BANJUL, GAMBIA
MKUU wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Gambia, Alieu Momar Njie, amekimbilia nchi jirani ya Senegal akihofia vitisho dhidi yake.
Hatua hiyo imekuja mwezi mmoja baada ya kutangaza kuwa Rais Yahya Jammeh ameshindwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba Mosi mwaka jana.
Mmoja wa jamaa zake ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa Njie alikimbia baada ya kupata taarifa kuwa Serikali ilikuwa ikipanga njama dhidi yake na wengine katika tume anayoiongoza.
Mtu huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama, amesema wajumbe wengine wa tume hiyo pia wameikimbia nchi.
Hata hivyo, hakueleza namna Njie na wajumbe wengine walivyoondoka.
Njie alimtangaza mgombea wa upinzani, Adama Barrow kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Desemba, mwaka jana na kuzitaka pande zote kuyaheshimu matokeo.
Awali, Rais Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 22 aliyakubali matokeo hayo, lakini baadaye alibadilisha mawazo na kupeleka malalamiko mahakamani.
Kabla ya hapo, vikosi vya usalama viliizingira ofisi ya Tume ya Uchaguzi na kuwakatalia watumishi kuingia ofisini kwa wiki kadhaa. Hata hivyo wanajeshi hao wameshalihama eneo hilo.