Na MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Madini, Doto Biteko, amekitaka Chama cha Wachimbaji Wadogo nchini kuisaidia Serikali kufichua uovu unaofanywa na baadhi ya wachimbaji wasio waaminifu, wakiwamo wanaoshiriki utoroshwaji wa madini ya aina mbalimbali.
Biteko alisema hayo jana mkoani Shinyanga, alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha kazi, mara baada ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani hapo.
Alisema wachimbaji wadogo na wakubwa kote nchini wanapaswa kujibainisha katika ulipaji kodi, kwani kufanya hivyo kutaimairisha utendaji na kuongeza pato la Taifa.
Naibu waziri huyo alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, pamoja na majukumu ya kusimamia sekta nyingine, atilie maanani kwenye Sekta ya Madini, ili mchango wa Sekta hiyo kwenye pato la taifa uweze kufikia asilimia 10 kutoka asilimia 4 ya sasa.
Alisema pia Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa ni vema waendelee kuwalea wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa, katika utekelezaji wa Sheria ya Madini na kanuni zake.
Aliwataka viongozi wote wa mkoa kutoogopa migogoro katika Sekta ya Madini na badala yake waikabili na kuitatua katika njia zilizo sahihi.
Katika ziara yake hiyo, leo Biteko anatarajiwa kuzungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Mwazimba na wachimbaji wadogo wa kikundi cha Kasi Mpya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa, Telack, alimweleza Biteko kuwa mkoa wake umejipanga kusimamia vema sekta hiyo, kwani ni nguzo ya uchumi wa Mkoa wake pia.
Aliiomba Wizara ya Madini kuendeleza ushirikiano na ofisi yake ili kuongeza tija katika usimamizi wa Sekta ya Madini.