30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

BOMOAMOA TANESCO, WIZARA YA MAJI YAANZA

Na LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM

WIZARA ya Maji na Umwagiliaji na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), zimeanza uvunjaji wa majengo yake ili kupisha ujenzi wa barabara ya njia sita na barabara za juu (Fly over) za Ubungo.

Hatua ya kubomolewa kwa majengo hayo, ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa Novemba 11, mwaka huu.

Waliokuwa wa kwanza kuanza ubomoaji wa majengo yao jana saa moja asubuhi walikuwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kazi hiyo ilisimamiwa na Waziri Isack Kamwelwe.

Wakati wa uboamoji huo, tingatinga linalomilikiwa na Dawasco lenye namba za usajili SU 41706, lilianza kuvunja sehemu za mbele za uzio wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na baadhi ya majengo.

Wakati ubomoaji huo ukiendelea, MTANZANIA ilishuhudia baadhi ya watumishi wa wizara hiyo wakihangaika kuhamisha mafaili yenye nyaraka muhimu na vifaa vyao kwa kuvitoa nje ili visiweze kuharibika.

Akizungumza wakati wa uvunjaji huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Kamwelwe, alisema majengo yote ya wizara yake yaliyo katika hifadhi ya barabara yatabomolewa ndani ya wiki moja.

Alisema ili kuhakikisha ubomoaji huo unafanyika kwa wakati, aliwaagiza watumishi wote kuhakikisha wanahamisha vitu vilivyo kwenye majengo hayo ili kuruhusu kuvunjwa kwa majengo hayo.

“Hili ni zoezi la muda mrefu, lilianzia Kimara kwa wananchi kuvunjiwa, kwahiyo na sisi ni lazima tupishe, ndiyo maana nimeamua kuja mwenyewe kusimamia ubomoaji huu, jana (juzi) tumeshinda hapa tukihamisha vitu hadi saa 2:00 usiku.

“Hakuna sababu ya majengo yetu kukwamisha ujenzi wa barabara hiyo kwani tayari wizara imehamia Dodoma, kwa hapa Dar es Salaam hatuwezi kupata shida, Katibu Mkuu atafanya utaratibu wa kupata ofisi nyingine, lakini pia tunazo idara zilizo chini ya wizara kama Dawasa na Dawasco, tunaweza kutumia,” alisema Waziri Kamwelwe.

Alisema hifadhi ya barabara katika eneo hilo la Ubungo ni mita 182 ambazo ni sawa na mita 91 kila upande.

Uvunjaji wa majengo hayo umeanza ikiwa ni siku mbili tangu Rais Magufuli aliposisitiza kuvunjwa kwa majengo hayo Novemba 25, mwaka huu alipokuwa akifungua Hospitali ya Tiba na Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), Mloganzila.

 TANESCO WACHUKUA HATUA

Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), umesema kuwa umeanza utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, kuhusu kubomolewa kwa jengo la ofisi zao za makao makuu, liliopo Ubungo, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano cha Tanesco, ilieleza kuwa kuanzia jana wameanza kuvunja ukuta wa mbele wa jengo lao, huku baadhi ya watumishi wakianza kuhamishiwa katika ofisi zao nyingine ili kupisha shughuli za ubomoaji kufanyika kwa usalama zaidi.

“Uongozi wa shirika pamoja na Wakala wa Majengo (TBA) wanaendelea kufanya taratibu zitakazowezesha zoezi la ubomoaji wa jengo kufanyika bila kuathiri huduma kwa wateja wa shirika.

“Katika kipindi hiki cha utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais. Tunapenda kuwahakikishia wateja wetu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa huduma za umeme zitaendelea kupatikana kama kawaida ikiwamo huduma ya manunuzi ya Luku. Uongozi wa Shirika utaendelea kutoa taarifa kwa kadri zoezi hili linavyoendelea,” ilieleza taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles