mfupi aliona akiwa anaruhusu kufanyika kwa vurugu katika uchaguzi maeneo mbalimbali, huku akiwataka baadhi ya wagombea wakiwamo wa Arumeru wajitoe.
Alisema alishangazwa sana na kauli ya mwenyekiti huyo kumwona anaweka mpira kwapani wakati awali alijinasibu ushindi.
Polepole alisema mwenyekiti huyo alionyesha dhahiri kwamba ni mwoga na kwamba hajakomaa kisiasa.
“Kwanza huyo mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani tulipita kwenye moyo wao huko Hai, ni kwamba hana chochote alichofanya zaidi ya maneno, hana uwezo wa kutumia fursa katika kuwawakilisha wananchi wake,” alisema.
Hata hivyo aliendelea kuwashutumu wapinzani kwa kusema kuwa siasa kama zilizofanyika, kwao hazipewi nafasi na wao walijipanga kufanya siasa za kistaarabu.
Alisema chini ya Rais Dk. John Magufuli na mwenyekiti wao wa chama, wanaahidi kuendelea kufanya vizuri.
Polepole alisema kuwa Rais Magufuli anafanya vizuri kiutendaji licha ya wapinzani wao kumshambulia mitandaoni.
Chadema waendelea kupinga
Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema, alisema uchaguzi huo haukuwa huru na haki na kwamba baadhi ya taasisi za Serikali zilitumia vibaya madaraka yake kwa lengo la kuisadia CCM.
“Jamani uchaguzi huo haukuwa na mazingira rafiki wala ya ushindani wa kisiasa, vyombo vya dola vilitumika kuharibu mazingira ya uchaguzi huku wafuasi wa Chadema wakijengewa mazingira magumu na yenye hofu,” alisema Lema.
Wasemavyo wasomi
Baadhi ya wasomi kutoka vyuo vikuu nchini, wameitaka Serikali kufufua mchakato wa Katiba mpya ili uruhusu Tume Huru ya Uchaguzi (NEC), ambayo ikisimamia uchaguzi wadau watakuwa na imani na matokeo yatakayotangazwa.
Msomi wa siasa, Profesa Mwesiga Baregu, alisema: “Bila ya Tume Huru ya Uchaguzi, hakutakuwa na matokeo ya haki, kwa sababu wanaosimamia chaguzi hizo ni wateule wa rais na makada wa CCM, hivyo basi watakubali vipi washindwe wakati wanatetea kibarua chao?”
Profesa Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema hadi sasa, wakurugenzi wa halmashauri ambao ni wasimamizi wa uchaguzi, jambo la kwanza wanaloangalia ni masilahi ya chama chao.
Alisema hali hiyo inawafanya waingie kwenye kundi la kubatilisha matokeo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Josiah Kibira kilichopo mkoani Kagera, Dk. Azavel Lwaitama, alisema kasoro zinazojitokeza katika uchaguzi ambazo ni pamoja na kupigwa kwa baadhi ya wanachama, matokeo batili na mengine ni zile zile.
“Kila tunapofanya uchaguzi, lazima kasoro hizi zijitokeze, hali ambayo inasababisha kuwepo kwa malalamiko ya kutokuwa na imani na washindi, hivyo basi Serikali inapaswa kuziangalia kasoro hizo na kuzifanyia kazi ili kuepusha malalamiko hayo.
“Ningeshangaa kama ningesikia upinzani umeshinda wakati wasimamizi ni wa CCM, tena nahisi wakurugenzi ambao wamesimamia uchaguzi kwenye maeneo hayo wangefukuzwa kazi, ifike wakati wananchi wakatae suala hili na kupiga kelele ya uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema Dk. Lwaitama.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa, alisema vyama vya upinzani bado vina kazi kubwa ya kuhakikisha vinapata ushindi kutokana na mfumo uliopo wa uchaguzi kusimamiwa na chama tawala.
Alisema hadi sasa nchi haijafika mahali uchaguzi unaweza kuwa huru na haki ili kuwapa nafasi wapigakura waweze kumchagua kiongozi wanayemtaka, badala yake bado wapo kwenye mfumo wa uchaguzi kusimamiwa na watendaji wa Serikali ambao ni makada wa CCM.
“Tuna safari kubwa ya kuhakikisha demokrasia inatawala kwenye uchaguzi mbalimbali nchini, kwa sababu wasimazi wa uchaguzi ni wateule wa Serikali ambao wana masilahi na CCM,” alisema Dk. Kahangwa.
Mhadhiri mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema vyama vya upinzani vinapaswa kujitafakari na kusimamisha wagombea ambao wataweza kukubalika kwenye chaguzi zijazo kuliko kuchagua watu ambao hawakubaliki.
Alisema matokeo hayo iwe sehemu ya kusahihisha makosa yaliyojitokeza na kujipanga upya ili ifikapo 2020 waweze kusimamisha wagombea ambao wataweza kuwanadi na kukubalika.
“Matokeo ya uchaguzi mdogo yanaonyesha wazi kuwa wagombea waliosimamishwa na upinzani hawakubaliki, ndiyo maana wameshindwa kupata ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani, hivyo basi wanapaswa kujitafakari na kuhakikisha kuwa wanasimamisha wagombea ambao wataweza kupigiwa kura na kupata ushindi katika chaguzi zijazo,” alisema Dk. Bana.
Aliongeza kuwa haiwezekani chama kitangaze sera zake na kushindwa kupigiwa kura kama hakuna kasoro zozote za uongozi ndani ya chama hicho.
“Ni wakati sasa umefika wa upinzani kubadili uongozi na kusimamia demokrasia ambayo itawasaidia kupata ushindi,” alisema Dk. Bana.
NEC yazungumzia Uchaguzi Mkuu 2020
NEC imesema uchaguzi huo umekuwa wa mafanikio kwa asilimia 95 na kwamba sasa itaanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 mapema ili iweze kufanya vizuri zaidi.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, alisema maandalizi hayo yataanza baada ya kukamilika kwa uchaguzi mdogo.
“Baada ya uchaguzi huu, tutaanza maandalizi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 ili tufanye vizuri zaidi.
“Tutajipanga mapema kwa maana ya wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi tutawaandaa mapema,” alisema Kailima.
Alisema katika maeneo mengi matokeo yalitangazwa kwa wakati isipokuwa Kata ya Isiyu iliyopo mkoani Singida yalichelewa hadi saa 9 usiku kutokana na jiografia ya eneo hilo.
“Uchaguzi huu umefanikiwa kwa asilimia 95, asilimia tano ni zile rabsha ndogondogo na dunia nzima lazima zinakuwepo, kwenye masuala ya uchaguzi haziwezi kukosekana, labda uchaguzi huo uongozwe na malaika,” alisema.
Kuhusu malalamiko ya baadhi ya vyama kuchezewa rafu, alisema si kweli kwani wana ushahidi wa baadhi ya wabunge ambao waliingilia uchaguzi huo na kuwaamuru mawakala waondoke.
“Hakuna ambaye ni mkamilifu, changamoto zilizotokea si za tume, kuingia kwenye uchaguzi ni hiyari na kujitoa ni hiyari.
“Taarifa za mawakala kuondolewa kwenye vituo si kweli, tuna ushahidi baadhi ya wabunge waliwaambia waondoke,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema pia waandishi wa habari wanapaswa kupata kibali cha kuripoti uchaguzi kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi.
Alisema kipengele cha 9 (15) kuhusu maelekezo ya wasimamizi wa uchaguzi, kinaeleza wazi kuwa waandishi wa habari wataruhusiwa kuripoti baada ya kupata idhini ya msimamizi wa uchaguzi.
“Huwezi kupata idhini ukiwa kwenye kituo cha kupigia kura, lazima uende kwanza kwa msimamizi wa uchaguzi, tukiacha tu kila mtu aingie je, tutakuwa na uhakika gani kama kila anayekuja ni mwandishi wa habari?” alihoji Kailima.
Habari hii imeandaliwa na PATRICIA KIMELEMETA, ASHA BANI, NORA DAMIAN (DAR ES SALAAM) NA SAFINA SARWATT (KILIMANJARO)