Maregesi Paul
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, ameeleza jinsi ukaguzi wa hesabu za serikali ulivyogundua mambo mbalimbali ya ubadhirifu wa fedha za umma katika mwaka wa fedha wa 2017/18.
CAG amesema hayo mjini Dodoma leo Jumatano Aprili 10, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ripoti yake kuwasilishwa bungeni leo asubuhi.
Katika maelezo yake, CAG ameeleza jinsi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilivyonunua gari lenye thamani ya Sh milioni 127 na jina la gari hilo kusajiliwa kwa jina la mmoja wa viongozi wake badala ya jina la Bodi ya Wadhamini.
Aidha, CAG Assad pia amefafanua namna Chama cha Mapinduzi (CCM) kisivyowasilisha fedha katika mifuko ya jamii makato ya mishahara ya wafanyakazi wake.
Pamoja na mambo mengine, CAG pia amebainisha baadhi ya taasisi za umma ikiwamo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jeshi la Polisi na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zilivyotumia vibaya fedha za umma katika mwaka huo wa fedha.