33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CHADEMA ASHIKILIWA NA POLISI

Na MWANDISHI WETU-MOROGORO

POLISI mkoani  Morogoro wanawashikilia watu 41 akiwamo Mbunge wa Mlimba, Susan Kiwanga (Chadema), kwa tuhuma za kufanya fujo na kuchoma moto ofisi ya mtendaji   baada ya kutangazwa   matokeo ya udiwani katika Kata Sofi wilayani Malinyi.

Pamoja na kukamatwa kwa watu hao pia polisi wanamsaka Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema), ambaye anadaiwa kuhusika katika tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei  alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili   saa 5.00 usiku ambako viongozi hao walikwenda kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani.

Matei alisema wabunge hao na madiwani wawili wa Chadema kutoka Ifakara walionekana kuhamasisha vurugu.

“Watuhumiwa wanadaiwa kuchoma majengo ya umma ambayo ni ofisi ya Shule ya Msingi Sofi, nyumba ya walimu wa shule hiyo na ofisi ya mtendaji kata.

“Fujo na uharibu huo ulitokea baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo kuwa mgombea wa CCM ndiye alishinda kwa kupata kura 2,099,” alisema.

Alisema mgombea wa Chadema alipata kura 1,684 jambo lililopingwa na wafuasi wa chama hicho na kuanza vurugu.

Kamanda Matei alisema baada ya kuchoma majengo hayo kwa  petroli, walidhamiria pia kwenda katika zahanati lakini askari waliwakamata.

“Polisi inaendelea kuwatafuta watu wengine waliohusika na vurugu hizo, akiwamo mbunge Lijualikali. Watuhumiwa 41 wamepelekwa wilayani Ulanga kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” alisema.

Alipotafutwa, Mbunge Lijualikali,   alisema anashangazwa na taarifa hiyo.

Alisema wakati  matokeo yakitangazwa alikuwa nyumbani kwake Ifakara.

“Taarifa za kutafutwa na polisi ndiyo nazisikia kutoka kwako.

“Mimi binafsi baada ya kumalizika  kampeni Jumamosi nilirejea Ifakara kwa hiyo sijui chochote kuhusu hizo vurugu na nashangazwa kuhusishwa na tuhuma za aina hiyo.

“Na kama kweli natafutwa nitakwenda kujisalimisha polisi mimi mwenyewe,” alisema Lijualikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles