27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

CAG aibua utata makusanyo ya Sh bilioni 681

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema katika mwaka wa fedha wa 2018/19 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshindwa kuonyesha ushahidi wa kodi ya Sh bilioni 681.33 kama ilikusanywa kupitia Mfumo wa Kukusanya Mapato Kielektroniki (eRCS).

CAG amebainisha hayo kupitia ukaguzi wa mapato kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano ambao ulikuwa na lengo la kujua iwapo mapato hayo yanakusanywa kwa ufanisi.

Ukaguzi huo ambao ulijumuisha ripoti za mwaka 2015/16, 2016/17, 2017/18 na 2018/19 ulibaini kuwapo kwa matumizi duni ya mfumo wa kukusanya mapato kielektroniki na mwingiliano wa mifumo ya kielektroniki ya eRCS na Mfumo wa Uhakika wa Mapato ya Mawasiliano ya Simu (TRAS).

Aidha katika ukaguzi wake, CAG alibaini pia kutotumiwa vizuri kwa mifumo ya eRCS na TRAS kama vyanzo vya taarifa za uhakika ili kuthibitisha usahihi wa mapato ya kodi yaliyowasilishwa.

“Uchunguzi ulibaini kuwa mipango ya ukaguzi wa kodi ya TRA haikuwashughulikia watoa huduma wote wa mawasiliano ya simu katika kila mwaka wa fedha.

“Timu ya ukaguzi iligundua kuwa kulikuwa na utata wa taarifa kati ya mifumo miwili ya kielektroniki inayotumiwa ili kuhakikisha usahihi wa mapato ya kodi yaliyowasilishwa.

“Taarifa zilizotolewa na eRCS zilitofautiana na TRAS kinyume na matarajio ya kuanzishwa kwa mifumo hiyo. Kutokana na hali hiyo, ilikuwa vigumu kuthibitisha taarifa za kweli, hadi wakati wa kuandika ripoti hii ya ukaguzi hakukuwa na maridhiano baada ya kulinganisha mifumo hiyo miwili,” alisema Kichere.

Suala lingine lililobainika katika ukaguzi huo ni matumizi duni ya taarifa kutoka TRAS ili kuthibitisha uhalali wa mapato na ushuru kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano.

Pia ilibainika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano haijafuatilia vizuri utendaji wa TCRA katika kudhibiti sekta ya mawasiliano ili kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano.

MCHANGO PATO LA TAIFA

CAG alisema licha ya Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo ya Miaka Mitano (2016/17 – 2020/2001) kutazama mawasiliano kama moja ya sekta muhimu katika mchango wa Pato la Taifa (GDP), lakini mchango wa sekta hiyo umebaki asilimia 1.5 mwaka 2018 kama ilivyokuwa mwaka wa 2017.

“Shughuli za habari na mawasiliano zikijumuisha huduma za mawasiliano ya simu zilirekodi kiwango cha ukuaji wa asilimia 9.1 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 6.2 kwa mwaka 2017, lakini Pato la Taifa lilibaki asilimia 1.5 mwaka 2018 kama ilivyokuwa mwaka wa 2017 licha ya kuripotiwa ukuaji wa sekta katika mwaka 2018,” alisema Kichere.

Alifafanua kuwa ukaguzi huo umesukumwa na mchango usio sawa wa sekta hiyo kwa Pato la Taifa kwani katika mwaka wa 2014, 2015 na 2016 ulikuwa kwa asilimia 2 na ulipungua hadi asilimia 1.5 mwaka 2017 na 2018 licha ya kuripotiwa ukuaji wa sekta katika mwaka wa 2018.

“Mapato kutokana na miamala ya fedha za simu yaliongezeka kwa Sh trilioni 8 kwa robo ya Juni 2019, na kuhamasisha uhitaji wa kuelewa ni kwa kiwango gani Serikali inakusanya mapato kutoka katika sekta hiyo.

 “Kwa hiyo, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iliona umuhimu na unyeti wa kukagua eneo hili ili kutathmini jinsi Serikali kupitia TRA na TCRA ilivyofanikiwa kukusanya mapato kwa ufanisi kwa watoa huduma za mawasiliano,” alisema.

WATUMIAJI SIMU ZA MKONONI

Kulingana na ripoti hiyo, hadi kufikia Desemba 2019 watumiaji wa simu za mkononi walifikia milioni 47.7 idadi ambayo imepanda kutoka milioni 2.96 mwaka 2005.

Aidha ripoti za TCRA zinaonyesha hadi kufikia Juni 2019, miamala ya fedha kupitia simu za mkononi ilifikia Sh trilioni 8.31 ikiongezeka kutoka Sh trilioni 7.44 (Mei 2019).

USHAURI

Kichere alisema licha ya juhudi za Serikali kupitia TRA kuboresha ukusanyaji wa mapato kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano, hatua zaidi zinahitajika kwa uboreshaji.

“Matokeo yaliyowasilishwa katika ripoti hii yanaonyesha kwamba bado kuna mianya ambayo inasababisha upotevu wa mapato ya Serikali kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano.

“TRA, TCRA hazijafanya kazi ipasavyo kuhakikisha kuwa mapato kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano yanakusanywa kwa ufanisi,” alisema Kichere.

Aidha alisema wizara ilishauriwa kusimamia vyema utendaji wa TCRA ili kudhibiti sekta ya mawasiliano kwa ajili ya kuongeza makusanyo ya mapato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles